Kimataifa

Hatutaki ‘wawekezaji’ wanaouza karanga mitaani

  • Kuanzia Januari mwakani Serikali pia itachukua hatua dhidi ya kampuni yoyote itakayoajiri raia wa kigeni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na wazawa.

Tumetiwa moyo na hatua ya Serikali ya Zimbabwe kupiga marufuku kampuni za nje zinazofanya biashara zinazoweza kufanywa na wazawa.

Kuanzia Januari mwakani Serikali pia itachukua hatua dhidi ya kampuni yoyote itakayoajiri raia wa kigeni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na wazawa.

Amri hiyo imekuwapo tangu mwaka 2010, lakini haikuwahi kutekelezwa. Rais Robert Mugabe alirejeshwa madarakani kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu uliopita kwa kuahidi kuitekeleza.

Mpaka sasa mpango wa Serikali wa kuwainua wazawa kiuchumi umekuwa ukiilenga sekta ya kilimo pekee. Mashamba makubwa yaliyokuwa yakimilikiwa na wakulima wa kizungu yamemegwa na kugawiwa kwa wazalendo katika hatua iliyozua utata na kupingwa vikali na nchi za Magharibi. Serikali imesema raia wa nchi hiyo wameandaliwa vizuri ili kuchukua nafasi za kuendesha shughuli zilizokuwa zikiendeshwa na wageni.

Kutokana na suala hilo la kuwagawia wananchi ardhi, Serikali ya Zimbabwe bado imewekewa vikwazo vya kiuchumi na nchi hizo za Magharibi. Hatua ya hivi sasa ya kuwazuia raia wa kigeni kuendesha biashara zinazoweza kuendeshwa na wazawa lazima itasababisha Serikali hiyo izidi kutengwa.

Hata hivyo, biashara ambazo zimetengwa kwa ajili ya wazawa ni pamoja na za rejareja na jumla, maduka ya kunyoa, biashara ya saluni, biashara ya kutengeneza na kuuza vitafunwa, kilimo, usafirishaji, biashara za majengo, matangazo na nyingine nyingi. Migahawa inayomilikiwa na wageni ambayo haitengenezi vyakula vya asili haitaathirika.

Tukiiangalia juu juu hatua hiyo ya Serikali ya Zimbabwe, tunaweza kujenga dhana potofu kwamba ni ya kibaguzi.

Lakini tukiiangalia historia ya nchi hiyo tangu ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980, tutagundua kwamba wazawa wengi wa nchi hiyo mpaka leo hawajafaidi kikamilifu matunda ya uhuru huo kutokana na Serikali ya Rais Mugabe kurithishwa mifumo ovyo ya kikoloni iliyoasisiwa na Serikali ya walowezi waliojitangazia uhuru bandia kutoka Uingereza mwaka 1965.

Hivyo, mwaka 1980 Serikali ya Rais Mugabe ilikabidhiwa uhuru wa bendera, siyo wa kiuchumi. Biashara ya ndani na nje, ardhi yenye rutuba, madini, nishati, utalii, maliasili na kadhalika vilibaki mikononi mwa wazungu, huku wananchi maskini na maelfu ya askari waliopigana vita ya msituni ya kuikomboa nchi hiyo wakiishi maisha ya udhalilishaji ya ombaomba. Huo ndiyo muktadha ambao hatua iliyotangazwa na Serikali ya Zimbabwe hivi karibuni unapaswa kuangaliwa.

Hakuna ubishi kwamba hatua hiyo ni ya kijasiri na inapaswa kuigwa. Hapa Tanzania raia wengi wa kigeni wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, huku baadhi ya kampuni za kigeni zikikiuka masharti ya mikataba zilizoingia na Serikali.

Raia wengi wa kigeni, hasa Wachina wamesambaa kila mahali; kwenye viwanda, migodi, misitu, mbuga za wanyama, huku wengine wakiendesha mikokoteni, kuuza karanga, vitumbua na nguo za mitumba.

Wengine wengi wanajihusisha na vitendo vya ujangili na biashara ya dawa za kulevya. Raia hao wameiteka nchi yetu kinamna na tunaweza kusema tayari wamejitangazia jamhuri.

mwananchi

Share: