Habari

Jeshi la Polisi lazusha Taharuki Zanzibar

· Jeshi la Polisi lazusha Taharuki Zanzibar
· Lawapiga maafisa wa ZAECA na kuwafunga, Mmoja wao ni Mjamzito

Jeshi la Polisi Zanzibar limedaiwa kuvamia ofisi za Mamlaka ya Kuzuwia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi, Zanzibar (ZAECA) iliyopo Vuga kuwapiga ikiwemo Mwanamke mmoja Mjamzito.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Mjini hapa zinaeleza kwamba Jeshi la Polisi juzi lilivamia ofisi za Mamlaka hiyo na kuwachukua maafisa wa ZAECA kwa kuwafunga pingu hadi kituo cha Polisi Madema na kuwapiga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alisema aulizwe Kamishna wa Polisi kwa kuwa tukio hilo lipo kwake.

Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mohammed Hassan Haji alithibitisha na kusema kwamba tukio hilo lipo kwenye meza yake na. litasuluhishwa kwa njia ya mazungumzo kati ya maafisa wa jeshi la polisi na maafisa wa ZAECA.

“Ni kweli hili suala na sasa hivi tunalisuluhisha kwa njia ya mazungumzo kati yetu na wenzetu wa ZAECA kwa sababu hizi taasisi zipo kwa mujibu wa sheria na hakuna haja ya kuvutana kwa hivyo tunalizungumza na tutapata suluhisho” alisema Kamishna.

Awali Maafisa wa Mamlaka ya kuzuwia Rushwa na Uhujumu Uchumi wanadaiwa walimuwekea mtego mmoja wa Askari wa Jeshi la Polisi na kumshika na Rushwa jambo ambalo limechochea hasira kwa jeshi hilo kutokana na mwenzao huyo kukamatwa na mtego na kwenda kutoa kichapo kwa maafisa wa ZAECA kwa madai kwamba wamedhalilishwa kukamatwa mwenzao.

“Kwa ufupi wamekuja gari mbili za Defenders hapa na kwa kishindo wakiwa na yale mavazi yao na silaha wakaingia ndani na kuwakamata maafisa wa ZAECA lakini kishindo kilikuwa kikubwa watu wengine wakataharuki na wengine wakakimbia nje wengine ndio wakaingia Ikulu na kule Ikulu watu waliokuwa nje na walinzi walishituka sana” alisema mmoja wa mashuhuda.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya kupambana na Rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar ZAECA Mussa Haji Ali hakuwa tayari kulizungumza suala hilo licha ya kwamba limempa mshituko na khofu.

Watetezi TV

Zanzibar

Share: