Habari

Huu ndio umuhimu wa vyama vingi kwa taifa

Mikhail Gorbachev (pictured) GCL is a Russian and former Soviet politician. He was the eighth and last leader of the Soviet Union, having been General Secretary of the Communist Party of the Soviet Union from 1985 until 1991. Wikipedia

Na Bryceson Kayungilo – Raia Mwema

INAFAHAMIKA kwamba mfumo wa vyama vingi vya siasa uliingia katika nchi nyingi duniani mara baada ya kuanguka kwa dola la nchi zilizokuwa za muungano chini ya Umoja wa Kisoviet (Usoshalisti) zikiongozwa na Urusi baada ya kuanza kuwepo vuguvugu la mageuzi ndani ya iliyokuwa USSR.

Kiongozi wa Urusi enzi hizo, Mikhael Gorbachev ndiye chanzo kikuu cha kusababisha kuanza kwa mageuzi ya kuingia mfumo wa vyama vingi katika nchi nyingi duniani.

Historia inaonesha kuwa Gorbachev amekuwa chanzo cha mageuzi duniani baada ya kukubaliana na kushauriana mara kwa mara na waliokuwa viongozi wa mataifa makubwa ya Marekani na Uingereza wakimtaka kubadili mfumo wa uendeshaji wa taifa lake hasa upande wa siasa, utawala na uchumi.

Matokeo ya mashauriano hayo kati ya Gorbachev na Ronald Reagan aliyekuwa Rais wa Marekani na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Margreth Thatcher ilifanya Urusi kuingia katika mageuzi ya kisiasa na kiuchumi bila kutarajia.

Hapa ndipo kasi ya kuenea kwa vuguvugu hilo katika nchi za Ulaya ya Mashariki ilipoanza kutikisa kwenye mwaka 1988 na kuendelea kwa kaulimbiu yake ya Mageuzi na Uwazi (Grassnost na Perestroika) ya Gorbachev, nchini Urusi.

Hata hivyo, mageuzi hayo ya kisiasa na kiuchumi hayakuweza kufanikiwa kutokana na hali halisi ya sera ya Kikomonisti kwa wakati huo kwa sababu dola ndiyo ilikuwa inaendesha siasa na uchumi wa taifa ambapo ilikuwa kinyume na mwenendo wa sera za mataifa mengine makubwa yenye mfumo wa kibepari wa soko huria.

Inaelezwa kuwa mageuzi hayo yalikuwa chanzo cha kusabaratika kwa dola la Kisovieti iliyokuwa na jumla ya nchi 15, hali iliyosababisha nchi hizo kujitenga na dola hiyo, hivyo kufuata mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi na soko huria.

Hapo ndipo dunia ikaanza kuona umuhimu wa nchi nyingine kufuata mfumo huo wa vyama vingi vya sasa ambao unajenga na kuimarisha demokrasia, utawala bora na uchumi duniani.

Mtiririko wa kuenea kwa mfumo wa vyama vingi uliyakumba maeneo mbalimbali duniani, mfano ni nchi zilizokuwa za Kikomonisti barani Asia, Ulaya Mashariki, Afrika na Mashariki ya kati.

Lakini kabla ya hapo nchi nyingi zilikuwa katika mfumo wa chama kimoja cha siasa zikiongozwa na utawala wa mabavu sambamba na nchi zilizokuwa zina tawaliwa kifalme na kijeshi.

Wakati linaanza vuguvugu la kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa dunia kote viongozi wengi waliokuwa madarakani wakati huo hawakupenda kwa kuhofia mambo mengi ikiwemo kupunguziwa madaraka ya kiutawala, na kuondolewa madarakani kwa nguvu ya umma.

Kutokana na hali hiyo, watawala waliona kuwa kuingia kwa mfumo wa vyama vingi kungeleta upinzani ambao wasingeupenda kwa kuhoji na kukosoa mambo mbalimbali ya kiutawala namna yanavyoendeshwa na viongozi husika waliomo madarakani.

Hata hivyo, kwa kuwa mabadiliko ni jambo la lazima katika kuleta maendeleo, nchi nyingi zililazimika kukubali kuingia katika mfumo huo kutokana na mazingira na matakwa ya kidunia kwa kipindi hicho.

Baadhi ya nchi za mwanzo ambazo ziliingia katika mfumo wa vyama vingi kwa upande wa Afrika, ni pamoja na Ethiopia mwaka 1991, Kenya mwaka 1990, Malawi mwaka 1993, Tanzania mwaka 1992 na Zambia mwaka 1990.

Pamoja na baadhi ya nchi hizo za Afrika, kwa upande wa Ulaya ya Mashariki, Poland lilikuwa taifa la kwanza kuingia katika mfumo wa vyama vingi.

Kiongozi aliyeongoza mabadiliko hayo aliitwa Lech Walesa ambaye alibadilisha nchi hiyo ya Poland na kuitwa Jamhuri ya watu wa Poland baada ya kusambaratika kwa dola la Kisovieti ikishirikisha nchi za Hungary na Bulgaria zilizojiondoa katika ushirika huo.

Hata hivyo, kiongozi huyo aliongoza taifa hilo kwa mafanikio makubwa kwa kipindi cha muhula mmoja tu wa kutoka 1990 hadi 1995.

Wachambuzi wa mambo waliona kuwa mabadiliko hayo yalileta ukombozi kwa jamii za kimataifa iliyokuwepo wakati huo kwa kuondokana na mfumo uliokuwa kandamizi.

Mfumo kandamizi uliokuwepo wakati huo ulisababisha mateso kwa jamii iliyokupo na hivyo kuwa rahisi kwao kukubali mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo, kuna faida kubwa ya uwepo wa vyama vingi vya siasa duniani. Hili liko wazi. Na unapozungumzia faida ya vyama vingi, ni lazima kutaja mfumo wa utawa wa mabavu na ufalme.

Kwanini? Kwa sababu utawala wa mabavu katika nchi nyingi ulikuwa mbaya ambapo wananchi walikuwa na mateso makubwa kufuatia utawala wa kidhalimu uliokuwepo.

Kadhalika, utawala wa kifalme nao umekuwa kwa miaka mingi ukikandamiza demokrasia na haki za binadamu.

Utawala wa kidhalimu

Utawala wa kidhalimu ulikuwa umejaa uonevu na kuminywa kwa demokrasia na haki za binadamu hali iliyosababisha kuzaliwa kwa wakimbizi wengi katika mataifa husika.

Mfano wa utawala huo wa kidhalimu ni nchi inayoitwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, chini ya Rais Jean-Bédel Bokassa, alitawala kuanzia Desemba 31, 1965 hadi Septemba 1979.

Utawala wa kifalme

Kuna mfano mwingine wa nchi za kifalme ambazo awali zilikuwa zikiendesha utawala wake kwa mtindo wa ubaguzi na hazikutoa uhuru kwa watu wake kwa maana ya kutokuwepo kwa demokrasia lakini ujio wa vyama vingi umezifanya baadhi ya nchi hizo kulegeza taratibu za uendesha wa kiutawala.

Mfano wa nchi hizo ni Oman na Saudi Arabia na zinginezo ambako awali kulikuwa na sheria zilizokuwa za kibaguzi kwa kuwatenga wanawake kuingia katika shughuli za kijamii na uongozi wa serikali.

Lakini hivi sasa nchini Omani wanawake wanashikilia vyeo katika wizara na wameshateuliwa kuwa mabalozi wa nchi nyingi duniani. Pia, wanashikilia nafasi za ubunge na vyeo rasmi katika taasisi kadhaa huku wakitoa huduma katika jeshi.

Hata hivyo, sheria na kanuni zote zilizopo kwa sasa katika Omani hutao nafasi sawa kwa wanawake katika kufanya biashara, huduma za kiserikali na bima za kijamii.

Nako Saudi Arabia baada ya wanawake kutengwa kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuongozi, kwa miaka kadhaa, sasa wameondolewa vikwazo hivyo na muda mfupi ujao wataanza kufaidi matunda ya mabadiliko ya mfumo wa utawala na kiuongozi. Sasa wanawake wana uhuru wa kuendesha gari bila ya pingamizi.

Mfumo huo wa utawala wa kifalme ni wa kurithiana na hivyo wananchi hawana nafasi hata kidogo katika uendeshaji wa nchi yao wala utungaji wa sheria.

Aidha, nchi zenye mfumo huo hakuna misingi mingine ya demokrasia kama vile uchaguzi wa viongozi, vyama vya siasa, na uhuru wa vyombo vya habari.

Vyama vingi Tanzania

Kwa Tanzania, mfumo wa vyama vingi vya siasa ulianza baada ya serikali kuunda tume chini ya uenyekiti wa Jaji Francis Nyalali Februari 1991, chini ya utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ally Hassan Mwinyi.

Tume hiyo iliundwa mahsusi ili kuratibu maoni ya wananchi, nchi nzima, ambapo iliwahoji ili kupata maoni yao kama wanapenda mfumo upi kati ya uliopo kwa wakati huo wa chama kimoja na vyama vingi vya siasa.

Matokeo ya uratibu huo wa maoni ya wananchi, yalionyesha asilimia 20 walikubali uwepo wa vyama vingi vya siasa huku asilimia 80 wakitaka kubaki katika mfumo wa chama kimoja.

Ingawa maoni ya wananchi kwa idadi kubwa ya asilimia 80 walipendekeza nchi kubaki katika mfumo wa chama kimoja, lakini kwa busara za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishauri kura za wachache za asilimia 20 zifuatwe.

Hii ilitokana na ukweli kwamba kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa lilikuwa jambo lisiloepukika kwa wakati huo kutokana na kuchangiwa na vuguvugu

Aliyewahi kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa, katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari alisema serikali iliamua kufuata maoni ya wananchi wachache kuhusu mfumo wa vyama vingi kwa kuzingatia hali halisi ya matakwa ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa wakati huo.

“Hatua ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa kuchagua idadi ndogo ya kura za maoni (asilimia 20) ya wananchi ilitokana na hali halisi ya matakwa ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kwa wakati huo,” alisema Tendwa.

Wachambuzi wa duru za kisiasa na kijamii waliona kuwa huo ulikuwa ni uamuzi wa busara kwani ndani ya mfumo huo kuna ushindani wa fikra, mawazo na sera na taratibu mbadala kwa kuongoza nchi kwa misingi ya kidemokrasia yenye kuheshimu utu na kulinda haki za binadamu.

Faida ya vyama vingi

Kwa ujumla mfumo wa vyama vingi una faida kubwa katika nchi husika, unaongeza wigo wa kidemokrasia katika jamii husika.

Uongozi wowote katika nchi ya vyama vingi, unafuata misingi ya kidemokrasia yenye kuheshimu utu na kulinda haki za binadamu. Hii maana yake ni kuwa vyama vingi ni kuleta ushindani wa kisiasa na maendeleo ya nchi.

Mfumo huo huziba na kuzuia mianya aina yoyote iwe ya ufisadi, kutokuwajibika kwa watumishi wa umma na matumzi mabaya ya raslimali za umma, kuisukama serikali iliyoko madrakani kutekeleza majukumu na wajibu wake kwa umma, kwa sababu kunakuwa na upande mwingine ambao una hoji mambo ya kiutendaji ya serikali husika.

Mfumo huo unatoa fursa ya kufuatilia Mihimili Mikuu ya Serikali, kwa maana ya Utawala, Mahakama na Bunge ( checks and balance), kuona na kufuatilia mienendo ya mihimili hiyo kama inawajibika ipasavyo kwa mujibu wa katiba.

Athari bila vyama vingi
Nchi zilizokuwa zikifuata mfumo wa chama kimoja katika utawala wake zimekuwa zikisababisha athari nyingi kwa jamii kutokana na kukosekana kwa demokrasia na utawala bora.

Nchi nyingi zenye mfumo wa chama kimoja cha siasa zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na viongozi wake kuminya demokrasia shirikishi, hivyo kukosa kukubalika na jamii yote.

Hili limeanza kuonekana katika baadhi ya nchi duniani kufanya mambo kinyume cha matakwa ya wengi huku viongozi wengine wakibadilisha katiba za nchi zao ili waongoze bila ukomo.

Kwa maana hiyo, mazingira yanayoonekana katika uchambuzi huu yanadhihirisha umuhimu wa uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa taifa, kwani faida zake zimeleta mabadiliko makubwa kwa jamii.

Mwandishi wa makala haya ni mchambuzi wa mambo ya kisiasa, kijamii na kijeshi. Anaptikana kwa simu; 0713 236727

Tagsslider
Share: