Habari

Jamiiforums waburuzwa mahakamani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepanga kuanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri wa kesi inayomkabili Mwanahisa wa  mtandao wa Jamii Forums, Micke William na Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo, Agosti 7.

Melo anakabiliwa na mashtaka ya  kuzuia uchunguzi wa Jeshi la Polisi dhidi ya mtandao wake. 

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa. 

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa jana, lakini shahidi wa Jamhuri ni mgonjwa, hivyo aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine.

Hakimu alisema kesi hiyo itasikiliza Agosti 7, mwaka huu, na dhamana ya mshtakiwa inaendelea. 

Upande wa Utetezi ukiongozwa na  Mawakili Peter Kibatala, James Malenga na Ishabakaki Benny hawakuwa na pingamizi. 

Katika kesi ya msingi, Micke na Melo wanadaiwa kuwa  kati ya Mei 10 na Desemba 13, 2016 Mikocheni, jijini Dar es Salaam, wakiwa wakurugenzi wa mtandao wa Jamii  Media Co. Ltd, ambao unaendesha tovuti ya Jamiiforums, wakijua Jeshi la Polisi Tanzania linafanya uchunguzi kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa katika tovuti yao kwa njia ya kuzuia uchunguzi huo walishindwa kutekeleza amri ya kutoa taarifa walizo nazo. 

Washtakiwa waliyakana na wako nje kwa dhamana. 

Share: