Habari

Fatma Karume Rais mpya wa TLS


Uongozi na wasomaji wa Mzalendo.Net wanatoa hongera za dhati kwa Rais Mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Fatuma Karume kwa kupata ushindi wa kishindo wa chama hicho.

Kadhalika, wanamtakia Kila la kheri, ufanisi na mafanikio katika kusimamia vyema majukumu yake kwa uadilifu na kuongeza ujasiri katika kupambana na changamoto zinazomkabili mbele yake na uongozi wa TLS .

Tunaamini kwamba TLS itazidi kuwa imara yenye kuzingatia misingi ya haki na sheria kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, wakili nguli, Tundu Lissu.

Tunamuomba Mola wetu mtukufu, amsaidie na mlinde na shari zote za wanaojifanya kuwa na nguvu, rais mpya wa TLS, Wakili Fatma Karume.

Sources: Mitandao ya Kijamii/Magazeti.
Jumapili, April 15, 2018

Wakili Mwandamizi, Fatma Karume amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), akichukua mikoba kutoka kwa Tundu Lissu (Mb) ambaye amemaliza muda wake wa uongozi.

Wakili Fatma Karume amechaguliwa kwa kura 820 akifuatiwa Godwin Ngwilimi aliyepata kura 363, Godwin Mwapongo 12 huku, Godfrey Wasonga akipata kura 6.

Fatma Karume, ambaye ni mwanachama wa TLS kwa muda mrefu, lakini pia ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar (awamu ya sita), Amani Abeid Karume. Wakili Fatuma, Juni 15 mwaka huu atakuwa na umri wa miaka 49.

Zoezi la kupiga na kuhesabu kura lilianza tangu asubuhi jana Jumamosi, Aprili 14 mjini Arusha na lilikamilika baadaye jioni huku, Wakili huyo akiibuka mshindi.

Katika uchaguzi huo, Dk Rugemeleza Nshala amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TLS. Uongozi wa TLS hudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Fatma ni nani?

Fatma Karume alizaliwa Juni 15, 1969 Zanzibar.

Ni mtoto wa Rais Mstaafu wa Zanzibar (awamu ya sita), Amani Abeid Karume.

Ni mjukuu wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume.

Ni mwanasheria katika kampuni ya uwakili ya IMMA Advocates

Ni mwanzilishi wa kampuni ya uwakili ya ‘Karume and Co Advocates 2004.’

Fatma amewahi kuwa wakili wa mwanasiasa Tundu Lissu katika kesi yake ya uchochezi, Julai mwaka jana.

Ofisi za kampuni ya uwakili ya IMMMA zilizopo Upanga, mjini Dar es Salaam, ziliungua moto Agosti mwaka 2017.

Tagsslider
Share: