Habari

Juma Duni: Haikuwa rahisi kwangu kuhamia Chadema

By Muhammed Khamis – Mwananchi
Jumatano, Novemba 21, 2018

Miaka mitatu baada ya Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania aliyekuwa mgombea mwenza kupitia Chadema na Ukawa, Juma Duni Haji amevunja ukimya na kuweka hadharani ilivyokuwa vigumu kwake kuhamia katika chama hicho.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Zanzibar, Duni anasema mchakato wa yeye kuhama kutoka CUF alikokuwa Makamu Mwenyekiti na kuingia Chadema kulimweka njia panda baada ya kutakiwa kufanya hivyo na viongozi wakuu wa CUF.

Duni anasema yeye hakuwa anafahamu lolote kuhusu kutakiwa kwake kujiunga na Chadema ili awe mgombea mwenza wa Edward Lowassa aliyekuwa pia amehamia huko kutoka CCM.

Anasema aliitwa nyumbani kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba (wakati huo kabla hajajiuzulu nafasi hiyo), Dar es Salama akiwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na kuelezwa dhamira ya yeye kutakiwa kuhamia Chadema.

Anasema kabla ya hatua hiyo, hakuwa amewahi kukaa kikao chochote kumtaka ushauri. Siku chache badaye alikutana tena na Maalim Seif katika ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Migombani Zanzibar, na kusisitiza mpango huo.

“Wote wawili kwa nyakati tofauti walikuwa na ajenda mimi nijiunge na Chadema kwa vile wamekubaliana kwenye vikao vya Ukawa. Iliniuma lakini sikuwa na jinsi kwa vile mimi ni askari wa chama, nipo tayari kufanya kazi popote pale,” anasema Duni.

Anasema watu wengi hawafahamu ukweli na wapo wanaoendelea kudai hadi leo kwamba alipewa fedha ili ajiunge Chadema jambo ambalo halina ukweli.

Anasema kwa kujiunga kwake Chadema alipoteza haki zake za msingi ikiwamo kukatwa mishahara miezi mitatu akiwa Waziri wa Miundombinu na Mawasialino pamoja pensheni yake ya kustaafu uwaziri kutoka miezi 60 hadi 57.

Hata hivyo, Duni aliyewahi pia kuwa Waziri wa Afya wa SMZ, anasema licha ya kuwa na ugumu kujiunga na Chadema, ilikuwa rahisi sana kurudi kwenye chama chake cha CUF baada ya uchaguzi kumalizika.

Anasema ndiyo maana alipokewa kwa shangwe kubwa kwa vile kuingia kwake Chadema ilikuwa ni ajenda maalumu ya kupambana na adui.

Duni ameweka bayana kuwa ikitokea tena fursa kama ile na kushauriwa agombee tena kupitia Ukawa, hatakuwa tayari kwa sababu anaamini ni muda wa vyama kuwatengeneza watu wengine kwa ajili ya nafasi hizo.

Anaionaje hali ya vyama vya upinzani nchini. Duni anasema bado kuna safari ndefu na bila baadhi ya viongozi wa vyama hivyo kuacha ubinafsi hadhani kama wataweza kutimiza malengo yao.

Anasema alichokiona kwa haraka ni kwamba viongozi wengi wa upinzani bila ya kutaja vyama vyao, wana ubinafsi jambo ambalo anadai linaweza kuwakwamisha kwa kiasi kikubwa katika kushika hatamu za dola.

Anasema siku zote nia njema kwenye nafsi za watu ndiyo suluhisho la kufikia malengo, bila hivyo wapinzani wataendelea kufanya siasa kwa muda mrefu bila kufikia dhamira zao.

Duni akizungumzia kuhusu mwenendo wa CUF hivi sasa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 anasema, anaamini bado chama chao kina nguvu kwenye mapambano ya kisiasa visiwani Zanzibar na wanachama wao hawatetereki kama baadhi ya watu wanavyodhani.

Kuhusu tuhuma za baadhi ya wabunge kushindwa kutekeleza wajibu wao ndani ya chama, Duni alikiri kuwapo changamoto hiyo akisema ni utashi binafsi na si maagizo ya chama.

Kuhusu hamahama ya viongozi wa upinzani kwenda CCM, alisema pia inatokana na tamaa ya kwenye siasa inayotokana na wanaoingia kwenye siasa bila malengo maalumu, bali kujipatia kipato.

“Kwa mfano mtu kama Mtatiro (Julius) amewahi kuwa mpaka Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi kwenye chama chetu eti leo anatoka anaunga mkono juhudi za Rais. Inashangaza sana na lazima hili lisemewe,” anasema Duni.

Anasema: “Inashangaza kwa sababu hakuna chochote kilichobadilika kwenye serikali au utawala ulipo, lakini mtu kama Mtatiro anaamua kutoka upinzani na kujiunga nao akisahau kabisa malengo na dhamira ya chama chake.”

Anasema kuna haja ya wanachama na viongozi wa siasa kujifunza kwa kiongozi wao wa muda mrefu, Machano Khamis Ali ambaye kwa muda wake wote hakuwahi kuwa mbunge wala mwakilishi lakini alikitumika chama hicho hadi kustaafu kwake.

Anasema kuwa iwapo Mzee Machano angekuwa na ubinafsi na kulazimisha kuwa kiongozi, anaamini angekuwa na nafasi kubwa ya uongozi wakati wa Serikali ya SUK na hata kabla.

Duni anasema chama chao bado kitaendelea kuwa na imani na Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu ndiyo wenye mamlaka ya kusema nani agombee na nani asigombee.

Anasem zipo chuki binafsi zinazoelekezwa kwa kiongozi wao kutaka asigombee ili iwe rahisi kwao kushinda kwa vile Maalim Seif kwenye siasa za Tanzania ana mvuto kwa wananchi, wana CUF na nje ya chama.

Share: