Habari

IKULU YAINGIA WAZIWAZI

Sasa Ikulu yaingia waziwazi mgogoro wa CUF kuwaokoa Lipumba, Mutungi

  • Njama za kumvua uwanachama Maalim Seif zaiva
  • Ni baada ya kutishwa na ziara ya Katibu Mkuu Jumuiya ya Madola

Baada ya juma lililopita kupatikana habari za mkakati wa kambi ya Profesa Ibrahim
Lipumba, anayetambuliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi, kumfukuza katibu mkuu wa chama hicho,
Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kuandaa mkutano mkuu ‘feki’ kwa kushirikiana na ofisi ya
msajili huyo, taarifa za ndani zimezidi kuanika msingi wa mkakati huo na nani aliye nyuma
ya jambo hilo.

Mzalendo.Net imebaini kuwa Maalim Seif anawindwa ‘kufukuzwa uanachama’ kinyume na
sheria na taratibu ili kuinusuru Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na kibano cha
kutengwa na jumuiya ya kimataifa kufuatia kutotekeleza sharti la kuirejesha Serikali ya
Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) na makabidhiano ya ushindi kwa mshindi kufuatia
uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015.

Awali, jumuiya ya kimataifa ilitegemea SMT ingeliingilia kati mgogoro wa uchaguzi
uliotokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum
Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo na kuitisha mwingine tarehe 20 Machi 2016, ambao
ulisusiwa na CUF na kupingwa na jumuiya hizo ya kimataifa iliyotoa msimamo wake wazi
wazi wa kutokubaliana na jambo hilo.

“Jambo hilo limeiweka Zanzibar katika hali mbaya kiuchumi, kidiplomasia na kisiasa.
Matarajio kuwa Serikali ya Muungano ingeliingilia mgogoro huu, yalitokana na hotuba ya
Rais John Pombe Magufuli katika uzinduzi wa Bunge (la Jamhuri ya Muungano mjini
Dodoma) mwezi Novemba 2015,” kinasema chanzo chetu kilicho karibu na serikali zote
mbili, ya Muungano na ya Zanzibar.

Itakumbukwa kuwa kwenye hotuba hiyo iliyoshuhudia Dk. Ali Mohamed Shein akizomewa
na wabunge wa upinzani, Rais Magufuli aliahidi kufanya kila awezalo kulimaliza suala la
Zanzibar kwa kushirikiana na pande zote husika.

Hata hivyo, mara baada ya kutulia Ikulu ya Magogoni, inaonekana Rais Magufuli alipata
ushawishi wa kuachana kabisa na suluhu ya Zanzibar na badala yake akaelekeza nguvu
zake kukinusuru chama chake cha Mapinduzi (CCM) na aibu hiyo na hali hiyo kwa serikali
yake kuandaa mpango wa kukihujumu chama cha CUF kupitia msajili wa vyama vya siasa.
Kwa pamoja, Ikulu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa walimshawishi na hatimaye
kumrejesha Lipumba katika nafasi ya uongozi wa CUF aliyokuwa amejiuzulu tangu tarehe 5
Agosti 2015, miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015.

“Ilikuwa rahisi kumshawishi Lipumba kushiriki mpango huo, kwani alikuwa ameshakubali
pale mara ya mwanzo kushawishiwa ajiuzulu pamoja na Dk. Wilbroad Slaa (aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA) ili kuwasambaratisha
UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi unaoundwa na CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi
na NLD),” kinasema chanzo chengine.

UKAWA itaingia kwenye vitabu vya historia ya chaguzi za vyama vingi nchini Tanzania kwa
kufanikiwa kwa mara ya kwanza kuitikisa na kuipa CCM wakati mgumu katika uchaguzi
mkuu kwa pande zote mbili za Muungano (Bara na Zanzibar).
Chanzo hicho kinasema kuwa baada ya CUF “kuchukua hatua kadhaa za kujihami na
hususani uamuzi wa kukimbilia mahakamani na kufungua kesi zenye mashiko”, sasa

Serikali ya Muungano chini ya uongozi wa Rais Magufuli imeamua kutumia gharama na kila
aina na nguvu kumsaidia Lipumba kufanikisha jambo hilo.

Katika siku za hivi karibuni, nguvu ya dola imejidhihirisha waziwazi kwenye mgogoro wa
CUF baada ya taasisi nne za dola kuonekana kwa wakati mmoja zikijiingiza kichwa kichwa –
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA), Bunge la
Jamuhuri ya Muungano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) – katika mpango wa waziwazi
kusajili wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini ya CUF kinyume cha sheria, kufukuza
wabunge wanane wa viti maalum na kuteua wengine wapya katika utaratibu wa kasi kubwa
mno.

“Tatizo kwao ni kuwa CUF inafunguwa dhidi ya kila hatua wanayoona inawaelemea,
ikiwemo moja ya jinai inayohusu contempt of court proceedings (kwa kughushi nyaraka ili
kuishawishi mahakama isitende haki) dhidi ya Jaji Mutungi kama msajili wa vyama vya
siasa, Emmy Hudson kama kaimu kabidhi na wasii mkuu wa RITA na Thomas Malima,
ambaye ni mkurugenzi wa fedha wa Lipumba,” anasema mwanasheria mmoja wa ngazi za
juu katika Chama cha Mawakili cha Tanganyika (TLS).

Mtandao huu wa Mzalendo.Net umefahamishwa kuwa mara tu baada ya CUF kuamua rasmi
kuwekeza nguvu zake mahakamani kinyume na ilivyotazamiwa na ilivyozoeleka huko
nyuma, ambapo chama hicho hakikuwa kikiamini uwezo na uadilifu wa mahakama, Ikulu
iliamuru kufanyika kwa utafiti na timu ya wanasheria kutoka Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na Msajili wa Vyama vya Siasa kujuwa nafasi ya ushindi kwa serikali kwenye kesi
hizo.
“Ukweli ni kuwa wanasheria waliwaeleza wazi wakubwa wao kuwa katika mashauri yote
yaliyofunguliwa mahakamani, basi msajili hawezi kunusurika kama kesi zitaendeshwa
kiadilifu. Ndipo ikaamuliwa kuwaomba majaji wanaoendesha mashauri ya CUF kusaidia
kumnusuru Jaji Mutungi na kuiokoa serikali kutokana na aibu hii kubwa,” anasema
mwanasheria mwengine ambaye yupo kwenye idara moja muhimu serikalini.

Chanzo chetu chengine kinasema kuwa kazi hiyo alipewa Jaji Mfawidhi Mama Mutungi
(mkewe Jaji Francis Mutungi), lakini majaji wanaonekana kusutwa na nafsi zao kutenda
dhambi hiyo kwa jambo lililo wazi na lenye maslahi na watu wengi.

Matokeo yake, chanzo chetu kinasema, majaji waliishauri Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali itafute mawakili wazuri wanaoweza kuweka mapingamizi kupitia hoja za awali ili
mashauri yaondolewe katika hatua za awali, kwani yakisikilizwa kama yalivyo, hakuna
uwezekano wowote wa kutokipa chama cha CUF ushindi katika takribani mashauri yote
kilichofunguwa.

Mzalendo.Net ina taarifa kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwasiliana na Ikulu
juu ya jambo hilo na ndipo ikulu ikatoa maelekezo kwa Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis
Juma kuhakikisha kuwa kesi zote zinatengenezewa mazingira ya kufutwa kupitia
mapingamizi katika hoja za awali.

Naye, Kaimu Jaji Mkuu Juma kwa kutambuua kuwa hajathibitishwa na hivyo anaweza
‘kutumbuliwa’ wakati wowote, amelichukulia jambo hilo kuwa ni fursa na analifanya kwa kasi
na usimamizi wa karibu sana.

Chanzo chetu kinatueleza kuwa Ijumaa ya tarehe 18 Agoti 2017, Kaimu Jaji Mkuu Juma
alifika katika ofisi ya Jaji Kiongozi na kisha akakutana na Jaji Wilfred Dyansobera katika kile
kilichosemekana ni kumkabidhi hukumu aliyoiandaa ya amri ya kuondoa zuio la ruzuku ya
CUF kwa Lipumba siku ya Jumanne tarehe 22 Agosti 2017.

Aidha kila shauri limeundiwa kamati maalum inayofuatilia, ambazo hukutana kila siku na
kufanya tathmini kisha kutoa mrejesho moja kwa moja Ikulu ili kuiwezesha Ikulu kuelekeza
ifaavyo.

Kasi ya maelekezo ya Ikulu imeongezeka kufuatia ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Madola, Patricia Scotland, kufuatilia mchakato wa utekelezaji wa utatuzi wa mgogoro wa
uchaguzi Zanzibar. Serikali zote mbili – ya SMT na ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) –
zinaamini kuwa endapo Maalim Seif akifukuzwa chama, watapata utetezi kuwa hawawezi
kumkabidhi serikali kwa kuwa hatokani na chama cha siasa.

“Aidha mahakama imeelekezwa kutopokea mashauri mengine mapya kutoka CUF kwa hoja
kwamba kwanza inayashughulikia na kumaliza haya yaliyopo,” kinasema chanzo hicho.
Maelekezo hayo yalijaribiwa kutekelezwa na Msajili wa Mahakama pale CUF ilipotaka
kufungua shauri jipya kuhusiana na wizi wa ruzuku baada ya lile la awali (Na.21/2017)
kuondolewa kwa pingamizi la Jaji Wilfred Dyansibera.

“Awali Jaji Dyansobera alipangua hoja za pingamizi zote zilizowasilishwa, lakini katika hali
yenye utata aliibuka na kile alichosema ni kwa maoni yake shauri lilipaswa kuletwa kwa
kifungu cha 2(3) cha Judicature and Application of Laws Act, ambacho kwa wanaofahamu
sheria wanafahamu kuwa hakisemi chochote kuhusu judicial review, mandamus and
prohibition or prerogative orders (mapitio ya kimahakama),” kinafafanuwa chanzo chetu.
Uamuzi huo ambao taarifa za uhakika zinasema alipewa ausome na kuliondoa shauri
ulikuwa katika karatasi iliyoandikwa kwa mkono tofauti na ile ya uchambuzi iliyokuwa
imechapwa kwa kompyuta ambayo ndiyo alikusudia kutolea maamuzi. Jambo hilo
liliwashangaza wengi kwa sababu miongoni mwa majaji wanaoaminika katika kusikiliza na
kuamua mashauri yanayohusu haki za binadamu, utawala bora, utawala wa sheria na
demokrasia ni Jaji Salvatory Bongole, Jaji Fauz Abdallah Twaibu na yeye Jaji Dyansobera.
Uamuzi wake ulionyesha wazi kuwa kuna mazingira yanayoshinikiza na kuondoa uhuru wa
utendaji kazi wa Jaji Dyansobera.

Hata hivyo, baadaye Msajili wa Mahakama Kuu alilipokea shauri hilo pamoja na lile
lililofunguliwa na wabunge wa CUF, ila taarifa za uhakika zinasema ameelekezwa
asiyapangie jaji miongoni mwa waliopo sasa mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam, na
badala yake panaangaliwa uwezekano wa kumleta jaji kutoka mikoani mahsusi kwa ajili
hiyo.

Hatua hiyo inatokana na Ikulu kuona kuwa huenda majaji waliopo Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam wameshikwa kigugumizi na kuchoshwa na udhalimu unaoendelea dhidi ya
CUF na uvunjwaji wa sheria na haki.

Taarifa zaidi zinasema baadhi ya mawakili wanaosimamia mashauri ya CUF wametishwa
kuwa watavuliwa uwakili iwapo wataendelea kusimamia mashauri hayo. Chanzo cha habari
hizo kinasema baadhi ya mawakili hao wameanza kuchukua hatua za kujihami kwa
kujiondoa katika mashauri mapya yanayowasilishwa mahakamani hapo.

Mtoa taarifa wetu aliye mahakama kuu anasema jambo hilo ni rahisi kufanyika kwa sababu
utaratibu ni kutengeneza malalamiko tu na kuyawasilisha kwa Jaji Kiongozi ambaye
anawezesha mchakato huo katika muda mfupi sana.

Tagsslider
Share: