Habari

IGP: Maalim Seif anachochea vurugu Zanzibar

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu

Solome Kitomari
18 Julai 2016

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu ametaka Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ashtakiwe mahakamani kwa tuhuma za uchochezi Zanzibar.

Akizungumza alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni jana, IGP Mangu alisema jalada la tuhuma dhidi ya Maalim Seif liko tayari kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP).

IGP Mangu alisema Uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, na ule wa marudio Machi 20, mwaka huu, ulifanyika kwa amani lakini baada ya Maalim Seif kuitisha vikao vya ndani katika maeneo mbalimbali ya Kaskazini Unguja na Pemba na kuchochea wafuasi wake kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, ndipo matatizo yalipoanza.

“Hali ya Zanzibar inaendelea kuimarika, ilichafuka kidogo baada ya Maalim Seif kuchochea wafuasi wake kuwanyamazia wana CCM na kuwanyima huduma kwenye maduka na kutumia biashara kufanya siasa, kususia misiba na hata CCM walivyoenda kwenye misiba yao CUF waliwafukuza, yote haya ni matokeo ya mikutano ya Seif ambayo ilifanyika chini kwa chini, ” aliongeza Mangu.

IGP alidai vikao vya Maalim Seif na wafuasi hivyo vilichochea matukio ya uvunjifu wa amani na kutolea mfano kuchomwa moto kwa mashamba ya wapinzani wa CUF.

IGP alisema licha ya Maalim Seif kuachiwa baada ya mahojiano na jeshi, lakini aliongeza jalada lipo kwa DPP kinachosubiriwa ofisi hiyo kukamilisha taratibu zao ili ashitakiwe kwa kuchochea fujo.

Aidha, alisema kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na jeshi hilo, hali ya usalama itaendelea kuimarika na polisi watawafuatilia wafuasi wa CUF watakaoendelea kumsikiliza Maalim Seif na kufanya uhalifu.

Maalim Seif alihojiwa Mei 30, mwaka huu, kwa saa tatu na polisi huko Zanzibar kwa tuhuma za uchochezi. Alipoulizwa uwezekano wa kuwapo kwa mazungumzo na pande zinazovutana, Mangu alisema kazi yao (Polisi) si kupatanisha bali kuangalia kama kuna jinai na kuwakamata wahusika na kulinda amani wanapofanya kunapokuwa na muafaka.

“Sisi tunachukua hatua kwa wahalifu. Kama wanachukua hatua za kisheria kumaliza tofauti zao hatuna tatizo, wasichukue hatua za kijinai kumaliza tofauti zao au kukomoana wakifika hapo tutashughulika na wanaokomoa wenzao, na bahati mbaya wakiwa ni wa upande mmoja tutawashughulikia hata zipigwe kelele namna gani,” alitahadharisha IGP Mangu.

Alisema kazi ya polisi haifanyiki kwa kificho bali kukamata, kupeleleza na kupeleka mahakamani, na wanafuata taratibu za kisheria kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

“Wanasiasa wana utashi wao, wanalazimisha kutupeleka (polisi), ambako hatutaki kupelekwa. Tutafanya kazi yetu ya kuwatuliza na kukamata wanaofanya makosa ya jinai,” alionya IGP Mangu..

Share: