Habari

HAZINA ZETU ZAONDOKA

Tumepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Maalim wetu Ali Abdulla Juma, kilichotokea leo na maziko yatakuwa leo Unguja.

Marehemu Maalim Ali Abdulla Juma katika uhai wake aliwahi kusomesha katika skuli mbali mbali za Pemba na Unguja na kushika  nafasi nyingi Serikalini.

Marehemu ambaye alikuwa akiishi Hurumzi, Unguja karibu na Idara ya Elimu na karibu na skuli ya Forodhani na jirani kabisa na mchonga masanduku ya njumu alizaliwa 1932 Mtambwe Pemba.

Skuli alizowahi kusomesha ni Ng’ambwa na Ziwani, Chake Chake.  Utaani, Wete boys, Gando, Kizimbani zote za Wete, Pemba.  Pia alisomesha akiwa mwalimu mkuu skuli ya Ngambu (Raha-leo) Unguja.

Amekuwa mkaguzi wa elimu katika skuli za Unguja  kwa muda mrefu kabla ya kuwa Mkuu wa mitaala na baadae Mkurugenzi wa Idara ya elimu ya watu wazima Zanzibar. Na Mkuu wa Utumishi Wizara ya HUTV.

Kwa upande wa nafasi nyengine za Serikali aliwahi kuwa Ofisa mdhamini Wizara ya elimu Pemba, Mkurugenzi Idara ya Uchapaji, Meneja uwanja wa Amani na Viwanja vya kufurahisha watoto. Mkurugenzi Idara ya Mila na Sanaa na Mkurugenzi mtendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni , Utalii na Michezo.

Katika umri wa ujana wake  Maalim Ali Abdulla Juma, alikuwa mpenda michezo na hasa football na kuweza kuanzisha club ya mpira ya Cosmopolitans (sasa Mwenge)  ya Wete na kuwa captain wa timu.

Kwa upande wa mambo ya siasa za Zanzibar, hasa katika wakati wa malumbano na uhasama baada ya kurudi kwa mfumo wa vyama vingi 1992 Maalim Ali, alionekana kuibenza CUF na kujiweka zaidi CCM. Watu wengi waliyomjua walimchukulia ni mtu moga, asiyependa matatizo.

Marehemu ameacha kizuka mmoja na watoto wanane (8) akiwamo mtoto wake mkubwa Maalim Abdulla Ali Abdulla, Mwenyekiti mstaafu wa  ZAWA ‘UK Zanzibar Welfare Association’,  Wengine ni pamoja na Salama Ali Abdulla, mfanyakazi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Inna lillaah wa Inna Ilayhi Raajiun..

 

Share: