Habari

“Hivi kuna mjinga gani ambaye hajui Meghji ni Mzanzibari? Sitta

Dar/Zanzibar. Utata wa kupiga kura unaomhusu Mjumbe wa lilikokuwa Bunge Maalumu, Zakia Meghji umechukua sura mpya baada ya kubainika kwamba alipiga kura upande wa Tanzania Bara tofauti na ilivyokuwa wakati wa kupiga kura ya uamuzi wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambako alipiga kura upande wa Zanzibar.

Tovuti ya Bunge Maalumu (www.bungemaalumu.go.tz) katika sehemu yenye orodha ya Kamati za Bunge hilo, Meghji ametajwa kuwa mjumbe anayetokea Bara ikimaanisha kwamba ndani ya kamati yake alikuwa akipiga kura kutoka upande huo wa Muungano.

Jina la Meghji ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa ni namba 37 katika orodha ya wajumbe wa iliyokuwa Kamati Namba Tano likisomeka kuwa ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano akitokea Tanzania Bara.

Baadhi ya waliokuwa wajumbe katika kamati hiyo wamelithibitishia gazeti hili kwamba mjumbe huyo alikuwa akipiga kura kama mtu wa Bara ndani ya kamati lakini walishangazwa na ‘uhamisho’ wa ghafla ambao alipewa wakati wa kupiga kura za jumla.

“Kwa kweli siwezi kufahamu walitumia kigezo gani kumweka Zanzibar maana tulipokuwa kwenye kamati alikuwa akipiga kura kama mtu wa Bara, kama huniamini watafute wajumbe wengine uwaulize,” alisema mmoja wa wajumbe huku akitafadhalisha jina lake kutoandikwa gazetini.

Licha ya uthibitisho huo, uliokuwa uongozi wa Bunge Maalumu umeendelea kung’aka kila unapoulizwa kuhusu suala hilo ambalo lilizua malalamiko kwamba lilifanywa ili kulazimisha upatikanaji wa theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema hakuna mtu asiyejua kwamba Meghji ni Mzanzibari hivyo kusema alipiga kura Bara ni hoja isiyokuwa na msingi.

“Hivi kuna mjinga gani ambaye hajui Meghji ni Mzanzibari? Alihoji Sitta na kuongeza kama aliolewa Bara hiyo siyo hoja ya kumfanya apige kura Bara.”

Sitta alisema ni muhimu watu wakaangalia hoja ya kuzungumza kwa kuwa Meghji alipiga kura Zanzibar na hata kwenye kamati ilikuwa hivyohivyo.

“Hata wewe mwandishi unajua Meghji ni mtu wa wapi au kwa mfano Hamad Rashid kwamba anaishi Bara lakini ni Mzanzibari sasa mlitegemea apige kura ya wapi? Bara au Zanzibar?” alihoji Sitta.

Katibu wa Bunge Maalumu

Aliyekuwa Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad naye aling’aka kama bosi wake akisema hawezi kujibu upuuzi kuhusu malalamiko yanayotolewa kuhusu uhalali wa Meghji kupiga kura kutoka kundi la Zanzibar wakati anaishi Tanzania Bara.
“Huo ni upuuzi, siwezi kujibu swali hilo la kipuuzi, mwendawazimu anaweza kujibu lakini kama lawyer (mwanasheria), siwezi kujibu swali hilo,” alisema Hamad.

Alisema anaamini taratibu zote za upigaji kura kutafuta theluthi mbili za Bara na Zanzibar zilizingatia kanuni na sheria na haoni sababu ya kujibu mambo yanayoendelea kujitokeza tangu Bunge hilo limalize kazi yake na kukabidhi rasimu ya mwisho inayopendekezwa.

“Kama kuna watu wanaogopa, siyo mimi,” alisisitiza Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi.

Alipoulizwa kuhusu jina la Meghji kuwapo kwenye tovuti ikionyesha kwamba anatokea Bara, Hamad alisema: “Siwezi kujibu hilo kwa sasa bila kuwa na nyaraka ambazo ndiyo msingi wa uamuzi, maana pia huwezi kufahamu kama kuna mtu ‘ame-temper’ na nini”.

Utata wa kura ya Meghji uliibuliwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba ambaye alisema mjumbe huyo alitakiwa kupiga kura upande wa Bara lakini katika upigaji kura, alipiga kura upande wa Zanzibar.

Wiki iliyopita aliyekuwa Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk Thomas Kashililah alisema upigaji wa kura ulizingatia asili ya mtu na siyo mahali anakoishi na kwamba hata uteuzi wa wajumbe haukuzingatia asili yao, bali makundi wanakotoka.

“Katika Bunge hilo kulikuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wajumbe 201 na wajumbe kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… lakini ieleweke kwamba mjumbe wa Baraza la Wawakilishi anaweza kuingia Bunge la Jamhuri lakini wa Jamhuri hawezi kuingia Baraza la Wawakilishi,” alisema Dk Kashililah.

Imeandikwa na Boniface Meena, Dar na Mwinyi Sadallah, Zanzibar.

Share: