Kimataifa

Maandamano ya maelfu ya Waingereza ya kupinga utawala wa kifalme mbele ya jengo la BBC

Suala la kuendelea utawala wa kifalme na falsafa ya kuwepo kwake nchini Uingereza, limeibua maswali mengi katika miaka ya hivi karibuni. Kadhia hiyo imekuja hasa baada ya kushadidi mgogoro wa kifedha na kiuchumi nchini Uingereza, suala lililopelekea serikali ya London kuchukua hatua ya kubana matumizi ya kiuchumi.

Katika hatua za awali serikali ya Uingereza ilipunguzwa bajeti ya sekta ya elimu, afya na huduma za jamii na kusababisha kuongezeka zaidi kiwango cha ukosefu wa ajira kwa raia wa nchi hiyo. Suala hilo limekuwa likizungumziwa sana hasa kwa kuzingatia kwamba, familia ya kifalme ya Uingereza hususan malikia wa nchi hiyo imekuwa ikifuja kiwango kikubwa cha fedha za wananchi wa nchi hiyo na hivyo kuwatwisha mzigo mzito raia wa Uingereza.

Hii ni kusema kuwa, bajeti ya familia ya kifalme nchini Uingereza mwaka huu, imeongezeka kwa asilimia 16 ikilinganishwa na miaka iliyopita na kufikia Euro milioni 43. Aidha mienendo mibaya na hatua zinazochukuliwa na familia ya kifalme ya Uingereza imegeuka na kuzua makelele katika vyombo vya habari vya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo Shirika la Habari la Uingereza BBC limekuwa likiipigia upatu familia hiyo ya kifalme, hali iliyopelekea kukosolewa vikali na jamii ya nchi hiyo. Pamoja na kwamba, shirika hilo la habari, linatakiwa kufanya kazi bila ya kuegemea upande wowote, hata hivyo limekuwa likiipigia upatu familia hivyo na kujikuta likiondoka katika mstari wake wa kazi.

Katika kulalamikia hatua ya shirila hilo la BBC, juzi Jumamosi maelfu ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa nchi hiyo, walikusanyika mbele ya ofisi kuu ya shirika hilo mjini London na kutoa nara na kaulimbiu za kukosoa vikali hatua ya kuipendelea familia hiyo katika habari zake. Waandamanaji walibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali wa kupinga utawala huo wa kifalme na halikadhalika mashirikiano yaliyopo kati ya viongozi wa shirika hilo na ufalme huo. Mkusanyiko huo uliratibiwa na kundi linalopinga mfumo wa kifalme nchini humo, linalofahamika kwa jina la “Jamhuri.”

Wiki iliyopita pia kundi la Jamhuri, lilitoa taarifa ya kupinga hatua ya Shirika la Habari la BBC kuakisi habari za familia ya kifalme na kusisitiza kuwa, shirika hilo la habari limegeuka na kuwa sawa na mashine ya matangazo ya familia hiyo. Kwa muda wa miaka mingi sasa kundi la Jamhuri limekuwa likifanya juhudi kwa ajili ya kubadili mfumo wa kifalme unaotawala nchini Uingereza na kutaka kuwepo rais wa kuchaguliwa na wananchi. Inaonekana kwamba, wapo watu wengi katika jamii ya Uingereza ambao wana mitazamo iliyo sawa na kundi la Jamhuri katika kupinga mfumo wa kifalme wa nchi hiyo.

Aidha kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya uchunguzi wa maoni ya ACM unaonyesha kwamba, uungaji mkono wa mfumo wa utawala wa kifalme nchini humo, umepungua kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, idadi ya watu wanaoamini kwamba, hali ya Uingereza itakuwa mbaya iwapo familia hiyo ya kifalme haitakuwepo, imepungua kutoka asilimia 63 na kufikia asilimia 51. Utajiri wa kuchupa mipaka, uwezo wa kupindukia na gharama kubwa za ulinzi wanaopewa familia hiyo na mkono wa sheria, ndiyo mambo yaliyosababisha matatizo hayo. Aidha kashfa za maadili na ubadhirifu wa fedha katika familia ya kifalme ya Uingereza, ni mambo mengine yaliyozusha makelele mengi katika vyombo vya habari. Na Sudi Jafar Shaban

Chanzo : http://kiswahili.irib.ir/uchambuzi/item/31822-maandamano-ya-maelfu-ya-waingereza-ya-kupinga-utawala-wa-kifalme-mbele-ya-jengo-la-bbc

Share: