Michezo

Wachezaji wa Kikwajuni wamshambulia mwamuzi Sheha Waziri

Na Mwajuma Juma

WACHEZAJI wa timu ya Kikwajuni juzi walimshambulia mwamuzi wa Kimataifa Waziri Sheha Waziri kwa kipigo kwa madai ya kutoridhika na maamuzi ya mwamuzi huyo.

Tukio la wachezaji hao kumshambulia mwamuzi huyo lilifanyika mara baada ya mwamuzi huyo kupuliza kipenga cha kumalizika kwa mchezo huo uliochezwa kati yao na timu Zimamoto.

Mchezo huo ambao ulichezwa kwenye dimba la Mao Dze Tung mjini hapa ulimalizika kwa timu ya Kikwajuni kufungwa bao 1-0.

Mbali na sababu hiyo pia wachezaji hao walidai kuwa wamelazimika kuchukuwa hatua hiyo baada ya mwamuzi huyo kuwatolea lugha ya matusi wakiwa kiwanjani.

“Ni mwamuzi gani yule anafikia hatua ya kututukana kiwanjani halafu tuseme mpira utakuwa kwa hali hii hauwezi kukuwa”, alisikika Omar Mohammed Kuzu akisema wakati mchezo huo ukiwa unaendelea.

Hata hivyo baadhi ya wadau waliohudhuria mchezo huo walikizungumzia kitendo hicho kwa hisia tofauti huku wengine wakisema kuwa kitendo hicho hakiendani na maadili ya mchezo huo.

Akizungumza na waandishi wa habari kocha mkuu wa timu ya KMKM Ali Bushiri alisema kuwa kitendo hicho si kizuri na wachezaji walipaswa kutafuta njia mbadala na sio kuchukuwa sheria mikononi mwao.

Bushiri ambae aliwahi kuwa kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ alisema kuwa kitendo hicho kingaliweza kudhibitiwa na uongozi wao kama wangalikuwa makini na wachezaji wao.

Waziri ambae alikosa watu wa kumsaidia wakati wa kupata kipigo hicho aliweza kukimbia hadi katika chumba cha waamuzi ndipo alipopata unafuu.

Licha ya mwmauzi huyo kukimbia chumbani humo lakini wachezaji hao walionekana kuwa na hasira kali waliweza kumfata na kuweza kugonga mlango wa chumba hicho kwa hasira.

Hata hivyo baadhi ya mashabiki waliokuwepo uwnajani hapo walisema kuwa ipo haja kwa ZFA Taifa kushirikiana na Jeshi la Polisi au vikosi vya usalama ili waamuzi waweze kupata ulinzi wakiwa viwnajani hapo.

Share: