Habari

HATA WAHAME WOTE UPINZANI HAUTOKUFA.

Na Abdalla Dadi.

Franklin D. Roosevelt aliwahi kuandika katika moja ya maandiko yake kua, “In politics, nothing happens by accident. If it happens, you can bet it was planned that way”. Akimaanisha kwamba, “Katika siasa hakuna kinachotokea kwa bahati mbaya. Kikitokea unaweza kusema kilipangwa kitokee hivyo”.

Patrick Murphy nae akaandika na kusema, “The political process does not end on Election Day. Young people need to stay involved in the process by continuing to pay attention to the conversation and holding their leaders accountable for the decisions they make”. Kwamba, “Mchakato wa kisiasa hauishii katika siku ya Uchaguzi. Vijana wanapaswa kuendelea kushiriki katika mchakato kwa kuendelea kuskiliza kwa makini mazungumzo na kuwawajibisha Viongozi wao kwa maamuzi wanayoyafanya”.

Nukuu hizi mbili na nyengine nyingi, nitazitumia kuelezea kile kinachoendelea sasa nchini Tanzania ambapo tumeshuhudia wimbi la wanasiasa wengi wa upinzani wakivihama vyama vyao na kuhamia CCM kwa hoja za kumuunga mkono raisi ama kukosekana kwa maelewano ndani ya vyama vyao.

■ Jambo la kwanza na la msingi sana tunalopaswa kulifahamu ni kwamba, matukio ya Wanasiasa kuhama Chama kimoja na kuhamia Chama chengine si matukio mageni duniani na hivyo Watanzania hawapaswi kushangazwa ama kusikitishwa na Wanasiasa wetu wa upinzani kuhamia CCM.

Matukio ya Wanasiasa kuachana na Vyama vyao na kuhamia katika Vyama vyengine ni matukio ya kihistoria ambapo yametokea katika mataifa mengi duniani.

Mfano; Katika hatua za awali za kuanzishwa kwa nchi za Ki-communists, kulishudiwa wawakilishi na wanachama wengi wa vyama vya Ki-communists wakihama vyama vyao na kuhamia katika vyama vya Ki-socialist na Ki-Conservatives. Wakati huo huo kulishuhudia pia hali ilivyokua nchini Uingereza ambapo Waliberali wengi walihama Vyama vyao na kuhamia katika Chama cha Labour Party mnamo karne ya 20. Matukio hayo yalikuja kufatia kuwepo kwa mitazamo tofauti ya kisera na kiitikadi kwa wanachama na wanasiasa hao.

Nchini Australia nako hakukubaki tu kama kulivyo. Kuhama kwa mwanasiasa mkongwe nchini humo mwaka 1997, Bibi Cheryl Kernot kutoka katika Chama cha Australian Democrats kwenda katika Chama cha Australian Labor Party kuliiibua sura mpya.

Kernot ni mwanamama ambaye alishika nyadhifa nyingi za Serikali nchini Australia ambapo moja ya nafasi zake alizowahi kuzitumikia akiwa na Chama cha Australian Democrats ni nafasi yake ya Useneti ambayo ameitumikia kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 1997. Kernot pia alijichukulia sifa ya kua kiongozi wa tano wa Chama cha Australian Democrats kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 1997.

Mnamo tarehe 15 October 1997, Kernot alijiuzulu nafasi yake ya Useneti na kuiacha nafasi yake ya Uongozi wa Chama cha Australian Democrats kwa naibu wake, Meg Lees na kujiunga na Chama cha Australian Labor Party.

Kernot tofauti na Wanasiasa wengi wanaojiuzulu leo nchini Tanzania, wakati wa kujiuzulu kwake, Kernot hakuwahi kukikosoa Chama chake cha mwanzo alichokitumikia kwa muda mrefu na badala yake Kernot aliibuka tena kupitia Chama chake kipya cha Australian Labor Party alichojiunga nacho na kuchaguliwa tena kwa kura nyingi katika Uchaguzi wa mwaka 1998. Kernot alishindwa katika Uchaguzi wa mwaka 2001 na hatimae akasimama kama mgombea huru (independent candidate) kuwakilisha New South Wales katika Senate kwenye Uchaguzi wa mwaka 2010.

Nchini Marekani nako mwanasiasa na Seneta James Merrill Jeffords aliechaguliwa kushika nafasi hiyo mwaka 1988 na kuchaguliwa tena mwaka 1994 na mwaka 2000 kupitia Chama cha Republican akafanya yake.

Jeffords aliezaliwa tarehe 11 May, 1934 na kufariki August 18, 2014 alikua ni mwanasiasa wa Kimarekani alietumikia nafasi ya Useneti kuanzia mwaka 1988 kupitia Chama cha Republican mpaka mwaka 2001 alipokihama Chama hicho na kuhamia katika Chama cha Democrats.

Pamoja na mambo makubwa aliyoyafanya Jeffords akiwa na Chama cha Republican, May 24, 2001 Jeffords alikihama Chama hicho na kutangaza kua huru. Jeffords alitangaza kukihama Chama hicho na kusema kwamba atajiunga na Chama cha Democrats kwa ajili ya malengo ya pamoja mara tu baada ya ripoti ya bili ya kodi itakapowasilishwa kwa raisi.

Jeffords licha ya kushika nyadhifa kadhaa ndani ya Serikali ya Marekani kupitia Chama cha Republican, alikua mpinzani mkubwa wa sera za Uongozi wa raisi George W. Bush ikiwemo Sera ya Bush tax cuts iliyopelekea kuhama kwake.

Kuhama kwa Jeffords ndani ya Chama hicho kulitokana pia na Senate ya Republicans kukataa Sheria ya kuwalipia masomo watu wenye ulemavu (full fund with Disabilities Education Act).

Katika maelezo yake Jeffords alisema, “Kwa hakika, naona nafsi yangu haikubaliani na Chama changu. Nafahamu kwamba watu wengi kutika Chama cha Republican ni wahafidhina zaidi yangu mimi. Kuubadilisha uhalisia wa Chama cha kitaifa imekua ni mapambano kwa Viongozi wetu kukabiliana na mimi na kwangu mimi kukabiliana na wao”.

Jeffords hatimae, baada ya kuona mambo hayaendi sawa akaamua kukihama Chama alichokitumikia kwa muda mrefu sana katika historia ya maisha yake.

Nchini Uturuki nako kukazidi kutokea vioja. Mwanasiasa Kubilay Uygun aliezaliwa mwaka 1955 huko Ankara alihama na kuhamia Vyama vyengine mara kadhaa katika historia ya maisha yake.

Ndani ya mwezi mmoja mnamo July 1996, Uygun alikihama Chama chake cha Democratic Left Party (DSP) na kuhamia katika Chama cha True Path Party (DYP), akarejea tena katika Chama cha Democratic Left Party na akajiunga tena katika Chama cha True Path Party. Na huu ndo ukawa msururu wa mara alizohama na kuhamia katika Vyama hivyo;

July 3, 1996, Uygun alijiuzulu katika Chama cha Democratic Left Party (DSP)baada ya Uchaguzi wa December 24, 1995 na kujiunga na Chama cha True Path Party (DYP).

July 6, 1996, Uygun alijiuzulu katika Chama cha True Path Party na kujiunga tena na Democratic Left Party mnamo tarehe 8 July, 1996.

July 30, 1996, Uygun akajiuzulu tena katika Chama cha Democratic Left Party na kujiunga tena na Chama cha True Path Party.

June 27, 1997, Uygun akajiuzulu tena katika Chama cha True Path Party na kujiunga na Chama cha MHP.

July 18, 1997, Uygun alijiuzulu katika Chama cha MHP na kujiunga na Chama cha DTP mnamo December 28, 1997 na hatimae June 10, 1998, Uygun akajiuzulu katika Chama cha DTP.

Matukio kama haya ya Wanasiasa kujiuzulu na kuhama Chama kimoja na kuhamia Chama chengine hayakuishia hapo. Nchini Canada nako kukawa na msururu wa Wanasiasa waliohama Chama kimoja kwenda Chama chengine kwa nyakati tofauti.

September 1, 1868, Stewart Campell, ambae alikua Mbunge wa Chama cha Anti-Confederation alikihama Chama hicho na akawa mwanachama wa Chama cha Liberal-Conservative.

Mwaka 1873, Newton LeGeyet Mackay alihama katika Chama cha Conservatives na kujiunga na Chama cha Kiliberali.

Mwaka 1917, William Andrew Charlton alihama katika Chama cha Kiliberali na kujiunga na Chama cha Liberal – Unionist.

Nako nchini Nigeria katika Uchaguzi wa 2015 wanasiasa waliowengi walitimkia vyama vyengine. Chama tawala cha Peoples Democratic Party (PDP) kikapoteza wanachama wake kadhaa. Naibu Gavana na Wanasheria kadhaa wakakihama Chama hicho kwasababu tofauti tofauti.

Tele Renner Ikuru, Naibu Gavana wa jiji la Rivers nchini humo akatangaza kuhamia APC kutoka PDP mnamo March 22, 2015.

Ali Olanusi, Naibu Gavana wa Ondo nchini humo akakihama Chama cha PDP mnamo March 26, 2015 na kujiunga na Chama cha APC. Olanusi alisema katika maelezo yake kua, ameamua kuhamia katika Chama cha APC baada ya kugundua kua, Chama hicho kinatoa fursa za haki na usawa.

Fred Ikhuebor ambae ndie aliekua Mlinzi Mkuu wa Kampeni za raisi Goodluck Jonathan katika mji wa Edo nchini humo aliwaongoza watu 3,000 kwenda kujiunga na Chama cha APC mnamo January 9, 2015. Ikhuebor alisema kua aliamua kurudi nyumbani na kujiunga na Chama cha APC ili kufanya siasa safi.

Chinwoke Mbadinuju, Gavana wa zamani wa Anambra alijivua Uanahama wa PDP na kujiunga na Upinzani mnamo February 24, 2015.

Mbadinuju alietumikia nafasi hiyo ya Ugavana kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2003 alisema kua, kutokuepo kwa haki ndani ya Chama cha PDP ndio sababu iliyomfanya aachane na Chama hicho na kujiunga na Chama cha Upinzani.

Orodha ya matukio kama haya pia ipo katika nchi mbali mbali Ulaya na barani Afrika.

Hivyo, orodha hii ya watu hawa wachache nimeiweka kama mfano tu wa kuthibitisha ukweli wa hoja yangu ya mwanzo kua, matukio ya Wanasiasa kuhama Chama kimoja na kuhamia Chama chengine si matukio mageni yaliyopata kutokea duniani. Hilo ni muhimu tulifahamu.

■ Jambo la pili na la msingi sana tunalopaswa kulifahamu ni kua, licha ya kuwepo kwa matukio hayo katika nchi mbali mbali duniani, kuna tofauti kubwa kati ya mifano niliyoitaja hapa na Wanasiasa wetu wanaojizulu nchini Tanzania kwa hoja ya kwenda kumuunga mkono raisi Magufuli.

Tofauti ya kwanza ni kwamba, niliowataja hapa ni Wanasiasa ambao walitumikia nchi zao katika nyakati tofauti tofauti ndani ya Serikali. Wao hawakua washamba wa madaraka na wageni wa kuitumikia Serikali na kwa hivyo, wao hawakua na uchu wa kuitwa ama kuonekana na nyadhifa kubwa Serikalini. Ndio maana waliacha nyadhifa zao na kujiunga na Vyama vyengine kutokana na sababu mbali mbali.

Nchini Tanzania ni tofauti. Wanaohamia CCM wanaonekana wazi kua, wanahamia huko ili kutafta vyeo, nafasi Serikalini na nyadhifa mbali mbali ambazo zitawapatia fedha na sifa za kuonekana wakubwa katika Serikali. Uchu na Ushamba wa madaraka na vyeo ndio tatizo linalowasukuma Wanasiasa wa Upinzani nchi Tanzania kujiunga na CCM.

Tofauti ya pili na ambayo ni ya msingi sana ni hoja walizotumia kuachana na Vyama vyao kina Kernot, Jeffords na wengine niliowataja katika makala hii. Wote niliowataja hawakuhama kwa kununuliwa. Wao walikua na uwezo wao wa kifedha na nafasi kubwa tu ndani ya Serikali na hivyo, kuhama kwao kulikuja kwa hoja za msingi sana tofauti na Wanasiasa wetu wanaohama kwa kununuliwa na kuja na hoja nyepesi ya kumuunga mkono raisi.

Tofauti ya tatu ni kwamba, orodha hii nilioitaja hapa inaonyesha wazi kua, wengi wao kama sio wote walihama katika Vyama tawala na kuhamia katika Vyama vya upinzani tofauti na tunavyoshuhudia leo nchini Tanzania ambapo wengi wa Wanasiasa wanaohama wanatoka upinzani kwenda kwenye Chama tawala.

Hili lina maana kubwa na moja ya maana yake ni kwamba, historia inaonyesha kua, Wanasiasa wengi wanapoona mambo yanakwenda kombo kama yanavyoenda kombo leo nchini Tanzania, Wanasiasa hao huhama katika Chama tawala na kwenda kupigania mambo hayo yaende sawa kupitia Vyama vya upinzani.

Ni Tanzania pekee ambapo tunashuhudia mambo hayaendi sawa halafu wapinzani wanajiunga na Chama tawala na sio Watawala kujiunga na Upinzani ili kuyafanya mambo yaende sawa. Hii ni kwasababu, wapinzani wa Tanzania labda wanaona ingekua tabu kwao kupata wanachokitaka kupitia Chama tawala katika nyakati ambazo mambo yanaenda sawa na hivyo wakaamua kuutumia mwanya wa mapungufu ya Chama tawala kwenda kujinyakulia wanayoyataka kama vile vyeo, fursa, fedha na nafasi Serikalini.

Wapinzani wa Tanzania wanajua wazi kua, mambo hayo wasingeweza kuyapata katika kipindi cha Kikwete ambapo CCM ilikua iko imara na inafanya vizuri angalau, lakini kwa sasa kwa vile mambo hayaendi sawa, hayo yote ni rahisi kupatikana. Hii ndio maana nasema pia kua, tofauti hizi zinamaanisha kwamba, siku zote wanaotafta vyeo, fedha, ulwa na sifa ndio huhama Upinzani na kuhamia katika Vyama tawala na wale wanaotafta maendeleo na kulinda hadhi zao kutokana na aibu ya kushindwa kufanya vizuri kwa Chama tawala huhama katika Vyama tawala na kujiunga na Upinzani.

■ Jambo la tatu na la mwisho na la msingi sana tunalopaswa kulifahamu ni kwamba, matukio haya ya Wanasiasa kuhama vyama vyao na kuhamia katika vyama vyengine hayajawahi kufanikiwa kuua upinzani au kuiua demokrasia Ulaya na barani Afrika. Hapa ni muhimu tukafahamiana sana.

Wakati Waliberali na Wahafidhina wanahama kutoka Chama kimoja kwenda Chama chengine ilikua ni miaka kadhaa iliyopita nyuma. Licha ya miaka hiyo kupita na mpaka sasa matukio hayo kuendelea kutokea, Vyama hivyo viwili bado vipo na sasa vimeimarika zaidi.

Hakuna sehemu barani Ulaya na Afrika ambapo Upinzani ulikufa na kupotea moja kwa moja eti kwasababu tu Wanasiasa wamehama Chama kimoja kwenda kujiunga na Chama chengine. Katika hili Watanzania ondoeni shaka.

Ni ukosefu wa kujua historia na mambo yanavyoenda duniani kudhani kua, upinzani utakufa kwasababu ya Wanasiasa kuhama Chama kimoja na kuhamia Chama chengine.

Kwa hivyo, nikirudi katika nukuu zangu mbili za mwanzo, ni muhimu Watanzania wajue kua, katika siasa zetu za Tanzania yanayoendelea sasa ni matukio yaliyopangwa na Watawala lakini sisi Vijana na Watanzania kwa ujumla hatupaswi kukata tamaa. Ni muhimu kwetu kuwaskiliza Wanasiasa wetu wanahubiri nini ili tuje tuwawajibishe katika Uchaguzi unaofata wa mwaka 2020.

Hiyo ndio nafasi pekee ya kuikumbusha CCM na waliohama katika Vyama vyetu na kujiunga na CCM yale maneno aliyoyasema Martin Sheen kua, “Future generation are not going to ask us what political party were you in. They are going to ask what did you do about it, when you knew the glaciers were melting”.

Maa Assalaam.

Share: