Habari

Gwajima alaani Lissu kupigwa risasi

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima

Waandishi wa Mwananchi
Sunday, September 10, 2017

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hatasita kukemea uhalifu nchini likiwemo tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Gwajima amesema hayo Jumapili asubuhi, 10/9/17 wakati wa ibada maalumu ya kumuombea Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi siku ya Alhamisi, 7/9/17 nyumbani kwake Area D, Dodoma na watu ambao hawajajulikana.

Lissu ambaye alianza kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa mjini Dodoma, kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan Nairobi, Kenya.

Gwajima: “Naomba tusimame kidogo nizungumze jambo, nimesema leo nitakuwa na ibada maalumu ya kumuombea Lissu. Somo langu la leo linasema damu isiyo na hatia,” amesema akizungumza na waumini.

Gwajima amesema kama kiongozi wa dini hatasita kukemea tukio lililomfika Lissu na kwamba, anashangaa viongozi wenzake wa dini kukaa kimya.

Amesema neno la Mungu linasema atakayemwaga damu ya mwanadamu mwenzake naye damu yake itamwagika vivyo hivyo: “Damu inayomwagika chini ya ardhi ina sauti, inamlilia Mungu,” amesema Gwajima.

Mchungaji Josephat Gwajima amesema Jumatatu tarehe 11/9/17 atakwenda Nairobi, Kenya kumuona Tundu Lissu aliyelazwa kwa matibabu. ‘twitter’

Awali, wanakwaya wa kanisa hilo waliimba wimbo maalumu wa kumuombea Lissu wakihamasisha taifa lote kufanya hivyo.

“Amani ya Tanzania inapotea, wasione tuko kimya… kwa nini haya yanatokea na watu wasiyojulikana… Watanzania wote tumuombee Lissu,” Waumini kupitia wimbo maalumu wamehimiza Watanzania, kumuombea Lissu.

Mdogo wake Lissu azungumza kanisani kwa Gwajima

Vincent Lissu, mdogo wake Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kabla ya kaka yake kushambuliwa kwa kupigwa risasi aliwaeleza kwamba kuna mtu anafuatilia gari lake. Vincent Lissu amewaomba Watanzania waendelee kumwombea kaka yake.

Akizungumza wakati wa ibada ya kumwombea Lissu iliyofanyika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima Jumapili, Septemba 10, 2017 amesema alimwona kaka yake akiwa amelala kitandani hospitalini mwili ukiwa na damu.

Amesema alipoamka asubuhi 10/9/17 alielezwa na mtu kuwa kuna ibada maalumu ya kumwombea Lissu, hivyo akaamua kuhudhuria katika kanisa hilo la Mchungaji Josephat Gwajima.

Vincent amesema baada ya kaka yake kushambuliwa siku ya Alhamisi, alienda Dodoma na kwamba anawashukuru madaktari waliofanya kila waliloweza kuokoa maisha ya kaka yake.

Amesema kaka yake ni mpenda haki tangu akiwa mdogo na amewaomba wananchi wazidi kumuombea, apone.

Msigwa awashangaa viongozi wa dini kukaa kimya kuhusu Lissu

Naye, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema anashangazwa na viongozi wa dini kukaa kimya juu ya kujeruhiwa kwa Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki).

Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa amesema anashangazwa na viongozi wa dini kukaa kimya juu ya kujeruhiwa kwa Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki).

Msigwa ambaye yuko Nairobi na viongozi wengine wa CHADEMA, waliomsindikiza Lissu aliyepigwa risasi na watu ambao hawajuilikani akitokea bungeni ametuma kwenye ‘Twitter’ kwamba anawashangaa viongozi wa dini kukaa kimya mpaka sasa.

‘’Inanishangaza kuona viongozi wa dini mpaka sasa wamekaa kimya juu ya kujeruhiwa kwa Lissu!. Na mwenendo wa siasa za Tanzania!’’amesema Msigwa kwenye ujumbe wake wa Twitter.

Maalim Seif: Hili la Lissu halijawahi kutokea. “Ufanyike mkutano wa pamoja wa mashauriano wa kitaifa ili kuepusha mgawanyiko. Ametoa shauri hilo siku ya Ijumaa, Septemba 8, 2017.

Katibu Mkuu wa CUF,  Maalim Seif Sharif Hamad amesema amesikitishwa kwa kushambuliwa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu tukio alilosema halijawahi kutokea Tanzania.

Amesema anampa pole Lissu na  kumwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie afya na kupona haraka ili aendelee na kazi yake ya  kuwatetea wananchi.

Pia, kutetea haki na utawala wa sheria na  kupambana na dhuluma, uonevu na hasa dhidi ya wanyonge. Ameshauri kufanyika mkutano wa mashauriano kitaifa ili kuepusha mgawanyiko.

“Tukio hili ni la kusikitisha, ni ushahidi mwingine unaoonyesha nchi yetu inaelekea kubaya. Hali hii inapaswa kudhibitiwa,” amesema Maalim Seif.

Maalim Seif amesema hayo siku ya Ijumaa, 8/9/17: “Bila hatua madhubuti kuchukuliwa za kuiepusha nchi na chuki na kulipizana visasi miongoni mwa wananchi, mambo hayo husababisha machafuko.”

Katibu Mkuu huyo wa CUF aliyewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema pamoja na kauli za serikali kuwa inawasaka wahalifu, anaisihi  itumie uwezo wake wote kuwatia mikononi watu waliohusika katika kipindi kifupi kijacho ili wananchi waimarishe imani yao kwa serikali.

Amesema kuna haja ya uongozi wa Tanzania kuandaa na kuitisha mkutano wa mashauriano ya kitaifa ili kushauriana namna ya kuzuia mgawanyiko nchini.

“Nampa pole Lissu na familia yake, uongozi wa CHADEMA na wananchi wa Singida Mashariki, pia wananchi wote walioguswa na shambulio hili la kikatili,” amesema Maalim Seif.

Lissu aliyeshambuliwa kwa kupigwa risasi tano, mbili kwenye miguu, mbili tumboni na moja mkononi anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, mjini Nairobi, Kenya alikopelekwa tangu Alhamisi usiku, Septemba 7, 2017.

Rais Magufuli ateua Jaji Mkuu
Wakati huo huo, Rais John Magufuli amemteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema uteuzi huo unaanza leo Jumapili, Septemba 10, 2017.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Juma alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu mwezi wa Januari, 2017 baada ya kustaafu Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman.

Ikulu imesema Jaji Mkuu ataapishwa kesho Jumatatu saa nne asubuhi, Ikulu mjini Dar es Salaam. Rais Magufuli Januari 17, 2017 alimteua Profesa Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu. Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo, Profesa Juma alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande hadi kufikia Januari Mosi alikuwa ameshafikisha miaka 65 ambayo ni ya kustaafu Majaji wa Mahakama ya Rufani kama ilivyobainishwa katika Ibara ya 120 ya katiba ya mwaka 1977.

Jaji Chande aliteuliwa katika nafasi hiyo na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2010 akichukua nafasi ya Jaji mstaafu Augustino Ramadhani.

 

Share: