Michezo

Ujenzi Uwanja wa Mao kuanza wakati wowote

Na: Abubakar Khatib Kisandu.

Tangu Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar, Rashid Ali Juma awakabidhi Uwanja wa Mao Tse Tung wakandarasi wa Kichina kampuni ya Zhengtar Group Company Limited kwaajili ya kuujenga kisasa uwanja huo ambao utajengwa kwa mwaka mmoja na miezi miwili, zoezi hilo la ujenzi litaanza rasmi wiki hii kuanzia kesho Jumanne kwa mujibu wa wataalamu wanaosimamia zoezi hilo.

Mtandao ulimtafuta Mhandisi wa uwanja huo Ali Mbarouk Juma ambapo ameelezea sababu zilizochelewa kidogo kuanza rasmi ujenzi wa uwanja huo.

Mbarouk amesema sababu kubwa iliyopelekea kudorora kujengwa uwanja huo ni mvua ambapo walilazimika kusitisha ujenzi kwa kupisha mvua hizo.

Aidha amesema vikwazo vyengine vilikuwa ni Vibali vya ujenzi ambavyo kwasasa tayari wameshapata na muda wowote watabandika bango lao la ujenzi kwenye eneo la uwanja huo.

“Tulikuwa tunasubiria mvua zipite ndipo ujenzi uanze rasmi, kwasasa mvua tayari zimeshakata muda wowote kutoka sasa utaanza rasmi, watakaopita katika eneo la uwanja wa Mao wataona bango ambalo litaonyesha kuwa pana ujenzi wa uwanja, mana ilikuwa kikwazo chengine vibali vya ujenzi hatujapata lakini kwasasa mambo yapo fresh na ujenzi kuanzia wiki hii muda wowote unaanza”. Alisema Mbarouk.

Ujenzi huo utakuwa na Viwanja viwili vya mpira wa miguu na chengine cha michezo ya ndani kama vile Mpira wa Kikapu, Mpira wa Mikono, Mpira wa Pete na mengineyo.

Katika Viwanja hivyo vya Mpira wa Miguu uwanja mmoja utakuwepo upande wa Magharibi ambao utakuwa na Jukwaa moja litakalochukuwa Mashabiki 1500 waliokaa.

Uwanja mwengine wa mpira wa miguu utakuwepo upande wa Mashariki ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua Mashabiki waliokaa 900 katika jukwaa moja ambalo litakuwepo katika Uwanja huo.

Viwanja hivyo vitakuwa na taa ambazo zitaweza kuwezesha kuchezwa michezo hadi usiku.

Uwanja huo utagharimu Shilingi Bilioni 12.5 kwa fedha za Tanzania ambapo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itatoa Shilingi Bilioni 11.5 huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia zaidi ya Shilingi Bilioni 1 kati ya hizo Bilioni 12.5 ambazo watalipwa Wakandarasi wa uwanja huo ambao ni Kampuni ya Zhengtar Group Company Limited ambayo ina uzoefu mkubwa wa kujenga Viwanja wa Michezo.

Zanzinews

Share: