Michezo

Olimpik ya walemavu – Gombani Pemba

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimvisha nishani kijana Mohd Khamis mwenye ulemavu wa akili baada ya kupata ushindi katika michezo ya Special Olimpik kwa ajili ya watu wenye ulemavu yaliyofanyika Morogoro. Hafla hiyo ilifanyika uwanja wa michezo Gombani Pemba.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekabidhi nishani mbali mbali kwa vijana wenye ulemavu wa akili kisiwani Pemba.

Vijana hao walijinyakulia jumla ya nishani nane zikiwemo 3 za dhahabu, 4 za fedha na moja ya shaba, baada ya kushinda katika michezo ya Special Olimpic yaliyofanyika mkoani Morogoro. Michezo hiyo ni pamoja na riadha na mpira wa miguu.

Akikabidhi nishani hizo huko uwanja wa michezo gombani kisiwani Pemba, Maalim Seif amesema michezo ni ni muhimu kwa watu wenye ulemavu wa akili na itaweza kuwa tiba mbadala kwao kutokana na kusaidia kuwakuza vizuri kimwili na kiakili.

Amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu wa akili na badala yake wawatoe na kuwashaiisha kushiriki michezo ambayo huwafanya kujiona huru wakati wanaposhiriki na kuchanganyika na watu wengine.

“Tumeambiwa hapa kuwa baadhi ya watu hawa wenye ulemavu wa akili tayari wameoa na wengine kuolewa na watoto wao hawana ulemavu kabisa, na kwamba hali imejitokeza baada ya vijana hao kushiriki michezo, huku wengine wakiajiriwa” alisema Maalim seif.

Amepongeza hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ya kuanzisha Elimu Mjumuisho ambayo hutoa fursa kwa vijana wenye mahitaji maalum kuchanganyika na wengine na kujiona wako huru wakati wanapojifunza.

Makamu wa Kwanza wa Rais ametumia fursa hiyo kuwaomba watu wenye uwezo wakiwemo wafadhili wa michezo kukisaidia chama hicho ili kukiwezesha kufanya shughuli zake vizuri kwa lengo la kukuza vipaji kwa watu wenye ulemavu wa akili.

Vijana waliopata medali hizo ni Asha Hassan Mussa, Mohd Khamis, Khamis Ali Faki, Hamad Haji na Harith Khamis Ismail ambae alipata medali nne.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, katibu wa chama cha Special Olimpik Tanzania kanda ya Pemba bibi Mashavu Juma Mabrouk amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, chama hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo ukosefu wa vifaa vya michezo.

Hassan Hamad (OMKR).

Share: