Kimataifa

Mmoja auawa katika ghasia za kundi la MRC na polisi ya Kenya

Mtu mmoja amefariki dunia na wanachama wengine saba wa kundi linalotaka kujitenga eneo la pwani mwa Kenya la Mombasa Republican Council (MRC) baada ya kupigana na polisi nje ya Mahakama ya Sheria mjini Mombasa.

Mapigano hayo yalitokea baada ya polisi kuwazuia wanachama wa kundi hilo lililopigwa marufuku kuingia katika mahakama hiyo iliyokuwa ikisikiliza kesi inayohusu wanachama wa MRC.

Vijana wa kundi hilo linalotaka kujitenga pwani ya Kenya waliokuwa wamevaa tisheti zenye maandishi “Pwani si Kenya”, walijaribu kuingia mahakamani kwa nguvu lakini wakazuiwa na polisi wa kuzuia ghasia.
Serikali ya Kenya imelipiga marufuku kundi hilo na imetangaza kwamba haitafanya mazungumzo na watu wanaotaka kujitenga.

Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga alisema jana kwamba serikali ya Nairobi haitafanya mazungumzo na kundi hilo hadi pale litakapotupilia mbali kaulimbiu yake ya “Pwani si Kenya” na kujitambua kuwa ni Wakenya.

Mahakama ya Mombasa sasa imemwagiza OCPD wa Mombasa Kipkemboi Rop kufika mbele yake kesho kuwasilisha uchunguzi wake kuhusu ni nini kilichosababisha kuuawa kwa mshukiwa mmoja wa kundi la Mombasa Republican Council jumatatu wakati wa rabsha kati yao na polisi.

Wakati huo huo mkuu wa polisi mkoani pwani amesisitiza kuwa polisi wataendeleza msako mkali dhidi ya kundi hilo.

Share: