Habari

Hamad Rashid kuacha siasa

Hamad Rashid Mohamed ni mwanasiasa mkongwe mwenye historia ndefu ya kisiasa Zanzibar na Tanzania. Amewahi kushika madaraka ya juu ya uongozi katika vyama vya CCM, CUF na ADC. Pia katika Serikali zote mbili ya Muungano na ya Zanzibar.

Aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani (Serikali ya Muungano). Amekuwa Mbunge na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa muda mrefu kutoka Jimbo la Wawi (CUF).

Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 na ule wa marudio wa Machi 20, 2016 aligombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ADC, chama ambacho tangu kuasisiwa kwake hakijawahi kupata hata Diwani. Kwa sasa ni Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

By Muhammed Khamis – Mwananchi
Ijumaa, Disemba 21, 2018

Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema ataamua kuachana na siasa mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ujao wa 2020.

Hamad ambaye ni mwanasiasa mkongwe na mwenye historia ndefu ya kisiasa Zanzibar na Tanzania aliyasema hayo mjini Unguja jana (Alhamisi, Disemba 20) wakati akizungumza na Gazeti la Mwananchi lililotaka kujua kama ana nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020 atagombea nafasi ya urais lakini itakua ndiyo mara yake ya mwisho katika harakati zake za kisiasa.

“Lazima ifike wakati kiongozi ujitathmini mwenyewe kabla ya kungoja kujadiliwa na wananchi ukizingatia siasa kila siku hukua na kubadilika.”

“Hivi sasa kuna kundi kubwa la vijana wenye weledi kuliko hata sisi wakongwe hivyo nafikiri ni muda na wao kupewa nafasi,” alisema Hamad. Hadi uchaguzi mkuu (mwaka 2020) bado takriban miaka miwili.

Hamad ambaye kwa sasa ni Waziri wa Afya Zanzibar, alisema baada ya kustaafu siasa kwa vile ana uzoefu mkubwa wa biashara na mambo ya siasa anafikiria kuwa mshauri wa ndani na nje katika masuala hayo.

Share: