Habari

Fatma Karume: Nitafanya mambo haya TLS

By Florence Majani – Mwananchi
Monday, April 16, 2018

Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume ametaja mambo matano ambayo atayafanyia kazi baada ya kuchaguliwa kuongoza chama Jumamosi mjini Arusha.

Pia, binti huyo wa rais mstaafu wa Zanzibar amesema ataendeleza yale yaliyofanywa na mtangulizi wake, Tundu Lissu, ikiwamo kusimamia demokrasia, haki, utawala bora, haki za wanasheria pamoja na kubaini sababu za kuchunguza sababu za watu kutotaka kufanya kazi hiyo.

Katika uchaguzi huo, Fatma alipata kura 820 akimzidi Godwin Gwilimi aliyepata kura 363, Godwin Mwalongo (12) na Godfrey Wasonga (6).

Fatma pia alisema TLS itahoji mamlaka ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Upelelezi (DPP), kuhakikisha wanasheria wanashirikishwa katika utungaji wa sheria na ada za uanachama wa TLS.

Akizungumza na Mwananchi jana, Fatma ambaye pia ni mtoto wa rais sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema jambo la kwanza atakalofanyia kazi ni kubadili hali ya wanasheria nchini.

“Nataka kujua kwa nini hawataki kufanya kazi za uwakili. Kuna tatizo hapa la kwa nini wanasomea kazi hii lakini hawataki kuifanya. Nataka tutafute sababu,” alisema.

Alisema wanachama wa TLS waliofanya kazi za uwakili kwa mwaka 2016 walikuwa 2,931 lakini mwaka huu, yaani 2018 ni 2,270. Fatma alisema TLS imepoteza wanachama 661 waliokuwa wanafanya kazi za uanasheria.

“Tukumbuke mwaka huu na mwaka jana kumetokea nini? Ofisi za (kampuni ya uwakili ya) Immma zilishambuliwa kwa bomu, ofisi za wanasheria wengine zimeshambuliwa na wengine wamewekwa selo bila makosa, lakini pia (aliyekuwa) rais wa TLS alipigwa risasi,” alisema.

Fatma, ambaye pia ni mwanasheria wa kampuni ya Immma, alisema hata kama Serikali itasomesha vijana wengi kuwa wanasheria, kama mazingira ya kazi yatabaki kuwa ya vitisho na mashambulizi, wengi wataiacha taaluma hiyo.

“Kwa maana hiyo wananchi ndio wataathirika. Hii ni changamoto kubwa sana,” alisema.

Jambo la pili ambalo Fatma alisema atalifanyia kazi akiwa TLS ni kuhoji namna DPP anavyotumia madaraka yake.
Alisema DPP amekuwa akiwakamata watu na baadaye kuwanyima dhamana au kuendelea kuwashikilia akidai kuwa upelelezi haujakamilika.

“Inakuwaje anawakamata watu wakati upelelezi haujakamilika?…Watu wakiomba kudhaminiwa anasema wasidhaminiwe. Anaiambia mahakama hakuna kutoa dhamana, hii ina maana anatumia madaraka yake vibaya,” alisema Fatma

“Mpaka sasa unajua ni wanasheria wangapi wapo ndani na kesi zao hazijasikilizwa na hawajapewa dhamana?…TLS isimamie suala hili kwa nguvu sana, kuhusu namna anavyotumia madaraka yake vibaya.”

Alisema zamani TLS ilipuuza suala hilo, lakini kwa sasa limekuwa kubwa na wameona walifanyie kazi kwa kina.

Kadhalika, Fatma amesema suala la tatu ni kuhakikisha wanasheria wanashirikishwa katika shughuli za kutunga sheria.

“Lazima tushirikishwe kwa sababu sisi ni wadau na tuna wajibu wa kutazama sheria, kuangalia hii inafaa na hii haifai, hii itamuumiza huyu,” alisema Fatma.

Kuhusu suala la ada za uanachama wa TLS, Fatma alisema hakuna haja ya kuzishusha kwa sababu hilo si tatizo linalosababisha wanachama kuacha kufanya kazi za uanasheria.

“Hatutapunguza ada, baraza kuu limeamua kuwa ni bora ada kubaki vilevile. Mungu akijalia tutamaliza mwaka salama na ninataka kuhakikisha kwamba tunawavutia watu kuingia katika taaluma hii kwa sababu (kwa sasa) imeharibiwa,” alisema.

Kuhusu kufuata nyayo za Lissu, mwanasheria huyo alisema mbunge huyo wa Singida, Mashariki (Chadema) ni kiongozi aliyesimamia utawala bora, haki na haki za wanasheria, hivyo na yeye anakwenda kusimamia hayo.

Kuhusu kanuni za uchaguzi za TLS, Fatma alisema, juzi baraza la kuu la chama hicho lilikubaliana kwamba alichokifanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ni uvunjaji wa sheria.

Machi 10, 2018, TLS ilidai kuwa ofisi ya AG imeongeza masharti katika mabadiliko ya kanuni za uchaguzi wa chama hicho, yanayowanyima fursa watumishi wa umma na wanasiasa kuwania uongozi wowote wa chama hicho.

Fatma alisema wanachama zaidi ya 1,500 wa baraza kuu la chama hicho walikubaliana kuwa AG alivunja sheria. Hata hivyo hakutaka kusema hatua ambazo TLS inachukua.

Nguvu ya TLS

Katika mahojiano hayo, Fatma alisema nguvu ya TLS ni kuwa na ujuzi akisisitiza vijana wanaposomeshwa na kufikia hatua ya kufuta ujinga, hiyo ndiyo nguvu.

“Mwalimu Nyerere alisema kuna maadui watatu – umaskini, ujinga na maradhi, kwa hiyo ukifika TLS basi umefuta ujinga,” alisema.

Alizungumzia pia suala la muda wa urais wa TLS akisema watu wengi wanataka muda wa uongozi ambao ni mwaka mmoja, fatma alisema unatosha.

“Hii ni kazi ya kujitolea, utakula nini? Mimi siungi mkono kuongeza muda, hiyo ni sababu na pingamizi kubwa la kuongeza muda,” alisema Fatma.

Mpango wa kuwa Rais

Tofauti na familia nyingine za wanasiasa, Fatma anasema hana mpango wa kuingia kwenye siasa wala kuwania urais wa Zanzibar kufuata nyayo za baba na babu yake.

“Nchi hii ina mihimili mitatu, mhimili wa kwanza ni Serikali, Bunge na Mahakama. Moyo wangu upo kwenye mhimili wa sheria,” alisema Fatma na kusisitiza “Sitaki kuingia kwenye serikali…sheria kwangu mimi, ni wito.”

Amiminiwa Pongezi

Wakati Fatma akieleza maono yake, wanasheria pamoja na viongozi wa Serikali wamemtumia salamu za pongezi, wengi wakitumia mitandao ya kijamii, ambayo ilianza kutuma picha zake jana jioni kabla ya matokeo kutangazwa.

Miongoni mwao ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyeandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema:

“Nachukua fursa hii kwa dhati ya moyo wangu kuwapongeza Fatma Karume na Omar Said Shaaban kwa kuchaguliwa kuongoza Tanganyika Law Society na Zanzibar Law Society….Sina chembe ya wasiwasi juu ya uwezo wao na nawatakia kila la kheri.”

Wengine ni mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT), Zitto Kabwe. Pongezi hizo pia zilitolewa na wanasheria wenzake wakimtaja kama wakili aliyebobea na mchapakazi.

Wakili Magdalena Sylister alisema ana matumaini makubwa na mwanasheria huyo kutokana na uzoefu wa muda mrefu katika kazi ya uwakili pamoja na uongozi na kuwa ni mtu sahihi katika kipindi hiki kuongoza taasisi hiyo.

“Wakili Fatma ni mchapakazi, anaipenda taaluma ya sheria na amejitolea kupigania utawala bora unaozingatia sheria na haki za binadamu. Niwaombe viongozi wa TLS na wanachama kwa ujumla tumpe ushirikiano,” alisema Magdalena.

Akizungumzia siri ya ushindi wake, alisema unatokana na ushawishi alionao wa kutetea haki na usawa na kwamba vitu hivyo viliwavutia wapigakura wengi hasa vijana ambao idadi yao imekuwa ikiongezeka na mara nyingi wana shauku ya mabadiliko.

Kwa upande wake, Andrew Akyoo alisema ushindi wa Fatma umekuja wakati muafaka katika kipindi ambacho mwanamke mwenye uwezo anapaswa kuongoza taasisi hiyo pekee ya wanataaluma ambayo ilianzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 1961.

“Ushindi wake uwe chachu kwa wanawake wenzake kuwa wanaweza kuonyesha vipawa vyao vya kiuongozi na kuaminiwa kutokana na ushawishi wao katika kujenga jamii inayozingatia utawala wa sheria na kuvumiliana,” alisema Akyoo.

Wakili Leah Reginald kutoka Iringa, alisema wamempata mwanasheria mbobezi, mtetezi wa haki za binadamu na utawala wa sheria ambaye wanamtarajia kuonyesha uwezo wake kiuongozi sio tu kwa mawakili wenzake, bali kwa jamii nzima.

Nyongeza na Ibrahim Yamola

Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi amesema ‘uchaguzi umemalizika, tumpe ushirikiano Fatma Karume na viongozi wengine waliochaguliwa.’

Ngwilimi ameyasema hayo Jumatatu, Aprili 16, 2018 kupitia waraka alioutoa akizungumzia masuala mbalimbali likiwamo mwelekeo wake baada ya kushindwa uchaguzi huo wa TLS.

Alisema uchaguzi wa TLS uliofanyika Aprili 14, 2018 ulikuwa wa kidemokrasia na bila dosari yoyote ile hadi ukawapata viongozi wake, ambao ni rais, makamu, wajumbe wa baraza la uongozi watakaoongoza kwa mwaka mmoja hadi 2019.

“Katika uchaguzi huo, mimi (Ngwilimi) niligombea nafasi ya urais, mwisho wa siku wakili mwenzetu Fatma Karume alichaguliwa kwa kura nyingi kuchukua nafasi hiyo kubwa na yenye heshima ya pekee si tu kwa mawakili, lakini pia katika mfumo na tasnia ya sheria na uwakili na sheria hapa nchini na kimataifa,” alisema Ngwilimi

Nyongeza na Muhammed Khamis

Wakati Fatma Karume akichaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mjini Arusha, Jumamosi, Aprili 14, 2018 siku hiyo hiyo, Omar Saidi Shabani alichaguliwa tena kuendelea kuongoza Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kwa awamu nyingine.

Omar alishinda urais bila kupingwa katika uchaguzi huo pamoja na katibu wake, Rajab Abdallah baada ya kuwa wanachama peke yao waliojitokeza kugombea nafasi hizo.

Baada ya kuchaguliwa alisema kutokupingwa kwake kunaonyesha dhahiri kuwa mawakili wenzake wanamwamini na kuukubali utendaji wake.

 

Tagsslider
Share: