Habari

JAJI MUTUNGI AVUNJA AMRI YA MAHAKAMA KUU ILIYOMKATAZA KUTOA RUZUKU YA CUF

THE CIVIC UNITED FRONT

(CUF – Chama Cha Wananchi)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Imetolewa leo Tarehe 11/6/2018

JAJI FRANCIS SALES KATABAZI MUTUNGI [MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA] AVUNJA AMRI YA MAHAKAMA KUU ILIYOMKATAZA KUTOA RUZUKU YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI):

ATOA MILIONI 600 NA KUZIINGIZA AKAUNTI YA LIPUMBA.

UONGOZI WA BENKI WAMKATALIA KUZITOA FEDHA HIZO KUHESHIMU AMRI YA MAHAKAMA KUU.

MASLAHI BINAFSI YA KUPATA GAWIO YAMSUKUMA JAJI MUTUNGI KUVUNJA AMRI YA MAHAKAMA KUU.

LENGO KUITISHWA MKUTANO MKUU FEKI WA LIPUMBA NA GENGE LAKE KUTAKA KUMFUKUZA KATIBU MKUU, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD.

1. THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama cha Wananchi) kinaujulisha umma wa Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa kwamba kimefanikiwa kuzima njama mbaya na zinazoashiria hatari katika uendeshaji wa nchi zikimhusisha Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji Francis Mutungi kutaka kuvunja kwa makusudi AMRI YA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA YA KUZUIA KUTOA FEDHA ZA RUZUKU YA CUF KWA LIPUMBA NA GENGE LAKE.

2. Itakumbukwa kuwa tarehe 29/5/2018, Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya Mheshimiwa Jaji Wilfred Dyansobera ilitoa AMRI YA ZUIO dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakala wao au mtu mwingine yeyote anayefanya kazi chini yao au kwa amri yao kutoa fedha za Ruzuku ya Serikali kwa Chama cha CUF hadi hapo Shauri la Msingi Na. 68/2017 litakapokuwa limesikilizwa na kutolewa uamuzi na/au mpaka hapo Mahakama Kuu itakapotoa maelekezo vinginevyo.

3. Mwenendo wa kesi za CUF zilizoko Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tazania unaonesha kuwa hii si mara ya kwanza kwa Jaji Francis Mutungi kwa kudharau na kuvunja amri za Mahakama, jambo ambalo yeye kama ofisa wa Mahakama alipaswa kuonesha mfano kwa kutolitenda. Tuwakumbushe Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwamba hili ni zuio la pili baada ya lile la kwanza kupitia Shauri dogo Na. 28/2017 lilitolewa tarehe 31/3/2017 kutoheshimiwa pia na mtu huyu ambaye ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

4. Katika uvunjaji wa amri hii mpya ya Mahakama, Jaji Mutungi na ofisi yake walipopelekewa AMRI HIYO YA MAHAKAMA KUU WALIKATAA KUIPOKEA. Hata hivyo siku ya pili yake tarehe 30/5/2018 Wakili Msaidizi wa Serikali Bi. Rehema Mtulia aliyekuwa akimwakilisha pamoja na Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata, alichukua nakala ya AMRI HIYO na kumpelekea mteja wake aliyekuwa anamuwakilisha katika shauri hilo. Kwa msingi huo Msajili Jaji Francis Mutungi kisheria alipokea NAKALA YA HUKUMU NA AMRI YA MAHAKAMA kupitia mawakili wake (Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali). Kwa ufafanuzi wa kisheria ni kwamba uwepo wa wakili wa mdaawa mahakamani wakati wa kusomwa hukumu ni hakikisho tosha kuwa mhusika amepata taarifa hata kama hatakuwa amepelekewa nakala ya hukumu na amri ya mahakama husika.

5. Tunazo taarifa za uhakika kwamba kwa kiburi na jeuri kubwa aliyo nayo Jaji Mutungi dhidi ya mhimili wa Mahakama ambayo yeye ni afisa wake, AMEKATAA KUHESHIMU AMRI HIYO YA MAHAKAMA KUU NA AMEENDELEA NA UTARATIBU WAKE WA KUTOA FEDHA ZA RUZUKU YA CUF KWA LIPUMBA. Tena mara hii ametoa fedha nyingi za walipa kodi (milioni 600) kwa lengo la kumwezesha Lipumba kuitisha MKUTANO MKUU FEKI WENYE AJENDA YA KUMFUKUZA KATIBU MKUU MAALIM SEIF SHARIF HAMAD, VIONGOZI WOTE HALALI WA CHAMA WASIOKUBALIANA NA LIPUMBA, KUTOA TAMKO ALILOAGIZWA NA DOLA LA KUTANGAZA KUMTAMBUA DK. ALI MOHAMED SHEIN NA MATOKEO YA UCHAGUZI BATILI WA MARUDIO WA MACHI 2016 NA KUTOA AZIMIO LA KUTAKA KUFUTA MASHAURI YOTE YALIOFUNGULIWA MAHAKAMANI ILI KUMNUSURU JAJI MUTUNGI NA MKONO WA SHERIA.

6. Hatua hiyo inachukuliwa baada ya ile ya kwanza ya kusajili Bodi feki kugonga mwamba kufuatia kufunguliwa Mahakamani Shauri Na. 13/2017 linalohoji uhalali wa usajili huo.

7. Baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kukataa kupokea Amri Halali ya Mahakama aliyopelekewa na Chama kupitia Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Mhe. Joran Lwehabura Bashange, Chama kilifanya kazi kubwa kufuatilia sababu ya kufanya hivyo na kujiridhisha kuwa Jaji Mutungi alikuwa tayari ameanza mchakato wa kuidhinisha mamilioni hayo ya fedha za ruzuku ya CUF kumpelekea Lipumba ili aweze kufanikisha dhamira na mipango yao ya pamoja ya kutaka kuitisha MKUTANO MKUU FEKI haraka, kwa madhumuni yaliyoelezwa hapo juu; yamkini kutokana na mwelekeo mbaya wa mashauri yanayowakabili Mahakamani, hasa baada ya kugundulika kuwa nyaraka zilizoletwa kama vielelezo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni za KUGHUSHI.

8. Uvunjifu na msukumo huu wa AMRI YA MAHAKAMA KUU si tu ni njama na hila za kutaka kuidhoofisha CUF, bali unathibitisha wazi kauli inayosemwa kuwa Jaji Mutungi anasukumwa kufanya hivyo anavyofanya kutokana na kupata gawio la fedha hizo kutoka kwa Lipumba na kundi lake kila mara anapowaingizia fedha. Hili suala limefika wakati sasa lichunguzwe na mamlaka zinazohusika.

9. THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama cha Wananchi) kinawajulisha kuwa kimetoa taarifa ya Ufisadi, Wizi na Ubadhirifu huu wa fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawa jinsi vita ya Serikali ya Awamu ya Tano kutaka kuidhoofisha CUF na demokrasia kwa ujumla inavyoendelea nchini na kuzinakilisha taarifa hizi kwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, mabenki yote nchini, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Shirika la Umoja wa Mataifa (UNDP), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Madhumuni ni kuzifanya taasisi hizo za Serikali, za kiraia na za Kimataifa kuona unafiki wa kile kinachoitwa uwajibikaji wa serikali iliyoko madarakani na KAULI MBIU YAKE YA VITA DHIDI YA UFISADI.

10. Vitendo hivi vya kuvunja na kudharau amri halali za Mahakama vya Jaji Francis Mutungi tena akiwa ni Ofisa wa Mahakama ambaye angepaswa kuonesha mfano katika kuuheshimu mhimili huo ni vitendo vya aibu kwa mtu mwenye hadhi kama yake na vinaonesha ni jinsi alivyo mtu wa ovyo na asiye na maadili na ambaye yuko tayari kufanya jambo lolote lile kwa kujinufaisha kibinafsi hata kama ni kwa gharama ya kujishushia hadhi na heshima yake na heshima ya taasisi anazozifanyia kazi.

Ni imani yetu kupitia kwenu wana habari Watanzania wataweza kupata taarifa hii muhimu ili kwa pamoja tuweze kushirikiana katika kuhakikisha kuwa vita dhidi ya ukandamizwaji wa haki za kiraia zilizowekwa kwa mujibu wa KATIBA na SHERIA inapiganwa kwa pamoja ili haki hizo ziweze kutunzwa na kwa maana hiyo kuendelea kudumisha HAKI, UADILIFU, AMANI na UTULIVU wa nchi yetu.

HAKI SAWA KWA WOTE

JORAN LWEHABURA BASHANGE
NAIBU KATIBU MKUU (BARA)

THE DIRECTORATE OF INFORMATION, PUBLICITY AND PUBLIC RELATION

P.O.BOX 3637 ZANZIBAR
Director: Salim Biman Zantel No. 0777 414 112 / Voda No. 0752 325 227

Deputy Director: Mbarala Maharagande Airtel No. 0784 001 408 / Tigo No. 0715 062 577

Share: