Habari

JK ATEUA VIGOGO KUUNDA TUME YA KATIBA

Itaongozwa na Jaji Warioba

Na watu wengi waunga mkono na kupongeza

RAIS Jakaya Kikwete ametangaza majina ya Watu 30 wanaounda Tume ya Katiba itakayoongozwa na mwanasiasa na mwanasheria anaeheshimika nchini Tanzania, Jaji Joseph Warioba.

Kikwete, akitangaza Tume hyo, amemteua Jaji Mkuu mstaafu Augostino Ramadhani, kuwa makamu mwenyekiti. Tume itayofanya kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi wa maeneo yote ya Tanzania na baade kuwasilishwa Bungeni katika kipindi cha miezi 18 ijayo.

Kikwete akitangaza majina hayo jana mbele ya wahariri wa vyombo vya habari Ikulu Dar es Salaam, ambapo alidai katika uteuzi huo kumshirikisha kwa karibu Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein.

Aidha, katika mkutano huo walikuwepo pia Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria Celina Kombani, Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Werema na Msajili wa Vyama vya Siasa John Tendwa.

Mbali na majaji hao wawili, wajumbe wengine kutoka Tanzania Bara ni pamoja na Katibu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Ester Mkwizu, na Mbunge Al-Shaymaa Kwegyir.

Wengine ni mwanasiasa na mwanasheria mashuhiri nchini Dk Sengodo Mvungi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Prof Mwesiga Baregu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof Palamaganda Kabudi na Alhaji Hamad Said El-Maamry.

Walioteuliwa wengine ni Riziki Shahari Mngwali, Richard Shadrack Lymo, John Nkolo, Jesca Sydney Mkuchu, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Maria Malingumu Kashonda na Mwantumu Jasmine Malale.

Wajumbe kutoka Zanzibar ni pamoja na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU) Dk Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Salim Hamad, Awadhi Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salama Maoulidi na Nassor Khamis Mohammed.

Wengine ni Simai Mohamed Saidi, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan (Kibibi ni mtoto wa Ali Hassan Mwinyi) Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdulla Ally Saleh. Katibu wa Sekretarieti ni Assaa Ahmed Rashid msaidizi wake ni Casmir Sumba Kyuki.

Baada ya kutangaza majina hayo Rais hakutaka maswali kutoka kwa waandishi, mpaka pale waandishi hao walipoamua kupiga kambi nje ya Ikulu kusubiri maelezo namna gani tume hiyo itaweza kufanya kazi na kwa muda gani.

Hata hivyo baadae Kikwete, alitoka nje na kuwaambia waandishi, kazi ya kuteuwa majina 30 ilivyokuwa ngumu kutokana na kwamba majina yaliyopendekezwa kutoka kwa kada mbalimbali yalikuwa zaidi ya 550.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete tume hiyo itaanza kazi mara tu baada ya kuapishwa kwa wateuliwa wote na kusisitiza kuwa itafanya kazi ndani ya miezi 18 kama ilivyoainishwa katika sheria ya Katiba mpya.

Kiongozi huyo alienda mbali zaidi na kudai kuwa ana imani ifikapo mwaka 2014 Katiba mpya itakuwa tayari ambapo baada ya kamati kukamilisha mapendekezo yake itayawasilisha katika Bunge Maalum la Katiba kabla ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kutoa yao maoni.

Alipohojiwa kuwa haoni muda huo ni mdogo sana akilinganisha na miaka 17 ambayo nchi ya Kenya ilitumia katika kupata Katiba mpya Kikwete, alijibu kwa ufupi kuwa “ile ni Kenya na hii ni Tanzania”,.

Wakati huohuo watu wa kada mbali mbali wamepongeza uteuzi huo wakisema kuwa wateuliwa wanazo sifa zote hasa Jaji Joseph Warioba, ambaye amewahi kuongoza Tume ya Rushwa, iliyoibua mambo mazito na kutoa mapendekezo kabambe ya kupambana na rushwa nchini..

Share: