Michezo

Rasimu ya Katiba mpya ya ZFA kutolewa karibuni

August 15, 2018

NA AMEIR KHALID

KAMATI teule iliyoteuliwa ya chama cha soka Zanzibar ZFA imesema bado inaendelea na mchakato wa Katiba ya ZFA, ambayo si muda mrefu itatolewa kwa wadau ili kutoa mapendekezo yao kabla ya kupitishwa rasmi.

Katibu wa kamati hiyo Khamis Abdalla Saidi amesema bado kamati inaendelea na jukumu lake la kusimamia upatikanaji wa katiba ya ZFA ambayo rasimu yake ipo chini ya wanasheria kwa sasa.

Alisema mchakato wa katiba ndani ya kamati hiyo haupo kimya kama watu wengi wanavyodhani, ila kwa sasa bado jopo la wataalamu linaendelea na majukumu yake ya kusimamia chombo hicho muhimu kwenye soka la Zanzibar.

“Tunaunga mkono juhudi zilizofanywa na viongozi wa ZFA waliopita katika kusimamia mpira wa Zanzibar, tayari rasimu ya katiba ipo na iko katika marekebisho muda si mrefu italetwa kwa wadau”alisema.

Kwa upande mwengine alisema rasimu hiyo bado inatakiwa kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya vifungu, ili kupata katiba nzuri ambayo italeta matumaini kwa wadau wa mpira Zanzibar.

“Tunatarajia ikimaliza rasimu hiyo itawafikia wadau wote wa mpira wa miguu na washabiki ikiwemo wachezaji wa zamani na wandishi wa habari ili kutoa maoni yao katika kutengeneza mpira wa Zanzibar kwa pamoja’’alisema.

Hata hivyo alisema kamati yao haifanyi kazi na makundi yoyote ya watu wala shindikizo fulani, lakini ipo tayari kushirikiana na mtu yeyote kwenye masuala ya mpira wa Zanzibar ili kuleta umoja kwenye mpira wa Zanzibar.

Kuhusu utendaji wa kamati hiyo alisema kuwa wanaendelea vyema na majukumu yao makubwa waliyopewa katika kuendesha soka la Zanzibar katika kipindi hiki cha mpito, ikiwemo kusimamia ligi hatua ya nane bora pamoja na ligi ya mabingwa wilaya ambazo zote zinaendelea vyema.

Hata hivyo alisema kuwa wataendelea kuwa makini katika kufuatilia vitendo vya waamu ambao tayari baadahi yao wameanza kulalamikiwa kutokana na uchezeshaji wao na kuahidi kuwa haitamvumilia mwamuzi yeyote anayevunja sheria za soka.

Pia alisema kuwa hivi sasa kamati imeanza kutafuta fedha na wadhamini ili kuendelea kusaidia uendeshaji wa soka la Zanzibar, kwani hivi sasa ZFA haina fedha hivyo amewaomba wadau na wahisani mbali mbali kuchangia hakuna fedha hivyo inaomba kuungwa mkono kwani ni ZFA mpya na haina mgawanyiko wowote.

Zanzibar leo

Share: