Michezo

Wazanzibari na shauku kubwa ya katiba mpya ya ZFA

Wazanzibari na shauku kubwa ya katiba mpya ya ZFA
July 27, 2018

NA AMEIR KHALID

SOKA la Zanzibar limeendelea kuingia katika mtihani mzito baada ya wiki iliyopita mrajisi wa vyama vya michezo Zanzibar Suleiman Pandu Kweleza, kuifungia Kamati Tendaji ya chama cha Soka Zanzibar ZFA kutofanya kazi, na kuteua kamati maalum itakayosimamia masuala yote ya mpira wa miguu Zanzibar.

Maamuzi hayo ya mrajisi wa vyama vya michezo kuvunja kamati hiyo, yanakuja ikiwa imepita miezi kadhaa, tangu kujiuzulu kwa viongozi wakuu wa ZFA, rais Ravia Idarous Faina, Makamu wake wawili Mzee Zamu Ali na Ali Mohamed pamoja na mkurugenzi wa ufundi Abdulghani Msoma.

Maamuzi hayo ya mrajisi yamepokewa kwa hisia tofauti na wapenzi wa soka hapa Zanzibar, ambapo wapo baadhi yao waliunga mkono na baadhi yao walibeza na kusema kuwa yamezidi kudumaza soka la Zanzibar.

Mimi sitaki kuwa hakimu ya hayo lakini ninachotaka kusema ni kuwa, kama maamuzi hayo yalifanywa kwa lengo la kukuza na kuinua soka ambalo tayari ilikuwa limekosea njia basi tunaomba kheri kwa hilo.

Akitangaza maamuzi hayo mbele ya waandishi wa habari Kweleza alisema kuwa ofisi yake ambayo ndio yenye mamlaka ya kusimamia vyama vyote vya michezo vilivyosajiliwa serikalini, kwa mujibu wa sheria namba 5 ya mwaka 2010.

Alisema kuwa kutokana na hali inayoendelea hivi sasa na ofisi yake kufanya mapitio, imebaina kuwepo na mapungufu mengi katika katiba hiyo na yalitakiwa yarekebishwe kutokana mamlaka ya ofisi ya mrajisi kutoa amri kwa chama chochote cha michezo kurekebisha katiba yao ndivyo ilivyofanyiwa ZFA.

Katika maelezo yake alisema kuwa ameamua kuchukua maamuzi hayo kutokana na sababu tatu za msingi ambazo ni kushindwa kufanya marekebisho ya katiba kama walivyotakiwa na ofisi yake tangu Machi 20 2018, na walipewa miezi miwili kufanya hivyo jambo ambalo walishindwa kutekeleza.

Sababu nyingi ni kushindwa kusimamia ipasavyo kanuni za mpira wa miguu Zanzibar ambazo kila mwaka ofisi yake huzipitia , lakini imeabaini kuwa kanuani hizo zimeshindwa kutekelezwa na ZFA hali inayoashiria uwepo wa malumbano na mizozo Zanzibar.

Sababu ya tatu inayolipelekea kuchukuwa maamuzi ya kuisimamisha kamati hiyo ni kushindwa kutekeleza amri ya Mahakama, ambayo iliitaka ZFA kufanya marekebisho ya katiba, baada ya kesi namba 64 ya mwaka 2014, ambayo ZFA ilitakiwa kuunda kamati ya kusimamia marekebisho ya Katiba jambo ambalo halikufanyika.

Kwa sababu hizo tatu alizozitaja mrajisi, ni wazi kuwa maamuzi ya mrajisi yanalenga kufungua ukurasa mpya wa soka la Zanzibar, kwani miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yanalikwaza soka la Zanzibar ni katiba mbovu.

Hivyo kutokana na mamauzi hayo mrajisi huyo alisema kuwa amatangaza majina ya watu saba, ambao watasimamia masuala yote ya ZFA kwa kipindi hiki ambapo pia kamati hiyo imepewa majukumu matatu mazito ya kuyafanyia kazi.

Kamati hiyo ya muda mbali na majukumu mengine lakini kubwa zaidi na ambalo ni muhimu kwa umuhimu wake,kusimamia upatikanaji wa katiba mpya ya ZFA ambayo itakuwa na malengo ya kuendesha mpira wa miguu Zanzibar.

Hili ni jambo ambalo pengine lilikuwa linaubiriwa sana na wapenzi wa soka Zanzibar ambao wamepita katika kipindi kigumu, kwani kila mmoja alikuwa alilalamika juu ya tabia ya viongozi wa soka ambao dhahiri walionekana walishindwa kusimamia majukumu yao.

Sitaki kukumbusha ya nyuma ambayo dhahiri yaliwafika kooni wadau wa soka, lakini mfano mmoja ni idadi ya timu nyingi za ligi kuu, ambapo hadi sasa ligi kuu bado haijamalizika huku msimu mpya wa ligi katika nchi nyingi dunia inaanza tena mwezi ujao.

Hivyo basi naiomba kamati hiyo kufahamu kuwa wanajukumu kubwa sana la kuwakata kiu wazanzibari ya kuwa na katiba mpya ya soka la Zanzibar, ambayo itaendena na matakwa ya Caf na FIFA kama nchi nyingine zilivyo ili kusahau madhila ya katiba ya nyuma.

Nawatakia kila la kheri na Mwenye Mungu awaongoze kufanya haki na kusimamia vyema sheria, ili kwa mara ya kwanza Zanzibar nayo ipate katiba inayokidhi matakwa yote ya mpira wa miguu.

0774423007

binkhalidson@gmail.com

Zanzibarleo

Share: