Habari

Jecha ni kama sultani/mfalme hahojiwi popote akisema kasema! – Bulembo

Dar es Salaam. Aliyekuwa Meneja wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Abdalah Bulembo amesema haoni dosari katika uamuzi wa kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kumshauri mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Fatma Karume akae pembeni badala ya kuwachanganya wananchi.

Bulembo alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuwa, uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika na kufutwa kwa mujibu wa sheria, hivyo siyo vyema Fatma akatoa kauli za kuchanganya watu.

“Fatma Karume ni nani kusema maneno hayo. Ukizaliwa katika familia ya rais, so who are you? Namshauri (Fatma) akae pembeni kwenye mgogoro wa Zanzibar na aendelee kuwatetea watu mahakamani,” alisema.

Alichosema Fatma
Kauli ya Bulembo imekuja siku kadhaa baada ya Fatma kumshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein kuachia madaraka kwa kuwa kuendelea kubakia ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi.

Alisema mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanziba (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
“Akidi ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na wajumbe wanne. Kama kikao kilifanyika akidi ilitimia na jambo hilo likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi walipokubali wajumbe wengine. Hata makamu mwenyekiti hajashiriki kwenye maamuzi hayo kwa sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila akidi hiyo.

Msimamo wa Bulembo
Kinyume na kauli hiyo ya Fatma, Bulembo alisema kufutwa uchaguzi wa Zanzibar siyo doa kwa sababu ZEC ipo kisheria na sheria inazuia kuhoji uamuzi wake mahali popote.

“Uchaguzi Zanzibar utarudiwa tu kwani kwa mujibu wa sheria zetu, akishasema Mwenyekiti wa Tume amesema, hahojiwi tena popote na ndiyo maana CUF haiwezi kwenda mahakamani. Hili ni suala la kisheria na tukitaka ifanyike vinginevyo, tubadili kwanza sheria,” alisema.

Alisisitiza kuwa watu wenye uelewa kama Fatma wanapaswa kuwaeleza ukweli wasioelewa.

chanzo:mwananchi

Tagsslider
Share: