Burudani

Michezo

KIVUMBI cha ligi Kuu ya Zanzibar kiliendelea tena juzi katika uwanja wa Mao Dze Tung na kushuhudiwa miamba miwili Zimamoto na Polisi ikitoka sare ya kufungana mabao 2-2.

Polisi ambayo ndio iliyotanguliwa kufungwa katika mchezo huo ilijinasua kutoka katika mtego huo katika dakika za 67 na 87 za mchezo huo.

Mabao yote hayo kwa upande wa Polisi yaliwekwa kimiyani na mchezaji wao Juma Mgunda.

Kwa upande wa Zimamoto ilifanikiwa kujipatia mabao yake katika dakika ya tisa na 72 kupitia kwa mchezaji wake Hakim Khamis.

Wakati huo huo timu ya soka ya Jiwe Gumu imetoka kidedea katika mchezo wa mashindano ya kumuenzi marehemu Maulid Hamad Maulid baada ya kuifunga Sungusungu ya Jang’ombe mabao 4-1 katika mchezo uliochezwa kiwanja cha Taifa ya Jangombe.

Jiwe gumu ilijipatia mabao yake hayo kupitia kwa wachezaji wake Lukman Mohammed Buda, Salum Juma Mchwa, Omar Seif Karike na Salum Haruna wakati bao la kufutia machozi la Sungusungu likifungwa na Yussuf Konkisko kwa mkwaju wa Penant.

 Michuano hiyo inaendelea tena leo kwa mchezo kati ya Mpendae na Magic.

_______________________________________________ Taarifa nyengine________________________________________________

 

MAAFANDE wa timu ya Mafunzo wanatarajiwa kuondoka leo nchini kuelekea Msumbiji kwa mchezo wa marejeano kati yao na timu ya Muculumano ya nchini huko.

Mchezo kati ya miamba miwili hiyo unatarajiwa kupigwa siku ya Jumamosi ya Machi 10 mwaka huu, ambapo Mafunzo ili iweze kusonga mbele inahitaji ushindi wa mabao 3-0.

Mafunzo ambayo katika mchezo wake wa kwanza ilifungwa nyumbani kwa jumla ya mabao 2-0 inaondoka ikiwa na msafara wa wachezaji 17 na viongozi nane.

Timu hiyo imeagwa jana na kukabidhiwa bendera na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamduni, Utalii na Michezo Ali Suleiman Mwinyikai huko katika Bwalo la timu hiyo liliopo Kilimani mjini hapa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwinyikai aliwataka wachezaji hao kutovunjika moyo na matokeo ya awali na badala yake wakacheze kwa nia ya kuleta ushindi ili kulipatia sifa taifa lao.

Alisema kuwa pamoja na kuwa walifungwa katika mechi ya kwanza lakini hali hiyo isiwavunje moyo na badala yake waongeze juhudi ili kushinda na kusonga mbele.

Nae Keptein wa timu hiyo Ramadhan Haji Mwambe alisema kuwa timu yao iko imara na inakwenda kushindana na kurejea na ushindi.

“Tupo imara tunawaahidi wazanzibari kuwa tutafanya vizuri na wajitayaruishe kuwapokea kwa ushindi tunakwenda kuwafunga kwao kama walivyotufunga sisi tukiwa nyumbani”, alisema.

 Timu hiyo inaondoka ikiwa chini ya mkuu wa msafara Hassan Haji Haji.

Share: