Kimataifa

Utumwa mamboleo Qatar kabla ya kombe la dunia

Makumi ya wafanyakazi wa kigeni wamefariki dunia nchini Qatar na maelfu ya wengine wananyanyaswa na kunyonywa wakati huu ambapo nchi hiyo inajitayarisha kuandaa fainali za kombe la soka la dunia hapo mwaka 2022.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Guardian la Uingereza umebaini kuwa wafanyakazi 44 raia wa Nepal wamefariki dunia nchini Qatar katika kipindi cha kati ya tarehe 4 Juni na Agosti 8 mwaka huu pekee. Uchunguzi huo unasema kuwa nyaraka zilizopatikana kutoka kwenye ubalozi wa Nepal mjini Doha zinasema kuwa, wahanga wengi kati yao wamefariki duniani kutokana na matatizo ya moyo au ajali kwenye maeneo ya kazi ngumu.

Nyaraka hizo pia zimeonesha kuwa wafanyakazi wengi wa kigeni nchini Qatar wanalazimishwa kufanya kazi nzito katika ujenzi wa taasisi zitakazotumwia katika fainali za kombe la dunia na kwamba badhi ya wafanyakazi hao hawajalipwa mishara yao kwa miezi kadhaa. Ripoti zinasema kuwa makampuni ya Qatar hayawalipi wafanyakazi hao mishahara yao ili kuwazuia kutoroka na kwamba wanapokonywa pasi za kusafiria na vitambulisho kwa sababu hiyo hiyo.

Gazeti la Guardian limesema baadhi ya wafanyakazi wa Kinepali wamekimbilia katika ubalozi wa nchi yao mjini Doha kutokana na manyanyaso makali waliyopewa na waajiri wao na vilevile ukatili mkubwa katika maeneo ya kazi ambao wanasema ni utumwa mamboleo.

chanzo Iranswahili radio

Share: