Habari

Futari ya pamoja mkoa wa kusini Pemba

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akibadilishana mawazo na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi (katikati), baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Maalim Seif kwa wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba huko ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Chake Chake Pemba.

MKOA WA KUSINI PEMBA,11/08/2012.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka waislamu nchini kuendeleza utamaduni wa kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kijamii, ili kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao.

Makamu wa Kwanza wa Rais ametoa wito huo huko ukumbi wa kiwanda cha makonyo Wawi, katika hafla ya futari ya pamoja aliyoiandaa kwa ajili ya wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema kitendo cha kufutari kwa pamoja ni cha kihistoria na utamaduni bora unaohitaji kuendelezwa katika kudumisha umoja, mapenzi na mshikamano miongoni mwa wanajamii, na kuurithisha utamaduni huo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Maalim Seif amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba kwa kuungana nae katika futari hiyo, na kuwataka kuendeleza utamaduni huo, ikiwa ni hatua muhimu ya kurithisha utamaduni bora kwa vijana.

Mapema akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Sheikh Nassor Ali Ghulam amemshukuru Maalim Seif kwa uamuzi wake wa kuwakutanisha wananchi wa Mkoa huo na kufutari nao, jambo ambalo linapasa kuendelezwa.

Sheikh Ghulam ametoa wito kwa waislam kuishukuru neema ya uhai waliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu, na kuwataka kuzidisha ibada hasa katika kumi hili la mwisho la mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Futari hiyo ya pamoja imewajumuisha wananchi na viongozi mbali mbali wa serikali na dini akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi.

Picha zote na Hassan Hamad (OMKR) kwa hisani ya Salma Said

Tagsslider
Share: