Habari

Ijue katiba ya nchi yako

Ijue katiba ya nchi yako
December 27, 2017

UTANGULIZI

Katiba ni sheria mama inayoongoza sheria nyengine zinazotakiwa kutumika katika nchi, katiba inatoa haki na kuunda taasisi muhimu katika nchi ili kuendesha utawala wao pamoja na kueleza kazi na mipaka ya taasisi hizo, hivyo taasisi muhimu ambazo zinaongoza nchi yoyote ile huwa zinaundwa kikatiba na hutakiwa ifate miongozo na taratibu zilizoekwa na katiba husika, taasisi hizo ni pamoja na Serikali, Bunge au Baraza la Wawakilishi na mahakama.

MAANA YA KATIBA

Katiba imetafsiriwa katika maana tofauti na wahusika tofauti. Kuna waliosema kuwa; Katiba ni taratibu za msingi zinazazotumika katika kuweka masharti ya uhusiano wa watu na mambo yao muhimu katika kundi au jamii Fulani.
Aidha Kwa mujibu wa Sheria ya mabadiliko ya Katiba sura ya 83 toleo la mwaka 2012 imeelezwa kuwa:-

“Katiba ni sheria ya msingi, iliyoandikwa au isiyoandikwa, ambayo inaweka mfumo wa taifa kwa kuainisha misimgi ya taifa ambayo jamii italazimika kuifuata, mgawanyo wa madaraka na majukumu ya mihimili mikuu ya dola, kwa kuainisha muundo wa serikali, Bunge, na Mahakama, usimamizi wake mgawanyo na ukomo wa mamlaka ya vyombo mbalimbali vya dola, na kwa kuainisha namna na taratibu za utekelezaji wa mamlaka ya vyombo hivyo”.

Kutokana na maana hizo Katiba inaweza kuwa ya familia, kikundi cha ngoma, klabu ya mpira, jumuhiya isiyo ya Kiserikali, chama cha siasa, Katiba ya nchi n.k.

MAANA YA KATIBA YA NCHI

Katiba ya nchi ni maamrisho maalumuu ya msingi yenye nguvu za kisheria yanayounda vyombo au ngazi tofauti za kiutawala ambazo ni muhimu katika kuendesha nchi na kuziekea kazi zake na pia kuweka taratibu muhimu za kufuatwa katika utendaji kazi wa vyombo na taratibu nyingine zinazohusu maisha ya watu.

Katiba ya nchi pia ni msingi wa chimbuko la sheria zote nchini (sheria mama) pamoja na uwezo wenyewe wa kutunga na kuendesha utawala kwa mujibu wa sheria. Kwani Katiba hugawa nguvu za dola kwa vyombo vikuu vitatu yaani vyombo vya utungaji wa sheria, vyombo vya utendaji na vyombo vya utoaji haki.

Kwa ufupi kabisa tunaweza kusema kuwa Katiba ya nchi ni mjumuiko wa misingi muhimu inayotumika katika kuendesha utawala mzima wa nchi.

Ikumbukwe kwamba Katiba ya nchi ni yale masharti au maamrisho ya msingi ambayo yanategemewa kuingia katika sheria ya nchi, na maamrisho mengine yanayopaswa kutungiwa sheria yanatungiwa sheria nyingine kulingana na matakwa ya nchi au jamii inayohusika. Kwa sababu haiwezekani masharti au maamrisho yote yanayohitajika kuendesha nchi yawekwe katika Katiba hivyo lazima ziwepo na sheria.

HADHI YA KATIBA YA NCHI

Katiba ndio chombo kikuu kwa Taifa lolote ulimwenguni hivyo hadhi yake imejieleza katika Katiba yenyewe katika Kifungu cha 4 ambacho kinaeleza kuwa

“Katiba hii ni katiba ya Zanzibar na itakuwa na nguvu za kisheria nchini kote na na ikiwa sheria yoyote inatofautiana na Katiba , basi katiba hii ndio itakayokuwa na nguvu na sheria hiyo itakuwa batili kwa kiwango kile ambacho kinatofautiana.”

Hivyo ni jukumu letu kuilinda, kuisimamia, kuiheshimu na kuilinda kaba pamoja na taratibu zake zote.

AINA ZA KATIBA

Kuna aina kuu mbili za katiba .

1. Katiba iliyoandikwa. Mfano wa nchi wanaotumia Katiba hizo ni marekani, Kenya, Jamhuri ya muungano wa Tanzani na Zanzibar.

2. Katiba isiyoandikwa, Mfano wa nchi wanaotumia Katiba hizo ni Uengereza na Israil.

TARATIBU ZILIZOPITIWA KATIKA UTAYARISHAJI WA KATIBA ZA NCHI KWA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA ZANZIBAR

kutoka na Historia ya utayarishwaji wa Katiba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar inaonesha kuwa kuna njia kuu tatu za utayarishwaji wa Katiba za nchi ambazo ni kama zifuatazo:-

1) Zilizotayarishwa kwa njia ya mapatano (Negotiation).

2) Zilizotayarishwa kwa njia ya Bunge/ Baraza la Wawakilishi.

3) Zilizotayarishwa kwa njia ya ushirikishwaji wa wananchi.

ZILIZOTAYARISHWA KWA NJIA YA MAPATANO (NEGOTIATION).

Ni Katiba iliyopatikana kwa njia ya Mapatano kati ya wenyeji wanchi pamoja na wakoloni. Katika aina hii ya utayarishwaji wa Katiba, historia zinaeleza kuwa katiba za kwanza katika sehemu zote mbili kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zilipatikana kwa njia ya mapatano, ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata Katiba ya Tanganyika mwaka 1961 na Zanzibar ilipata Katiba ya Uhuru 1963.

Mapatano hayo yalifanyika kati ya Wenyeji wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na wakoloni (watawala wa kipindi hicho). Kama ifuatavyo:-

 Katiba ya Tanganyika ya Uhuru ya Mwaka 1961(Independence Constitution of 1961)
Katiba Hii ilipatikana kupitia Order in Council mwaka 1961 ambapo ilitungwa Uengereza na ilitungwa na Bunge la Uingereza pamoja na baadhi ya Watanganyika katika nyumba yao maalum ya kutungia sheria inayojuulikana kwa jina la “Lancaster House ” na baadae kuletwa Tanganyika na kuwakabidhi pamoja na Uhuru wao.

 Katiba ya Uhuru ya Zanzibar ya 1963. Aidha kwa upande wa Zanzibar Katiba ya kwanza ilikuwa ni Katiba ya Uhuru ambayo nayo ilipatikana kwa njia ya mapatano nchini Uengereza kama ile ya Tanganyika na kukabidhiwa Katiba hiyo pamoja na uhuru wao 1963.

Katiba zote mbili zilitoa mamlaka ya kimaeneo na kumtambua Sultani ndio kiongozi wan chi kwa upande wa Zanzibar na Queen kwa Upande wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Hivyo kupitia katiba hizi wenyeji walipewa kazi ya kuendsha Serikali tu ambapo kwa Tanganyika alikuwa Mwalim Julias K. Nyerere na Zanzibar ni Moh’d Shamte.
Hivyo Uongozi kamili wa nchi pamoja na Ulinzi wa nchi ulibaki kwa wakoloni.

ZILIZOTAYARISHWA KWA NJIA YA BUNGE/ BARAZA LA WAWAKILISHI

Ni aina za Katiba zilizopatikana kwa njia ya Bunge au Baraza la Wawakilishi. Njia hii ilitumika baada ya Uhuru kwa nchi zote mbili kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, kwa kueka madaraka kamili kwa viongozi waliokuwepo madarakani mamlaka hayo ni pamoja na:-

 Uongozi kamili wa nchi

 Uendeshaji wa Serikali

 Ulinzi wa nchi.

Hivyo mamlaka hayo yaliwekwa katika Katiba za nchi, Katiba hizo ni kama ifuatavyo:-

 Katiba ya Jamuhuri ya 1962 (The Republican Constitution of 1962)

Ilianza kwa pendekezo la Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika. Pendekezo hili lilijadiliwa na Katiba hii kupitishwa katika Bunge, ambapo bunge hilohilo lilijigeuza kuwa Bunge Maalum la Katiba kupitia Sheria ya Bunge.

 Katiba ya Muda (mpito) ya Mwaka 1965(The interim Constitutionof 1965).

Katiba hii ilipatikana kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na iliitwa Katiba ya Mpito kwa sababu ilikusudiwa kutumika kwa muda Fulani tu na hatimae kutengenezwe Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo Katiba hii ilitoa nguvu ya chama kushika hatamu.

kupitia ripoti ya Tume iliyotolewa na Mwalimu Nyerere, Bunge la Jamhuri lilipitisha sheria iliyotangaza Katiba ya Muda ya Tanzania na kutangaza chama kimoja cha siasa Tanzania Bara na chama kimoja cha siasa Zanzibar. Kwa mantiki hii, Tanganyika African Nation Union (TANU) kilikuwa chama cha siasa kwa upande wa Tanzania Bara na Afro Shirazi Party (ASP) kilikuwa chama cha siasa kwa upande wa Zanzibar.

 Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

Katiba hii ni zao la Muungano wa vyama viwili vya siasa, TANU na ASP, ambapo baada ya kuungana ikajuulikana kwa jina la C.C.M, Tarehe 16 Machi 1977, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Notisi ya Serikali (Government Notice) Namba 38 ya tarehe 25-3-1977, aliteua Tume ya watu ishirini wenye idadi sawa kwa kila upande, ikiwa kumi kutoka Tanzania Bara na Kumi kutoka Zanzibar kutayarisha mapendekezo ya Katiba.

Wakati huo huo, kupitia Notisi ya Serikali (Government Notice) Nam 39 ya tarehe 25-3-1977, aliteua wawakilishi wa Bunge la Katiba kujadili mapendekezo ya rasimu ya tume. Tarehe 25-4-1977, Bunge la Katiba lilijadili na kupitisha mapendekezo ya Katiba ya Jamuhuri ya Muunganowa Tanzania ya mwaka 1977.

 Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya 1979

Katiba ya uhuru ya 1963 haikuchukua muda mrefu na yakafuatia Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyofanyika tarehe 12 Januari 1964 na baada ya hapo Zanzibar hapakuwa na Katiba na badala yake Baraza la Mapinduzi lilipitisha Sheria mbali mbali ambazo ziliweka taratibu za kuendesha shughuli mbali mbali za nchi.

Mnamo mwaka 1979 Zanzibar chini ya Uongozi wa Mh. Rais Aboud Jumbe ilipitisha Katiba iliyojulikana kwa jina la Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya 1979, Katiba hiyo mpya ambayo pamoja na mambo mengine lianzisha Baraza la Wawakilishi kuwa ni chombo kikuu cha Kutunga sheria. Katiba hii ilidumu hadi mwaka 1984.
 Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984

Mnamo mwaka 1984 Baraza la Wawakilishi lilifuta Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979 na katika Kikao cha tarehe 9 Octoba 1984 likapitisha Katiba ya Zanzibar ya nwaka 1984 ambayo mbali na kuwa na marekebisho mbali mbali, kwa sasa imefikia marekebisho ya kumi pia ni Katiba inayotumika Zanzibar hadi sasa.

ZILIZOTAYARISHWA KWA NJIA YA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI.

Ni miongoni mwa Katiba zinazofuata mfumo wa demokrasia kwa sababu utayarishwaji wake unahusisha wananchi moja kwamoja. Njia hii inamrahisia mwananchi kujua Katiba yake kwa urahisi kwavile ameshirikishwa wakati wa utayarishwaji na kupelekea kuondosha baadhi ya lawama zinazozikabili Katiba za nchi.

Miongoni mwa Katiba zilizotayarishwa kwa njia hii ni kama ifuatavyo:-

 Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Katiba hii imeshirikisha wananchi katika marekebisho yake ya kumi yaliyofanyika mwaka 2010 kuhusiana na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika katiba hii Kifungu cha 80A KINAELEZA nafasi ya wananchi katika utungaji wa Katiba kwa kupitia Kura ya Maoni.
Ushuhuda wa hili ni mwaka 2010 baada ya kurekebishwa Katiba hii, kwa kuanzishwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambapo katika kuipata serikali hiyo wanachi walipiga kura ya ndio na Hapana kwa imani ya kuikubali ama kuikataa Serikali hiyo.

Aidha kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba sura ya 83 toleo la 2012 limetoa ruhusa kwa Wananchi kushiriki katika kutunga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( ambayo hadi sasa nawasilisha mada hii rasimu ya pili ipo Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa).

Lakini mara tu wabunge wa Bunge la Katiba Kumaliza kazi ya kuijadili Rasimu ya pili ya Katiba italetwa kwa Wananchi kupiga kura ya ndio au Hapana juu ya Katiba hiyo.

TARATIBU ZA KUFANYA MAREKEBISHO YA KATIBA KWA JAMHURI YA MUUNGANO NA ZANZIBAR

Katiba hubadilika na kutayarishwa au kurekebishwa nyengine kutokana na mabadilko kwa jamii yalivyo, kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katiba hubadilika kwa utaratibu ufuatao:-

a) Kutakuwa na Mswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha katiba , Hoja ya mswada huo itakapoungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote. Ibara ya 98(a) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

b) Kwa masuala ya Muungano, Kutakuwa na Mswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha katiba , Hoja ya mswada huo itakapoungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzani na theluthi mbili kutoka Zanzibar, Ibara ya 98(b) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

Aidha kwa upande wa Zanzibar Katiba inaweza kubadilishwa au kurekebisha kupitia njia mbili kuu kama zifauatazo-:
a) Kutakuwa na Mswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha Katiba , Hoja ya mswada huo iungwe mkono na theluthi mbili ya wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi. Kifungu cha 80(1) Katiba ya Zanzibar.

b) Kutakuwa na Mswada wa sheria kwa ajili ya kubadilisha ama kurekebisha Katiba, Hoja ya mswada huo yakubaliwe na wananchi kwa Kura ya Maoni. Kifungu cha 80A Katiba ya Zanzibar ya 1984.

Maombo yanayohitaji ridhaa ya wananchi kwa kura ya maoni ni pamoja na:-

 Vifungu vyote vya sura ya kwanza katika sehemu ya kwanza, mfano Zanzibar na mipaka yake, masuala ya
muungano, muhuri wa serikali, vyama vingi n.k

 Kifungu cha 9, (Zanzibar itakuwa ni nchi ya kidemokrasia)

 Vifungu vyote vya sura ya tatu, (kinga na haki za lazima, wajibu na uhuru wa watu binafsi), (haki za binadamu)

 Kifungu cha 26. (Afisi ya Raisi na sifa za kuchaguliwa kuwa Raisi)

 Kifungu cha 28 (muda wa kuendelea na uraisi)

 Kifungu cha 80A (kura ya maoni kwa baadhi ya mabadilko ya Katiba) n.k

HITIMISHO

Katiba ndio msingi mkuu wa Binadamu katika nchi yake kwani inatoa picha halisi ya maisha ya mwanadamu kielimu, kiafya, kiusalama pamoja na haki za msingi, kutokana na hilo ni vizuri Katiba zikashirikisha wananchi moja kwa moja katika utayarishaji au ubadilishaji wa Katiba za nchi ili ziende sambamba na maisha ya mwanadamu.

“Ni jukumu la kila mwananchi kuilinda, kuiheshimu na kuisimamia Katiba ya nchi”

Pembatoday

Tagsslider
Share: