Habari

Hii haijawahi kutokea Ramadhan, Sheha amfuma mke wake akiku……….

June 8, 2018

Imeandikwa na Haji Nassor, PEMBA

JESHI la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, limesema baada ya kumaliza kumuhoji, kaimu sheha wa shehia ya Chimba wilaya ya Micheweni, Hamad Aayoub Khamis, kwa tuhuma za kumpiga mke wake kwa wizvu wa mpenzi, litampandisha kizimbani, pindi upelelezi ukikamilika.

Kamanda wa Polisi mkoa huo, Hassan Nassir Ali, amesema ni kweli Kaimu sheha huyo, juzi alihojiwa kutokana na kitendo cha kumpiga mke wake Juni 3, baada ya kudaiwa kumkuta akiwa na mwanamme.

Akizungumza na vyombo vya habari, alisema baada ya kumuhoji sasa kilichopo kwa Jeshi hilo, ni kuendelea na upelelezi wa kina wa tukio hilo, na pindi ukihusisha na tukio, atapandishwa mahakamani.

Kamanda Nassir, alisema baada ya kupokea malalamiko ya mwanamke mmoja miaka 38 kupigwa na mume wake, ndipo Jeshi hilo lilimpomtafuta na kumpata, na kisha kumuhoji, kwa kupata maelezio zaidi.

‘Ni kweli yupo kaimu sheha wa shehia ya Chimba, alimpiga mke wake na sisi Jeshi la Polisi tumeshamuhoji, na kilichobakia ni upelelezi, kwa lengo la kumfikisha mahakamani hapo baadae,”alieleza.

Hata hivyo, Kamanda Nassir ameendelea kutoa wito kwa wale wanaokosa, kuacha kujichukulia sheria mikononi, na badala yake wavitumie vyombo vya sheria kulalamika.

Akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu, Kaimu sheha huyo wa shehia ya Chimba, alikiri kumfumania mke wake nje ya nyumba yake, ingawa hakuthubutu kumpiga kama inavyodaiwa.

Alisema, baada ya kumfuma akiwa katika mazingira hatarishi, alichokifanya ni kumpapatuana, na yule mwanamme wa nje, ambapo hapo mke wake, alianguka chini na kisha kukimbilia hospitali na Polisi, akidai kuwa amepigwa.

“Aliniaga anakwenda kwa shoga yake, muda mfupi tu baada ya kumaliza kufutari hapo juzi, sasa mimi nikamfuatilia na kiasi ya masafa ya viwanja vitatu vya mpira (mita 300), nikamkuta kwenye nyumba na mwanamme wamekumbatiana hapo nikampapatua,”alisimulia.

Kaimu sheha huyo alieleza kuwa, yeye hajampiga na wala hajamucha mwanamke huyo, ingawa kwa sasa ameshachukuliwa na familia yake na hayupo nyumbani kwake.

“Mimi sijampiga, nilichofanya nilimpapatua mke wangu na yule jamaa, lakini pamepikwa mambo kuwa, nimempiga na wajomba zake, wamemchukua ingawa sijamuacha,’’alifafanua.

Kuhusu kuhojiwa Polisi, Kaimu sheha huyo alithibitisha kuhojiwa na kulala kituo cha Polisi kwa siku moja, ambapo alisema ataitwa tena kama akitahitajika juu ya tuhuma hizo.

Mwanamke huyo, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alikana kufumaniwa na mume wake, ingawa alikiri kupokea kichapo na sababu kubwa, akisema ni chuki ya mume wake.

“Unajua huyu mume wangu, anachuki zake muda mrefu sasa kanipiga kaniumiza, eti kisha anadai kunifumania , uongo mtupu, mwezi huu mimi muislamu nifanye hivyo,”alihoji mwanamke huyo.

Alieleza kuwa, kama kweli amefanya jambo hilo ovu na kubwa, wala wajomba zake wasingekuwa pamoja nae, na kumkimbiza kwa mume wake, lakini kwa vile amenipiga kwa chuki na hamaki zake, ndio maana amehifadhiwa kwao.

Mkuu wa wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib, ambae anadawi kumsaidia kumtoa sheha huyo kituo cha Polisi, alikana na kusema hata siku ya tukio hakuwepo mazingira ya kazi.

“Mimi sina taarifa mwandishi, maana hata siku ya tukio nilikuwa nje ya eneo la kazi, sasa sina taarifa na wala silijui kwa kweli,”alijibu Mkuu huyo wa Wilaya.

Kaimu sheha huyo, ameshazaa watoto watano na mke wake huyo, ambapo kwa sasa mwanamke huyo yuko kwa ndugu na jamaa zake na kuwaacha watoto wake wote.

Hili ni tukio la kwanza la aina yake kutokea katika kipindi cha miongo mitatu sasa, cha mume kumkuta mke wake akiwa katika mazingira ya kuvuuka maadili.

Pembatoday

Share: