Habari

HUZUNI NA MALALAMIKO YA MAMA MZAZI WA MSHTAKIWA WA KESI YA UGAIDI ANTAR HAMOUD AHMED

KUTOKA KWA:
AZIA ALI MUHAMED
MAMA MZAZI WA MSHTAKIWA
ANTAR HAMOUD AHMAD
ZANZIBAR
TEL: 0777 476210

BARUA YA WAZI KWA:
MKURUGENZI WA MASHTAKA (DPP) TANZANIA
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA TANZANIA
MWENYEKITI WA TUME YA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA

YAH: HUZUNI NA MALALAMIKO YA MAMA MZAZI WA MSHTAKIWA WA KESI YA UGAIDI ANTAR HAMOUD AHMED P129/ 2014

MAZUNGUMZO NILIYOFANYA NAE GEREZANI SEGEREA.
Mara nyingi nilipokuwa nikienda kumuona mwanangu gerezani katika siku tofauti alikuwa na mengi ya kuniambia juu ya kilichomsibu hadi kukamatwa kwake, na mimi nilimtaka anieleze ukweli bila ya kunificha kitu ili nifahamu ni nini hasa kilichosababisha akamatwe, ingawa muda wanaopewa gerezani kuzungumza na familia zao wanapokwenda kuwatembelea unakuwa ni mchache mno tena katika mazingira magumu kuelewana, kwahiyo ilinilazimu kusafiri mara kwa mara kwenda Dar es salaam kumuona na kuongea nae hali ya kuwa afya yangu hainiruhusu kutokana na maradhi niliyo nayo na uzee, hata hivyo ilichukua miezi kadhaa hivi mpaka nilipomuelewa na baada ya kumuelewa ndipo nilipoipata sura halisi ya kukamatwa kwake, na hapo ndipo nilipoamua kuandika huzuni zangu na masikitiko yangu kwa viongozi husika na watanzania na kwa walimwengu kwa ujumla ili waweze kupima ukweli na uhalisi wa shutuma hii nzito aliyopewa mwanangu ya ugaidi.

KUKAMATWA KWAKE.
Ilikuwa ni siku ya Jumatatu tarehe 01/07/2014 asubuhi mapema nililetewa taarifa ya kuwa mwanangu amekamatwa nyumbani kwake na kuchukuliwa na polisi usiku wa jana mnamo saa 6 usiku, hapo nilipata mshtuko mkubwa na ikawa chanzo cha kuzidi kwa maradhi yangu, kisha nikaanza kujiuliza maswali mengi ni nini hasa kilichosababisha mwanangu akamatwe, bila kuchelewa tulikutana familia na tukaanza kufuatilia kila kituo cha polisi ili kupata taarifa zake, hata hivyo jitihada zetu hazikufanikiwa na baada ya siku 17 (kumi na saba) tukasikia taarifa kwenye vyombo vya habari kupitia magazeti na runinga ameshtakiwa katika Mahakama ya Mkoa Kisutu siku ya tarehe 17/07/2014 kwa shutuma ya ugaidi, taarifa hii ilinishtua sana na kuzidi kuniathiri afya yangu na nikamfikiria mwanangu yuko katika hali gani kwa vile hajawahi kushutumiwa wala kushtakiwa na vyombo vya dola hata mara moja.

KUHOJIWA NA POLISI
Miongoni mwa yale aliyoniambia akiwa Segerea ni kwamba baada ya kufikishwa Dar es salaam alipelekwa katika nyumba moja katika eneo la Msasani siku ya tarehe 06/07/2014 kwa ajili ya kuhojiwa, na katika mahojiano aliulizwa kuhusu historia ya maisha yake, elimu yake, kazi alizowahi kufanya na nchi alizowahi kutembelea, lakini alishangazwa pale walipomnasibisha na UWAMSHO na akawajibu kuwa yeye hana uhusiano nao wowote, wala si kiongozi, wala si muhadhiri wala hajawahi kuhudhuria mikutano yao ya hadhara hata mara moja. Akawaambia isipokuwa wakati fulani “niliwahi kukutana na UWAMSHO mara kadhaa hivi na sababu iliyonifanya nikutane nao ni pale mahakama ilipotangaza dhamana za mashekhe wa UWAMSHO walikuwa gerezani (rumande) wakati ule, na mimi shida yangu nilitaka kujua taratibu za kisheria na namna ya kufuatilia dhamana hiyo, kwa lengo la kumchukulia dhamana ndugu yangu ambaye alikuwa ni miongoni mwa masheikhe waliokuwa gerezani”, kisha akaendelea kunambia kuwa “mama nimegundua kuwa walionihoji dhana yao kubwa ililenga kuwa mimi ni UWAMSHO lakini mama mimi niko tayari ikiwa kuna mtu yeyote ambaye anaweza kujitokeza na kuthibitisha kuwa mimi nahusika na dhana hiyo basi ajitokeze”
Aidha mwanangu alinieleza juu ya imani yake kwa chombo kinachochunguza tuhuma yake kwa alichohojiwa hakuona jambo la kumtia matatani kwani jambo la kutaka kumchukulia dhamana ndugu yake lipo kisheria kwa yeyote Yule anaye dhaminika, hakika mwanangu ananambia alijawa na tama kubwa kwamba asingeendelea kushikiliwa mpaka sasa kwakuwa hakuna baya aliloliona kwenye mahojiano yake.

KUHARIBIKA KWA KAZI NA BIASHARA ZAKE.
Katika jumla ya mambo aliyonieleza, ambayo yanamfanya aishi katika mazingira magumu gerezani na kuathirika kisaikolojia ni kule kuharibika kwa kazi zake na biashara zake kwa kiasi kikubwa, kati ya kazi zilizoharibika ni kule kukwama kwa miradi miwili (2) anayoisimamia, ambayo iko chini ya mamlaka ya vitega uchumi Zanzibar ZIPA, mradi wa kwanza unanihusu uwekezaji kutoka Kenya wa kampuni ya BLUE HORIZON INVESTMENT CO. LTD I.P.Z ambapo yeye ndiye muwakilishi na meneja mkuu wa kampuni hiyo. Mradi huu unatarajia kujenga kiwanda cha mafuta ya kupikia aina ya SUNFLOWER (ALIZETI) mradi huu unatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani Milioni kumi na mbili ($ 12,000,000). Kwa hatua ya mwanzo na kuajiri wafanyakazi wasiopungua 150 na tayari serikali imeshawapatia eneo ndani ya bandari ya Zanzibar (Malindi) kwa ajili ya kujenga atenki ya kupokea na kuhifadhi mafuta ghafi yanapowasili kwa njia ya meli kisha kupelekwa kiwandani na kusafishwa, kisha kujazwa katika ujazo tofauti. Na mradi wa pili ni ule wa kampuni ya SINDBAD COMPANY LTD. Ambapo yeye ni Director, mradi huu ni wa kiwanda cha kutengeneza sabuni nyeupe ya unga na sabuni ya maji. Mradi huu unatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani Laki Tisa na Elfu Tisini ($ 990,000) kwa hatua ya mwanzo na kuajiri wafanyakazi wasiopungua 60. Chakusikitisha mpaka sasa miradi hii imekwama kama vile kujenga matenki ya kuhifadhia mafuta na kukamilisha baadhi ya taratibu za serikali kutokana na kuwekwa kizuizini kwa miaka mitano sasa.

HISIA ZAKE:
Kadhalika alinieleza hisia zake kuhusu marafiki zake wa muda mrefu namna walivyozipokea taarifa juu ya tuhuma alizopewa ambazo kwa kiwango kikubwa si kwamba zimeathiri haiba yake tu kwa jamii bali pia zimeathiri familia yake na jamii ambayo ingenufaika na uwekezaji wake, ajira kwa wazawa na kodi kwa serikali.
Tuhuma zinazohusiana na ugaidi si tu zinaathiri uwekezaji peke yake bali zinaathiri hata mahusiano ya kijamii, hivyo hata baada ya kunasuka katika kadhia hii mtu humchukua muda mrefu kujenga upya imani kwa jamii yake na wadau wa uwekezaji, kwani tayari alishaweka makubaliano na oda za bidhaa kama vile malighafi (row marerial) paking material na baadhi ya mitambo mbalimbali kwenye baadhi ya makampuni ya China. Hivyo kwa mtu anaepima mambo kamwe hawezi kupata utulivu wa akili na moyo wake hasa pale inapokuwa tuhuma zenyewe ni tofauti na muonekano wa muhusika.

KILICHONILIZA
Kwa haika nilishindwa kujizuia kulia pale nilipoyaona macho ya mwanangu yakitiririka machozi wakati alipokumbuka uhusiano mwema aliokuwa nao kati yake na baadhi ya watendaji wa chama cha CCM na serikali ambapo kupitia mahusiano hayo aliwahi kutoa michango mbalimbali na kusaidia katika kufadhili chaguzi kadhaa zilizopita na alikuwa ni mwenye kushiriki katika tenda mbalimbali za serikali. Iweje leo mtu huyu abebeshwe tuhuma kubwa namna hii, ni wazi kwamba uhusiano huu na marafiki zake utakuwa umefifia.
Mwanzo haikunipitia akilini kuwa ingechukua miaka 5 (mitano) kabla ya upelelezi dhidi ya tuhuma juu ya mwanangu kukamilika, na hii ni kutokana na namna alivyomuwazi kwa jamii yake na uwaminifu wake kwa nchi yake.

WITO WANGU
Kwa heshima na taadhima baada ya kuelezea mkasa wa mwanangu mpendwa sasa napaza sauti na kilio changu kwa wadau wa haki za binadamu sambamba na wahusika wa masuala ya katiba na sheria kusema yafuatayo:-
Sina shaka hata kidogo kwamba kushikiliwa mwanangu na vyombo vya usalama ni jambo lililofanywa kwa dhamira njema kabisa ya kutaka kujiridhisha juu ya tuhuma dhidi yake.
Mpaka wakati naandika barua hii tayari imetimia miaka 5 (mitano) na upelelezi wa kesi aliyopewa haujakamilika.
Nikiwa kama mama mzazi wa mtuhumiwa ambaye nyuma yake kuna orodha ndefu ya nguvukazi muhimu kwa nchi yake tangu ile ya familia yake mwenyewe, ndugu zake, jamaa marafiki na waliotarajia kunufaika na ajira katika uwekezaji wake, nimeshindwa kabisa kuendelea kubaki kimya pasi na kujua hatima ya mwanangu.
Miaka 5 (mitano) bila ya kukamilika kwa upelelezi nikipindi ambacho kinatosha kuiruhusu shaka, huzuni na simanzi kungia katika moyo na akili yenye kupima mambo. Kama mama mzazi wa mtuhumiwa na mzalendo wa nchi yangu kabisa nimeshindwa kuzizuia hisia za uchungu wa mama kwa mwanawe na hivyo nimeona ni vyema nitumie njia hii kuongea na nyote mnaohusika na jambo hili kwa njia moja au nyingine ili kulitupia jicho la makusudi suala hili ili kulipatia ufumbuzi.
Kamwe siandiki kwa nia ya kulaumu au kushutumu bali nimeandika kuziomba mamlaka husika zinazoongozwa na watu wenye uweledi wa mambo, wenye hisia za huruma kwa watoto wao na wenye mioyo laini na yenye kujali hisia za wenzao, kwamba miaka 5 (mitano) inatosha kujiridhisha na hivyo kufanya maamuzi.
Nimejawa na matumaini mengi kuwa kilio na huzuni zangu hazitopuuzwa.

Ahsante

Mama Mzazi wa Mshtakiwa

…………………………
AZIA ALI MUHAMMED

Tagsslider
Share: