Mashairi

Mashairi:Natafakari kauli, ulotowa kwa halaiki

Natafakari kauli, ulotowa kwa halaiki,
Moyoni sifurahiki, upumbavu siutaki,
Sipendipendi muziki, vichupi na ushabiki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki.

Tena twasema hatutaki, mipango ya kishabiki,
Jazba zenye mikiki, za Donge na Mashariki,
Upambe na chukichuki, usitufanyie rafiki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki.

Muungano sishiriki, kwetu haustahiki,
Upambe hatupambiki, twawapasha halaiki,
Msije kujenga chuki, vipi kwetu haupendeki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki.

Bora ukamate chaki, au ucheze na biki,
Wewe nimwenyee chuki, Ulotupiga bunduki,
Iko siku utasadiki, siku haki ikabaki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki.

Tunataka tuwashitaki, mlouwa bila haki,
Mpaka itendeke haki, mlouwa halaiki,
Jihadi haizimiki, kwa vishindo vya bunduki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki..

Hatupendi unafiki, na kufanywa mamluki,
Ikiwa huambiliki, (Wizaraya) Elimu hakukaliki,
Usije ukahamaki, Ukaja kutushitaki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki.

Tambua hatubadiliki, kwa vinyimbo na miziki,
Twaitaka yetu haki, tupate kuimiliki,
Mikononi idiriki, si huku kutudhihaki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki..

(Wizara ya) Ardhi hakushikiki, ya elimu utaimiliki?
Wazenj twasaka haki, agendani hatubanduki,
Wazenj twaweka biki, tumekasirika hatucheki,
Iwache yako dhihaki, Muungano hatuutaki..

Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Kwanza Hashuo Baadaee!!!

Al Udii

Share: