Habari

Juma Bhalo aliimba: ‘watakufa nacho kijiba cha moyo’

Al Nofli
Jumatano, Machi 27, 2019

Serikali zote mbili za Tanzania (SMT na SMZ), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CCM na ccmCUF vinaelezwa kuwa vimeandaa mkakati kuhakikisha wanamuondoa Maalim Seif Sharif Hamad katika ulingo wa siasa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani 2020.

Maalim Seif ndiye kiboko yao tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 hadi 2015 CCM Zanzibar kamwe haijawahi kushinda. Wimbi la Tsunami la ACT wiki iliyopita Unguja na Pemba, limewapa Pressure wengine wako ICU.

Kazi ya kuhakikisha kuwa Maalim Seif na wafuasi wake wanapotea katika ulingo wa siasa imekabidhiwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ccmCUF, Chama cha Mapinduzi (CCM), Jeshi la Polisi na Mahakama.

Kinachofanyika sasa katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni juhudi maalum za utekelezaji wa mkakati huo wa kumkwamisha Maalim Seif kuendelea kutamba katika kuzimiliki siasa za Tanzania hasa Zanzibar ambako CCM iko ICU.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mahakama na ccmCUF inayoongozwa na Profesa Lipumba, ambayo imesema wazi wazi kuwa itashirikiana na CCM chama ambacho kwa upande wa Zanzibar, kinaaminika ni chama cha kiadui kwa wananchi wa Zanzibar.

Madai hayo yanaweza kuthibitishwa na barua ya msajili wa vyama vya siasa inayodai mambo matatu kuwa ACT Wazalendo imekiuka sheria ya vyama vya siasa.

(l) Ofisi ya msajili imesema chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2015 kinakabiliwa na adhabu ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014.

(ll) Kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.

(lll) Kutumia dini katika siasa zake baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbiri), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.

Wakati haya yanatokea, Wabunge wa CUF waliokuwa wanamuunga mkono aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wametakiwa kujitafakari, la sivyo hawatavumiliwa.

Onyo hilo lilitolewa siku ya Jumanne, Machi 26, 2019 Dodoma na makamu mwenyekiti wa ccmCUF, Maftah Nachuma wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisema kuwa mgogoro wa chama hicho umekwisha.

Nachuma ambaye ni mbunge wa Mtwara Mjini ccmCUF alisema wabunge wote wanatakiwa kuungana na kuwa kitu kimoja ili kukiimarisha chama hicho baada ya misukosuko mingi.

“Chama hakiwezi kumvumilia mtu ambaye atakuwa mbunge kupitia chama chetu lakini akaonekana anatumia vibaya rasilimali yetu kwa kuunga ama kushabikia chama kingine, bora ajitoe mapema kabla ya kushughulikiwa,” alisema Nachuma.

Nachuma alijikita kusifu utendaji kazi wa mwenyekiti wa ccmCUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema waliohama chama hicho wanatakiwa kuwa wastaarabu na kuacha kuharibu mali za chama chao.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kueleza kuhusu suala la wabunge wa chama hicho ambao walichaguliwa katika uchaguzi mkuu uliyopita kwamba upande gani waelekee, uamuzi wa jukumu hilo uliachwa mikononi mwao.

Lakini, idadi kubwa ya wabunge wa CUF ambao tangu mgogoro wa chama hicho ulipoanza mwaka 2016 baadhi yao wamekuwa wakiunga mkono upande wa Maalim Seif. Kuna msemo: ‘chuma juani ule kivulini’ maana yake ni kwamba mbunge akiona bora aendelee na ccmCUF Lipumba, ajue tangu sasa uchaguzi mkuu ujao, asitarajie kitu.

Barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyotoka na kusambazwa Jumatatu Machi 25, 2019 kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari imeibua mjadali mpana.

Wapo wanaoshangazwa na vitisho vya msajili dhidi ya chama kinachoibuka kwa kasi Tanzania bara na Zanzibar, hasa Zanzibar cha ACT-Wazalendo, wanaojadili mshangao huo wanaamini msajili anashindwa kuzuia mihemko yake.

Hatua ya msajili sasa kuivaa ACT-Wazalendo imetanguliwa na malalamiko kutoka ccmCUF kwamba, bendera zao zinachomwa, ccmCUF walikwenda mbali zaidi kwa kuomba Ofisi ya Msajili ifute usajili wa Chama cha ACT-Wazalendo.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimesikiliza mlio wa zumari kutoka ccmCUF, Dk Bashiru Ally, Katibu Mkuu wa CCM alipokuwa katika Uzinduzi wa Mkakati Maalum wa CCM wa kukomaza demokrasia nchini uliofanyika Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita, alishadididia malalamiko ya ccmCUF kuhusu kuchomwa kwa bendera zao.

Sasa imekuwa zamu ya Ofisi ya Msajili kutoa tuhuma kuhusu kuchomwa bendera za CUF. Taasisi hizo tatu (ccmCUF, CCM na Ofisi ya Msajili) zimetoa tuhuma zinazofanana.

Hii ni sehemu ya barua yake msajili Jaji Francis Mutungi: “Aidha, baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kesi No. 23 ya mwaka 2016 iliyokuwa inahoji uhalali wa Profesa Ibraimu Lipumba, Machi 18 mwaka huu, kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa sheria.

“Ikiwamo kuchoma moto bendera za ccmCUF, uliofanywa na mashabiki wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wanadai sasa ni wanachama wa ACT. Kitendo cha kuchoma bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C, cha sheria ya vyama vya siasa.”

Kwenye barua hiyo msajili amekumbushia onyo lake la Machi 18 mwaka huu akikemea kitendo cha wananchama wa ACT-Wazalendo kutochukua hatua ya kukemea suala hilo, akisema chama hicho kimeafiki au kilitoa maelekezo kufanyika kwa vitendo hivyo.

“Kutokana na maelezo hayo, vitendo hivyo vinaakisi ukiukwaji wa dhahiri wa sheria ya vyama vya siasa ambao pia unasababisha chama chenu kupoteza sifa za usajili wa kudumu.

“Hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa anatumia fursa hii kukufahamisha wewe na wanachama wa ACT-Wazalendo nia yake ya kufuta usajili wa kudumu wa chama chenu kwa sababu hizo zilizotajwa,” imeeleza barua ya msajili.

Swali linaloibuka hapa ni kwamba, waliochoma bendera za ccmCUF walikuwa wanachama wa ccmCUF ama ACT-Wazalendo?. Hapa Jaji Mutungi, anatakiwa asaidiwe.

Amesema, waliokuwa wanamuunga mkono Maalim Seif ndiyo waliochoma bendera hizo; sawa lakini je wakati wanafanya hivyo walikuwa wanachama wa chama gani?…hilo ndiyo swali.

Muda mfupi baada ya Maalim Seif kuhama, waliochoma bendera hizo walikuwa bado ni wanachama wa CUF. Msajili, Jaji Mutungi lazima ajuwe hivyo.

Hawa wanaweza kufanya hivyo kutokana na CUF kushindwa kutatua mgogoro wake na hata Maalim Seif akaamua kuondoka, njia ya kuonesha hasira zao kwa chama chao (CUF) ikawa kuchoma bendera.

Ama walifanya hivyo kwa kuonesha kuchoshwa na chama chao wenyewe kutokana na sababu wanazoweza kujua wenyewe, lakini jambo la kuzingatia hapa ni kuwa, wakati wanafanya hivyo walikuwa ni wafuasi ama wanachama wa CUF.

Kama hivyo ndivyo, ACT-Wazalendo inawajibikaje kwa wafuasi wa CUF kuchoma bendera zao wenyewe?. ACT-Wazalendo wanayo mamlaka gani ya kuingilia hisia za wanachama wa CUF kwa kile wanachokitenda kuonesha hisia zao?.

Msajili anawezaje kuituhumu na hata kufuta Chama cha ACT-Wazalendo kwa vitendo vilivyofanywa na wafuasi wa CUF?. Hapa busara inahitajika.

Jaji Mutungu anapaswa kusimama katika haki. Njia rahisi ya kuonesha anasimamia haki ni kufafanua moja ya hoja zake kwamba, waliochoma bendera za CUF ni wanachama ACT-Wazalendo.

Jaji Mutungi anapaswa kujua kwa dhati kabisa taasisi yake anaweza kuitumia vizuri, nchi ikabaki salama ama anaweza kuiendesha kwa namna ambavyo nchi ikatumbukia kwenye matatizo. Busara yake ndiyo mafanikio ya taifa letu katika utulivu wa kisiasa.

Hapa narudia na kuitolea tafsiri tuhuma moja kati ya tatu zilizomo katika barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Barua hiyo imeyataja mambo yanayodaiwa kukiukwa na chama hicho kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kuchoma moto bendera za ccmCUF.

Vilevile, chama hicho kimetuhumiwa kutumia dini katika siasa zake baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu la Takbiri.

Chanzo cha neno Takbbiri linatokana na neno KABB’RA tafsiri yake KUTUKUZA, neno hili ndilo lililozaa Takbiri na maana yake UTUKUZWAJI inakusudiwa ‘mtukuzeni Allah. Hapa kwa mtu mwenye kujuwa ukubwa wa Mwenyezi Mungu yaani utukufu wa Allah, anakosea nini anaposema Takbirii?.

Tuhuma zilizomo

Barua hiyo imeyataja mambo yanayodaiwa kukiukwa na chama hicho kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.

Barua ilieleza kuwa vitendo hivyo vinafanywa na “mashabiki wa Maalim Seif, ambao wanadai sasa ni wanachama wa ACT-Wazalendo.”

“Kitendo cha kuchoma bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C cha sheria ya vyama vya siasa,” ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo hadi sasa nakala yake, inazagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Vilevile, chama hicho kimetuhumiwa kutumia dini katika siasa zake baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbiri), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.

Sisty Nyahoza alisema licha ya msajili kukemea vitendo hivyo Machi 19 na kusema kuwa anayafanyia kazi matendo hayo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na chama hicho ikiwa ni pamoja na kutokemea tabia hiyo.

“Kutokana na hilo, inaonekana chama chenu kiliafiki au kuelekeza vitendo hivyo kufanyika,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Mbali na hatua hizo, ofisi ya msajili imesema chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2015 kinakabiliwa na adhabu nyingine ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014.

Barua hiyo imenukuu barua ya Mei 22, 2018 kwenda chama hicho iliyokuwa inasitisha ruzuku sambamba na kuhitaji hesabu za miaka mitatu ya 2013/14, 2015/16 na 2017/17 lakini kilipojibu kilitoa hesabu za miaka miwili bila kuweza za 2013/2014.

Alisema kutowasilisha hesabu za mwaka wa fedha wa 2013/14 kinakuwa bado hakijakidhi matakwa ya barua ya msajili wa vyama vya siasa, hivyo kinakuwa kimekiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258.

Pamoja na barua hiyo, Ofisi ya Msajili Zanzibar nayo imetoa tamko ikiwatahadharisha wafuasi wa ACT-Wazalendo ambao wametokea CUF kuacha kufanya vitendo ilivyoviita vya uvunjifu wa amani la sivyo wataishia jela. Kauli hii inafanana na ile iliyowahi kutolewa na Rais John Magufuli, ‘wapinzani kuishia magerezani.’

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa upande wa Zanzibar, Mohamed Ali Ameir alisema hayo Jumatatu, Machi 25, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa ccmCUF, Mussa Haji Kombo alisaini hati ya kiapo cha mashtaka dhidi ya ACT-Wazalendo katika Mahakama Kuu Zanzibar, akidai wanachama wa chama wa ACT wameharibu mali za CUF na kuhatarisha amani.

Suala la kukamatwa kwa baadhi ya waliyokuwa viongozi wa CUF, Maalim Seif alilizungumzia katika moja ya hotuba zake, siku chache zilizopita baada ya kuhajjir na kujiunga na ACT-Wazalendo. Hilo linafahamika na sijambo jipya.

Tumeshuhudia, Mussa Haji alivyopelekwa kwa Defender za Polisi Mtendeni kwenye nyumba iliyokuwa makao makuu ya CUF ambayo sasa ni ccmCUF inaendeshwa na Dola ya Dk John Pombe Magufuli.

Wiki chache zijazo tutawaona CCM wakiingia na kutoka kama vile wanavyoingia Kisiwandui na Lumumba!. Magufu alitoa ahadi kuwa atahakikisha hadi 2020 Tanzania hakutakuwa na chama cha upinzani. Nimekumbuka ile nyimbo ya zamani kwenye miaka 70s ‘mambo bado.’

Narudi kwa ACT-Wazalendo

Wakati huohuo, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amemteua Juma Duni Haji maarufu Babu Duni kuwa naibu kiongozi wa chama hicho.

Akizungumza Dar es Salaam Jumanne, Machi 26, 2019 Zitto alisema kuwa kwenye kikao cha uongozi wa chama, wameridhia Babu Duni kuwa naibu kiongozi wa ACT.

“Nimepewa mamlaka na katiba ya chama kumteua, nikawasilisha kwa uongozi na wameridhia na ataanza kesho (Jumatano Machi 27) kutumikia nafasi hiyo,” alisema Zitto.

Babu Duni anashika wadhifa huo ni wiki moja imepita tangu alipokabidhiwa kadi namba kumi ya uanachama akiwa pamoja na viongozi wengine kutoka CUF akiwamo Maalim Seif aliyepewa kadi ya uanachama namba moja.

ACT-Wazalendo ni chama kubwa wiki moja tu limefunika hadi chama kizee CCM. Maalim Seif ni bahari nyingine kwa viongozi wote wa Tanzania. Baba lao Nyerere aliwahi kukiri mwenyewe kuwa: “najuta kumfukuza CCM Seif.”

Share: