Habari

Harufu ya UDIKTETA mpya Zanzibar

Jumapili, Novemba 22, 2015

UKIITAZAMA picha hii unaweza kupata hisia kuwa Dk Shein ni mtu muungwana wa kauli na vitendo, utaona ni mtu mwenye huruma, mnyenyekevu na mwenye heshima, mwenye kuheshimu maamuzi ya watu na haki zao.

Ukimwangalia machoni na usoni utamuona ni mtu mwema, mwenye sura jamili na utamuona hawezi kunyang’anya hata pesa mbili ya mtu seuze kunyang’anya uongozi wa nchi na haki za wapiga kura wa Zanzibar.

Binafsi, nafahamu kuwa Dk Shein, alikula kiapo (aliapa) kwa kushika Qur’an tukufu tarehe 3/11/2010 kuwa atailinda na kuitetea Katiba ya Zanzibar, leo amekuwa kinara wa kuivunja. Kadhalika kughalifu sheria za nchi.

Kuna sababu gani hasa kwa Rais wa Zanzibar aliyemaliza muda wake (Dk Shein), kuendelea kung’ang’ania madaraka kitu ambacho anafahamu fika kuwa katika uchaguzi wa tarehe 25/10/2015, ameshindwa.

Wazanzibari ndani na nje wamepaza sauti kuhusu UDIKTEKTA mpya wa Dk Shein kwa nguvu za viongozi wa Tanganyika na CCM dhidi ya dhuluma wanayofanyiwa ndani ya nchi yao.

Ndani ya Zanzibar, shughuli nyingi tangu kumalizika kwa uchaguzi zimesimama au haziendi kama kawaida yake. Maisha ya watu yamezidi kuwa magumu na kila uchao yanazidi kuwa magumu, hata kwa hao CCM wenyewe.

Baadhi ya watu wameanza kuhoji kwamba, ‘kuna umuhimu gani Tanzania na hasa Zanzibar kuwa na mfumo wa vyama vingi, huku watawala wa CCM, hawamini kuwa mfumo huo kazi yake kubwa ni kugeuza utawala wa nchi.

Hapa, namkumbusha Dk Shein kwamba, kesho AKHERA, katika masuala ya kuongoza watu yatakayomkabili na kuulizwa ni yake peke yake, hayatamuhusu Kikwete, hayatamuhusu Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Magufuli, Borafya na maCCM wengine.

Hilo anapaswa kujuwa leo ambapo wakati unamruhusu. Uadilifu wa kuongoza watu pekee ndiyo kinga na silaha ya kila kiongozi wa watu, hususan anapojinasibu kwa imani ya kuwa muislamu.

Nasikia wiki hii kajitoa kimasomaso kuwababaisha wananchi kwa kuanza kukagua miradi ya maendeleo, kama Rais wa Zanzibar. Dk Shein, dunia inamzomea, inamcheka kwa kuwa muhula wake wa uongozi kama rais umekwisha. anachokifanya anajikashifu kwa vishawishi vya ulinzi unaomzunguuka.

Namtanabahisha kuwa huko hakuna kuleta shahidi wala wakili. Huko hakuna kwamba, huyu alinambia, alinizuia alinishauri. Dk Shein, anapaswa kufahamu tangu sasa kuwa huko, hatapewa ulinzi wa kijeshi wa kumsimamia kwa nyuma wakati akijibu maswali ya Allah.

Pia, afahamu kuwa huko hakuna vifaru kutoka Tanganyika vya kuwatisha na kuwatia hofu na woga wazanzibari kwa kuimarisha utawala haramu wa CCM ndani ya ardhi ya Zanzibar. Wakiristo, wanamsemo wao kwamba: “Kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe”.

Kwa hivyo, Dk Shein anapaswa kujuwa leo kuwa atabeba msalaba wake, Jecha Salim Jecha, Salim Kassim Ali (Mkurugenzi wa ZEC), wote kila mmoja atabeba msalaba wake, hilo wajuwe tangu sasa wakiwa na pumzi za uhai.

Siku ya Alhamisi, Novemba 19, mwaka huu wazanzibari wanaoishi London na nje ya mji huo, wamefanya maandamano kutaka Serikali ya Uingereza, iingilie kati na kutoa shinikizo kwa Serikali ya Tanzania, ili kuhakikisha Mshindi wa Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, anatangazwa na kuapishwa.

Hatua ya maandamano hayo imekuja kutokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi, huku akitoa sababu tisa ikiwemo uchaguzi kutokuwa huru na haki, madaia ambayo ni uongo.

Awali, Jecha alisema kuwa wameamua kufuta uchaguzi huo baada ya kubaini kasoro tisa, ikiwemo kuchezewa kwa matokeo Kisiwani Pemba. Madai ambayo ni uongo na unafiki mkubwa, ni madai ya kupanga kutokana na madai hayo kutokuelezwa mapema na kwa wakati.

Ukipita nyumbani kwa Jecha Salim Jecha, pale Saateni, Unguja utakuta nyumba yake kila pembe imezunguukwa na vikosi vya ulinzi, eti wanamlinda.

Kwa hivyo, Jecha afahamu kuanzia leo kuwa ‘atabeba MSALABA wake mwenyewe’. Ajue kuwa huko hakuna Dk Shein, hakuna Balozi Seif Ali Iddi wala hakuna vikosi vya kumlinda, ‘dunia hadaa’.

Tangu kufutwa kwa matokeo hayo ya uchaguzi mataifa kadhaa ya nje yamekuwa yakiingilia hatua hiyo ikiwemo Serikali ya Marekani na kutaka tamko hilo liondolewe.

Serikali ya Marekani imesema imeshtushwa sana na tamko la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

Katika tamko lililotolewa Dar es Salaam na Ubalozi wa Marekani, lilisema hatua hii inasitisha mchakato wa uchaguzi uliofanyika vizuri na kwa amani, kama ilivyoelezwa na waangalizi wa uchaguzi kutoka Ubalozi wa Marekani, Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na kusitisha zoezi la majumuisho ya kura lililokuwa linakaribia kukamilika.

“Tunatoa wito wa kuondolewa kwa tamko hilo na kuzisihi pande zote kudhamiria kwa dhati kuukamilisha mchakato huu wa kidemokrasia kwa uwazi na kwa amani.”

“Watu wa Zanzibar wanastahili kupata haki yao waliyoitolea maamuzi,” ilieleza taarifa hiyo iliyotumwa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa vyombo vya habari.

Nikirudi kwa Rais wa Zanzibar aliyemaliza muda wake, Dk Shein namshauri kuwa muungwana kuwasikiliza wa Zanzibari katika kudai haki zao na pia, kukubalina na miito ya kimataifa kuhusu kumtangaza na kumuapisha mshindi wa uchaguzi wa Zanzibar, badala kuendelea kuwa king’ang’anizi wa haki za watu.

Mwishoni mwa wiki hii, tumeona wazanzibari wanaoishi nchini Marekani, walivyojitokeza kudai haki za wazanzibari wenzao wa ndani ya nchi katika kupatia haki yao ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura kama katiba inavyoelekeza.

Mimi naamini kwamba CUF, hawawezi kukubali kabisa kurudi tena katika uchaguzi wa marudio unaoandaliwa na CCM kurudiwa mwisho wa mwezi wa Desemba au mapema Januari mwakani.

Cuf, wanaweza kukubali kurudia uchaguzi na kushiriki labda, iwapo hatua zote za uchaguzi huo zitasimamiwa na taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa (UN) Jumuiya ya Madola (Commonwealth), lakini kwa Tume ya Jecha na Salim Kassim, watajirusha wenyewe..

Share: