Habari

Hoja ya kuidhibiti TLS yaibua mjadala

By Ibrahim Yamola na Tausi Ally – Mwananchi
Tuesday, April 24, 2018

Hatua ya Rais John Magufuli kutaka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kudhibitiwa, imeibua mjadala huku rais wa chama hicho, Fatma Karume akihoji kitu walichofanya hadi kufikia hatua hiyo.

Aprili 20, Rais Magufuli akizungumza baada ya kuwaapisha majaji 10, alimtaka Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma na mwanasheria mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi kuidhibiti TLS.

Bila kutaja jina, Rais Magufuli alirejea kauli ya Aprili 18 aliyoitoa Fatma Karume kuhusu bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka 2018/19, akidai mishahara ya watumishi wa mahakama wakiwamo majaji imepungua.

Hata hivyo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amesema Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kinafanya kazi za umma na kwamba hakipaswi kujiingiza katika siasa wala uanaharakati.

Jaji Juma ameyasema hayo jana Jumanne, Aprili 24 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari: “Majukumu ya TLS si siasa wala uanaharakati.”

Jaji Mkuu, amesema majukumu ya TLS ni kuishauri Serikali, Mahakama, Bunge na kuboresha elimu ya sheria na kusisitiza kwamba TLS ni taasisi ya umma na chama huru cha kitaaluma.

Jaji Juma amesema ukiangalia kazi za TLS, huwezi kuona siasa wala uanaharakati na kwamba TLS wasikubali kuingia katika siasa wala uanaharakati, wakiingia huko wengine hawatatoa ushirikiano.

Ameongeza na kusema iwapo TLS, wanataka kushirikiana na mahakama wabaki katika kazi zao, wakitaka kuwa huru wataachwa wawe huru lakini hawatapata ushirikiano kutoka kwetu sababu wengine haturuhusiwi kuingia katika siasa:

“Hapa Tanzania huwezi kutenganisha taaluma ya sheria na Uhuru wa Tanganyika,” amesema Jaji Mkuu.

Amesema TLS ilianzishwa 1954 tukiwa chini ya ukoloni wa Uingereza, wakati huo wanasheria wengine walikuwa ni Wazungu na Wahindi.

1960 na 1961 sheria zilizotungwa wakati wa ukoloni zilijadiliwa ni namna gani zifanye kazi, walifanya mabadiliko ambayo yaliwezesha TLS wabaki na ada zao ambapo zamani zilikuwa ni mali ya serikali.

Mwananchi ilipomtafuta Fatma Karume jana Aprili 24, kujua namna walivyoipokea kauli ya Rais Magufuli, alisema: “TLS imefanya nini hadi idhibitiwe na inadhibitiwa kwa malengo ya nani au faida gani?” alihoji na kuongeza:

“Hii kitu imenishtua sana, najiuliza kwa nini tudhibitiwe na ninachoweza kusema TLS itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na katiba iliyopo.”

Fatma alisema watakaoathirika baada ya TLS kudhibitiwa ni wananchi hasa ikizingatia kuwa wanasheria wanawatetea wao na wakati mwingine Serikali.

Alisema hakuelewa Jaji Mkuu aliposema TLS ni mali ya umma alichokuwa anamaanisha. “TLS si kama TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania) inayopata ruzuku, TLS inajiendesha kwa kutumia fedha za wanachama wake,” alisema Fatma.

Wanasheria hawabanwi

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga alisema duniani vyama vya wanasheria ni sehemu muhimu ya uendeshaji wa sheria katika nchi.

“Ili haki iweze kutendeka lazima kuwe na upande wa mashtaka, utetezi na mahakama na ili uhuru wa mhimili wa mahakama uweze kuonekana ni vyama vya kitaalamu kama hiki cha kwetu (TLS) kisibanwe au kudhibitiwa,” alisema Nyanduga.

Nyanduga alisema moja ya malengo ya TLS ni kuishauri serikali katika masuala ya kisheria. “Vyama hivi havipaswi kudhibitiwa kwa aina yoyote, ndiyo maana TLS ni mwanachama wa vyama mbalimbali vya kitaaluma,” alisema Nyanduga.

Alisema TLS haidhibitiwi ila kupitia kamati ya mawakili au Jaji Mkuu anaweza kutumia vyombo vyake kusimamia suala la ukiukaji wa maadili siyo kuwabana. “Kufanya hivyo ni kinyume cha kanuni za kimataifa,” alisema.

Nyanduga aliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba aliyesema TLS haikuanzishwa na mtu mmoja, bali ni watu na kama wanaona ina tatizo sheria ipelekwe bungeni kuifanyiwa mabadiliko..

Dk Bisimba alisema katika nchi zingine duniani, Mahakama inazuia mtu yeyote kuwabana wanasheria ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri.

“Kuwadhibiti wanasheria ni kuwanyima haki wananchi. Wanasheria wanapaswa kuwa huru na wasidhibitiwe, waachwe watekeleze wajibu wao na kama wanakiuka sheria wachukuliwe hatua si kudhibitiwa,” alisema Dk Bisimba..

Share: