Habari

Jamii yaaswa kusajili ardhi na kupatiwa hati milki

Na Salmin Juma, Pemba

Jamii kisiwani Pemba imetakiwa kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa na idara ya ardhi kwa kuzisajili ardhi zao na kupatiwa hati miliki zinazotambulika ambayo itamuepusha na migogoro ya ardhi.

Kauli hiyo imetolewa na afisa mtambuzi wa ardhi, Moh’d Salim kutoka Idara ya Ardhi Pemba alipokuwa akizungumza na maafisa wa wilaya pamoja wajasiriamali kutoka katika mikoa yote miwili.

Amesema kuwa imeonekana kwamba wajasiriamali wengi wanakosa fursa za kumiliki raslimali ardhi pamoja na mambo mengine ambayo yanawahusu katika jamii.

Aidha ameitaka jamii kutotumia ardhi kwa shughuli zisizoeleweka bali waitumie kwa maendeleo ya kijamii na kuhakikisha kwamba hawauzi kiholela ardhi zao bila ya kufuata utaratibu wa kisheria ili kuondokana na migogoro hiyo.

Nae mratibu kutoka jumuiya ya NGENEREKO, Mohd Nassor amesema lengo kuu ni kusaidiana na serikali kwa kupunguza migogoro ya ardhi kwani serikali ina nia njema na kuitaka jamii kutumia raslimali zao vizuri.

Hata hivyo amesema kuwa elimu bado ni ndogo kwa jamii hivyo amesema kupitia mradi huo watashirikiana na widhara husika ili kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii.

Akitoa wito kwa niaba ya wenzake, Maryam Mohd Muhene amesema watahakikisha wanachukua juhudi katika kutoa elimu katika vikundi vyao ili kuona kwamba wanachama wote wanakuwa na uwelewa wa kutosha juu ya hati miliki ya ardhi.

ZANZINEWS
Kwa Habari, Picha Na Matukio Tembelea ZanziNews Tangaza Nasi Kwa Bei Nafuu. Tupigie 0777 424152 Au Tuandikie Othmanmaulid@Gmail.com

Share: