HabariMakala/Tahariri

Hawaiombei Zanzibar wanafanya uchuro

Jabir Idrissa,

WAMETUMIA fedha “tele” za wananchi ili kugharamia kile wenyewe walichokiita “dua” ya kuiombea Zanzibar. Wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanajidai kuamini Zanzibar inaumwa kwa hivyo ni muhimu kuiombea.

Kwamba wakiiombea kwa pamoja, uwanjani ambako watawajumuisha masheikh wakubwa wa Zanzibar na wageni akiwemo Sheikh Alhad Mussa Salim, ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wakiongozwa na maulamaa kutoka Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, itapatikana dua mjarab kwa tatizo linaloisibu Zanzibar.

Kituko kikuu. Wakubwa wa CCM hawajawahi hata mara moja kusikika hadharani wakisema Zanzibar ina tatizo lolote linalostahili kuwepo mkusanyiko wa namna hiyo walioutumia wiki iliyopita kama hoja ya kuiombea Zanzibar.

Tunapojiridhisha kwa ukweli huo, kwamba hawajathubutu kutamka bayana kuwepo tatizo, na wamekuwa wakiwaeleza wanachama wao kutokuwa na wasiwasi wowote, na uchaguzi ndio umeshafanyika na CCM ndio imeshinda kila kitu, na Dk. Ali Mohamed Shein ndiye rais wa Zanzibar ambaye ameshaunda serikali, na hakutakuwa na mtu wa kumtoa Ikulu, inafikiaje leo wajisumbue kuandaa dua ya kuiombea Zanzibar amani na salama?

Ni wao ambao kwa kujiona na kujiamini kuwa wanafanana na majemedari wasioshindika na kuweza kutetereshwa na mtu yeyote awaye, bila ya hofu, hawajisikii kuwa ni dhaifu mbele ya Mwenyeezi Mungu aliyewaumba na kuwatunuku akili ya kufikiri na kuamua, macho ya kuona na masikio ya kusikiliza.

Ndivyo ilivyo hawajisikii wao ni viumbe dhaifu wa mwisho kwa Allah, ndio maana baadhi yao wanaoitwa viongozi wa ngazi ya juu wanashuhudiwa majukwaani wakipiga vifua na kuzikufuru aya za Mwenyeezi Mungu. Ni nini basi kinachowasukuma kipindi hichi hata kuamua kuzitumia aya zilezile kuitakia Zanzibar amani na salama?

Kama vile wanaamini kiukweli kutoka ndani ya vifua vyao, kuwa Zanzibar ina tatizo kubwa linaloiumiza nchi hii, linalowanyong’onyeza watu wake na linalovunja moyo wananchi wema kutowaridhia kwa njia wanayoitumia wao kuongoza serikali, wamekusanya watu kwenye Uwanja wa Amaan, na kusoma walichoita dua kwa ajili ya Zanzibar.

Ili kufanikisha nisichoona aibu kukiita “uchuro” – unavyoendelea kusoma hapa utanithibitisha huko mbele kwamba katika kusoma hiyo dua, asilani hawakusudii kumwelekea mola aliyewaumba – wakatumia fedha za wananchi kukusanya watu.
Wakazitumia fedha za umma kununua mafuta ya gari za kubebea watu hao kutoka maeneo mbalimbali ya mjini Zanzibar na wakalipa posho madereva binafsi kwa ajili ya kurahisisha kuwafikisha watu uwanjani.

Haikuchukua hata nusu siku baada ya kusoma walichokiita dua, walijiachia na kuonesha walivyo wakorofi kwa kasi inayomkaribia Firauni.
Kwa kuwatumia mawakala wao wanaowalisha bure, na kuwafundisha uharamia ndani ya kambi za serikali huku wakiwapatia tumbaku za kuvuta na pombe ya kujitoa haya usoni, wakiwabebesha silaha mbalimbali, za jadi kama mapanga, marungu na mapande ya nondo, minyororo pamoja na bunduki zilizojazwa risasi, walivamia barza ya wananchi wema na wakawapiga na kuwapora mali zao zikiwemo simu na fedha taslim.
Kama ulisikia tukio la kuvamiwa wananchi wema katika barza yao iitwayo Super Power, iliyoko Taveta, jimbo la Pangawe, basi ni uharamia uliofanywa jioni tu ya siku hiyo waliyoiombea Zanzibar amani na salama.

Katika tukio hilo la uvamizi lililofanywa usiku wa saa 3 hivi Disemba 6, maharamia waliotumia gari za serikali, wakiwa wamefunika nyuso zao kwa kutumia soksi au vitambaa vyeusi, kama mbinu ya kuficha kutambuliwa, waliwashambulia wananchi akiwemo mzee wa miaka 72 aitwae Maulid Abdalla Chawa.

Wananchi wengine walioshambuliwa na kujeruhiwa ni Suleiman Vuai (Lobilo) mwenye umri wa miaka 56, Aziz Muhamed Ali (42) na Mbaraka Pandu Makame (40). Wote hawa na ukweli hasa barza yao inakaliwa zaidi na Wazanzibari wa asili ya Wilaya ya Kusini ambako Chama cha Wananchi (CUF) kimejizolea waungaji mkono wengi hata kuwashtua CCM.

Inakuaje viongozi wenye akili timamu na wanaojitia kuwa wanaipenda Zanzibar na Wazanzibari, wakaridhie kushambuliwa wananchi kwa silaha na kuwadhulumu damu na mali zao?

Kuonesha kuwa viongozi wa CCM wakipewa nguvu kubwa na wakuu wa serikalini, hawapendi wananchi na kwa kweli hawana huruma na nchi, wala hawana uchamungu wanaojivunia hata kukusanyika kwa wanachokiita dua ya kuiombea Zanzibar, waulize ni kwanini hawajaamuru Jeshi la Polisi liwakamate maharamia walioshiriki uvamizi wa wananchi hao.

Jeshi la Polisi hata usikie wakuu wao wakisema kwa sauti kuwa watachunguza na kuwakamata wahusika na kuwashikisha mkono wa sheria, hawapo katika ukweli na uadilifu. Hawajawahi kumkamata hata mtu na kumhusisha na matukio ya namna hii, si mwaka jana kabla ya uchaguzi wala baada ya mapinduzi ya maamuzi ya wananchi, na hata baada ya uchafuzi wa “uchaguzi wa marudio.”

Makumi kwa makumi ya matukio ya kiharamia yamekuwa yakifanywa na maharamia hawa wanaotambuliwa kwa umaarufu siku hizi kwa jina la Mazombi, badala ya lile la Janjaweed kama wa Sudan Kusini, lakini hakuna aliyechukuliwa hatua za kisheria.

Taasisi ya Polisi sio tu kwamba haijishughulishi kudhibiti ushenzi unaofanywa dhidi ya wananchi wema wakiwemo watu wazima wa umri wa mzee Chawa, 72, bali kwa kweli wanakutwa askari wao wakifuatana bega kwa bega na mazombi na kusimamia utekelezaji wa mipango yao.
Wakati nikiweko Zanzibar baada ya CCM kujitangaza washindi wa uchaguzi wa marudio, Machi mwaka huu, nilishuhudia baadhi ya misafara ya maharamia hawa mitaa ya Kwarara. Wakiingia kwenye vioski vya chipsi na kupora fedha na pale walipokosa fedha, waliamuru hata wafungiwe chipsi wakisema, “mjue tuna njaa msituone hivi tunatumwa.”

Wakati mmoja walipotukuta nje ya penu za wenzetu njia ya Kwarara, tukizungumza maisha na yanayotusibu wananchi wa Zanzibar baada ya kudhulumiwa haki ya uchaguzi huru, wa haki na uliowapa ushindi CUF, maharamia walituamuru tukalale ikimaanisha wangependa wabaki peke yao mitaani na kujitanua watakavyo.

Zanzibar imekuwa ikiendeshwa kama vile ipo chini ya kafyuu, lakini hakuna kiongozi anayekemea uhuni huo. Viongozi wanaoshika serikali ambao ndio wanaonufaika na dhulma dhidi ya haki ya wananchi kutokana na maamuzi waliyoyafanya 25 Oktoba 2015, wanaridhika kuwa kila wanalolifanya maharamia ambalo linaumiza wale waliodhulumiwa haki, ni halali kwao.

Katika hali kama hiyo ya muendelezo wa dhulma kuzidi kuumiza nchi na watu wake, kukuta viongozi wa Kiislam wakishirikiana na wanasiasa chini ya wakuu wa mikoa na wale wa wilaya na kuomba amani na salama kwa nchi, ni unafiki mtupu. Dua ya mazingira hayo ni uchuro.

mwanahalisi

Share: