Michezo

MAKOCHA WATANGAZIWA AJIRA TIMU ZA TAIFA ZA VIJANA ZANZIBAR, WATAKIWA KUOMBA NAFASI HIZO

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Kamati ya Makocha wa Soka Visiwani Zanzibar ambayo imepewa dhamana na ZFA ya kuteuwa Makocha wa timu za Taifa za Vijana imetangaza nafasi za Makocha wanohitaji kuwa makocha wa timu za Taifa za Vijana Zanzibar chini ya umri wa miaka 14, 17 na 20 ambapo wametakiwa kwenda kuchukua fomu ya kuomba maombi hayo.

Akizungumza na Mtandao huu Katibu wa Kamati ya Makocha Visiwani Zanzibar Ibrahim Makeresa amesema kocha yeyote anaehitaji kuwa kocha mkuu au msaidizi wa timu hizo za vijana kwenda Afisini kwao kuchukua fomu na ikiwa atakidhi vigezo atapewa nafasi hiyo.

Ameelezea lengo la kutoa fomu maalum kwa makocha hao ni kuondoa malalamiko kwa baadhi ya wadau ambao mara nyingi wanalalamika kuwa makocha wa timu hizo wanateuliwa kwa upendeleo, ambapo amesisitiza kuwa mwenye sifa aombe kisha watachaguliwa kwa kuepusha malalamiko hayo.

“Unajua miaka ya nyuma akitangazwa kocha wa timu za vijana kuna kuja maneno mengi kwamba labda nafasi hizo zinakwenda kwa watu maalum, sasa kwa kuepusha hayo tutatoa fomu maalum kisha makocha waombe na akikidhi vigezo atachaguliwa ikiwa kocha mkuu au msaidizi”. Alisema Makeresa.

Fomu hizo za kuombea nafasi za ukocha kwa timu za Vijana zinatarajiwa kuanza kutolewa kuanzia Alhamis ya Mei 25, 2017 na mwisho wa kuzipitia fomu hizo itakuwa June 5, 2017 ambapo sifa kubwa ya kuwa kocha wa timu hizo, kocha anatakiwa kuwa na sifa ya ukocha kuanzia Leseni “C” ambayo inayotambuliwa na shirikisho la soka Barani Afrika na pia sifa nyengine kocha anatakiwa awe hajapatikana na hatia ya udhalilishaji kwa watoto (Wachezaji).

Zazninews

Share: