Habari

Jaji Mshibe: Hatutafika bila utawala bora

April 14, 2018

Ataka utekelezwe kwa dhati sio kuimbwa

NA MASANJA MABULA, PEMBA

MWENYEKITI wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakar, amewaomba viongozi wa taasisi za umma na binafsi kutekeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora badala ya kuzungumza na kuimba kwa maneno huku kukiwa hakuna utekelezaji wa dhati.

Alisema bado kuna baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali na binafsi hawajaonesha nia ya dhati ya kuitekeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora badala yake dhana hiyo inatekelezwa kwa maneno na nyimbo.

Aliyasema hayo wakati akifunga kikao juu ya maadili, rushwa na uendeshaji wa mashtaka kilichoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwenye ukumbi wa makonyo Chake Chake.

Aliwaomba washiriki wa kikao hicho kuwa wazalendo na waumini wazuri wa dhana ya utawala bora katika taasisi zao ili wanaowaongoza waige kutoka kwao.

“Hakikisheni mnaitekeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora na acheni kuizungumza na kuimba midomoni ili kuweza kufanikisha azma ya serikali ya kuimarisha dhana hii, ”alisisitiza.

Aidha alieleza kutoridhishwa na baadhi ya viongozi kukosa maadili na kupenda kujilimbikizia mali kinyume na utaratibu na sheria za utumishi wa umma.

“Kiongozi anaajiriwa leo na baada ya miezi mitatu unamuona anamiliki gari na nyumba, jiulize hela kapata wapi na pia linganisha na mshahara wake, huku ni kukosa maadili,”alisema.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mashaka Kubingwa Simba, alisema sheria haijakataza mtu kumiliki mali hoja ni jinsi alivyoipata.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya kikao hicho, Kubingwa alifahamisha kwamba moja ya majukumu ya tume hiyo ni kupokea matamko ya mali na madeni ya viongozi na kisha kuyafanyia uhakiki.

“Kumiliki mali sio tatizo kwa mujibu wa katiba, tatizo ni jinsi mali hiyo ilivyopatikana, hivyo moja ya majukumu ya tume ni kufanya uhakiki wa matamko ya viongozi waliyoyawasilisha katika ofisi za tume,” alisema.

Zanzibarleo

Share: