Habari

KALAMU KILMA NA DARUBINI YA KONDO.

Kwanza kabisa namshukuru Molla kwa kunipa afya na fursa ya kurudi tena hapa gazetini kwetu,pia nachukua fursa hii kurudisha salaam za kheri kwa waungwana wenzangu walionikumbuka Zamko na Mmtamwe nawashukuru sana.

Kweli nimeadimika kidogo hii imetokana na sababu nyingi za kutafuta riziki, na kufanya chunguzi zangu za kina kabla sijarudi kuleta salaam au maoni yangu.

Leo nina machache ya kuwasilisha kwenu,huenda nikachanganya mada na huenda nisichanganye sijui, lakini muhimu nataka kutoa warka wa utafiti wangu wa hali halisi ilivyo na inavyoelekea kisiasa hapa kwetu.

Nianze na tafakuri ya CCM kukiiba chama cha wananchi yaani “cuf” kwa kuitumia mahakama,wengi mtakumbuka kuwa niliweka wazi kwa Maalim kuwa asitegemee mahakama kupata haki,na ni lazima awekeze kwenye “plan b” na nilishauri kuwa wakati muafaka ukifika ni lazima achukue uamuzi mgumu  na nilimulekeza na wapi kwa kuelekea,nilivitaja vyama vya NCCR -MAGEUZI na ACT -WAZALENDO kwa majina na kukiacha chama cha ‘CHADEMA’ kwa makusudi,nilifarijika baada ya kuona washauri wa Maalim pamoja na yeye mwenyewe wamefikia uamuzi huo,sababu zangu haziku husiana na SERA za vyama vya kukimbilia bali niliegemea zaidi kwenye sababu za kimikakati zaidi {strategy}

Nilizungumza sana huko nyuma katika moja ya makala zangu kuwa kama Watanganyika hawatokomaa kisiasa kama Wazanzibari,wananchi wake ni lazima wapate na kupitia dhiki,maafa,mauwaji na mateso yote waliyopata na wanayoendelea kuyapata Wazanzibari,kuvikomboa visiwa vyetu hivi itatuchukua karne nyingine au itakuwa ndoto tu.

Ni lazima “level” ya upinzani wafikie tulipo fikia sisi ndio sote tutaweza kujikomboa kwa kujivua huu Muungano jina,na kweli hivi sasa madhila na wao yamewakuta na wanaendelea kuyaonja utamu wake, hivi sasa na wao wanauwawa,wanatekana,wanafungana ovyo,wanabaguana kwa makabila na dini,uhuru wa kusema/maoni wamepokonywa,baada ya kuwekewa sheria ya kuzuwia uchochezi, nia na madhumuni ya sheria hii ni kukandamiza na kufunga midomo hamna ziada.

Huko nyuma niliwahi kusema kuwa Tangayika kuitawala Zanzibar wanaona raha au uroda lakini niliwaonya kuwa visiwa hivi havitotawalika kwa bei nafuu,hivi visiwa vinawagharimu na bei ya kuvitawala itawatokea puani, lakini la kuvunda halina ubani, hawa waungwana hawatosikia, sasa safari ya kuibomoa Tanganyika iko jikoni inachemka taratibu, wazungu husema ‘thanks to Seif Sharrif’ au shukrani kwa Malim.

Nilitoa tahadhari kwa chama changu cha Mapinduzi kuwa sisi tumejikita katika kufanya ubaya muda wote wa kukihujumu chama cha cuf na hususan Maalim, kwa kuwa ugomvi wetu na kiumbe huyu hauna kikomo ni wa mpaka kiama,,lakini nilisema na nina kumbusha kuwa kitakachotokea baada ya hapo hatukijuwi na tutakuja kujuta,kwa sababu Molla humjalia mtu au kikundi cha watu wakikusudia kufanya ubaya au hujuma,huwa anazielekeza akili zake/zao katika maasi peke yake waliyokusudia, huwa hawapi fursa ya kutafakari matokeo yake baada ya kufanikisha azma yao”the aftermath” sasa nani atafaidika na awamu hiyo, hiyo huwa siri yake.

CUF katika visiwa vya Zanzibar ni sawa sawa na ASP kwa sasa yaani ni Marehemu wote wawili,Maalim na wafuasi au wanachama wake hawapo, wamesha shusha Tanga na wamepandisha Tanga kwa sasa wanatumia anuani mpya kwa barua zao zote ni lazima zipitie kwa Zitto Kabwe ndio utawakuta huko.

Proffesa/propesa Lipumba anapenda pesa lakini sio kama hana akili,huyu kiumbe alijua mapema chama cha cuf bila Maalim ni sawa sasa na kuwa na chama cha wavuvi jangwani,sidhani kama utapata wanachama wengi,au sawa na kuwa na Tanzania bila Nyerere,sio CCM kwa sababu mwenyewe aliwahi kusema ccm yeye sio mama yake wala baba yake,lakini Tanzania bora afe yeye lakini Tanzania ibakie na hilo limetendeka.

Lipumba alirudishwa cuf na Magufuli ili aje kukimaliza sio kukiimarisha kama anavyodai katika mikutano yake,na kazi hiyo ameifanya na imekwisha,  pesa ameshalipwa kwa kupitia ruzuku ambazo Lipumba alizigawa kama njugu, kwa kina Khalifa, Kambaya na Sakaya pamoja na washirika wote wa mradi huu,chama hiki cha ccmcuf kwa sasa kikitaka msaada wa wanachama wa kuhudhuria mikutano yao,tutawaazima wanachama wetu wa CCM mpaka pale tutakapoona hatuna haja nao tena kwa lolote.

Kuuwawa kwa CUF Zanzibar lengo kuu ilikuwa ni kuumaliza mgogoro wa SMZ NA ST dhidi ya wafadhili na mashirika ya nje waliotaka kujua hatma ya uchaguzi wa Jecha wa 2015 na dhulma zake,ulipandikizwa mgogoro huu kuzinusuru hizi serekali mbili za Tanzania,sasa haitowezekana kumrudishia URAIS Maalim wakati mshindi wa uchaguzi huo ameshafukuzwa chama,SMZ hawana tena wa kumkabidhi nchi, hawakuwa na nia wala dhumuni hilo, lakini sasa wamepata na sababu.

Maalim Seif ana ushawishi na nguvu kubwa katika Taifa hili la Tanzania kisiasa sio Zanzibar peke yake,Tanganyika sio muda mrefu watalielewa hili, baada ya kuona umati utakaokusanyika mara tu mikutano ya kisiasa ikiwa huru,Kiongozi huyu akiamua kesho umati wake washushe bendera ya ACT- WAZALENDO na wapandishe bendera ya CCM, umati wake utamfuata kwanza, masuali watamuuliza baadae,sasa kwa nini sisi ccm tunashindwa kuutumia mtaji huu wa kisiasa vizuri, alionao Muungwana huyu kwa busara, badala yake tunatumia fedha nyingi kununua watu,kuhujumu na kuuwa uchumi wa nchi,tunamwaga damu nyingi ya wananchi wetu wasio na hatia, tunavitumia vyombo vya ulinzi vya dola vyenye jukumu la kuwalinda raia, badala yake vyombo hivi tumevigeuza mali ya CCM ya kuwakandamiza wapiga kura,tutatawala au kuongoza kwa muda gani kwa vigezo hivi? huu ndio utawala bora wa Kiafrika?

Hivi sasa tayari tumeandikisha ADUI mpya sio cuf tena, sasa adui ni ACT-WAZALENDO sijui adui huyu tutadumu nae kwa muda gani?huyu nae tumpachike jina la HIZBU  kama wale ‘macuf’ au huyu tumtafutie la kwake? maswali yako mengi kwa huyu adui mpya,inaonyesha hatukosoma kitu kwenye miaka yote hii tuliyopoteza katika kumhujumu Seif Sherrif, kwa maoni yangu kila tukimfuata fuata ndio tunajipalilia makaa au kujishonea sanda “solution” sio nguvu ni akili wakereketwa.

Zanzibar kazi ya kuimarisha upinzani Maalim hana tena, amemaliza na amefuzu huu ndio ukweli hautaki ubushi,kama huamini itisha uchaguzi huru na wa haki uone cha mtema kuni, chaguzi tano zote kashinda kila siku zikienda mbele ndio idadi ya kura zake zinaongezeka hazipungui,sababu moja kubwa Zanzibar kama mataifa mengine duniani, wapiga kura wamebadilika wengi ni vijana chini ya miaka 25, na hawa huwezi kuwadanganya tena kama mlivyotu ongopea sisi miaka ya nyuma,dunia imebadilika “this is digital generation” wanapokea na kupeana habari za ulimwengu mzima kwa sekunde chini ya tano.

Msajili sijui tutamtumia na atavifuta vyama vingapi vya upinzani ikiwa ataanza na ACT -WAZALENDO, ni vema tukajua kuwa hii safari au njia tunayoichukua ndio inayo imarisha upinzani kwa kuwaunganisha vyama vyao,hata tukikifuta leo kesho, Maalim atajiunga na nccr-mageuzi cha Mbatia na hicho tutamtafutia sababu tukifute, hatimae atavimaliza vyote, mwisho atajiunga na CHADEMA,nimekiweka mwisho makusudi kwa sababu hilo ndio lengo kama mnajua kuchambua siasa,tukifika hapo Tanzania au Tanganyika HAKUNA TENA CCM, jee hili ndio lengo letu? kumbuka polisi hawajawahi kukilinda chama chochote cha siasa duniani maisha, upepo ukizidi wao na majeshi  ya ulinzi huegemea kwa watu sio chama.

Maalim ni muungwana sana na ni lazima tukae nae kitako kama alivyo fanya Amani Karume tusione haya,huyu mtu ana nia njema na Taifa hili sio Zanzibar peke yake,hana kinyongo amepitia misuko suko mingi na amesamehe na bado ana pata fursa na anacheka na wale wale waliomhukumu na kumhujumu.

Ninacho kihofia sana baada ya kumsikia Kangi Lugola  hivi karibuni alipokuja kututisha kidogo hapa Zanzibar, Waziri wa Tanganyika wa mambo ya ndani/sisi hatuhusu tuna serekali yetu japo kuwa ya Sultani huyo huyo mmoja,kahama Oman siku hizi anaishi Dodoma,CCM tusije tukafanya mchezo tukamkamata Maalim na kumuweka rumande au kumtafutia kesi na kumuweka jela,huyu muungwana sie yule kijana aliyewekwa jela na Salamin Amour wakti umepita na hivi sasa ni mtu mzima umri umekwenda,akija akitufia mikononi mwetu wakati tunae jela au mahabusu siku hiyo ndio mwisho wa kucheza na shilingi chooni.

Huyu sio sawa na wale masheikh wa UAMSHO msione kwa kuwa wale bado tunao ndani mwaka wa sita sasa na hakuna chochote kilichotokea tukadhani tujaribu na hapa,hapa sipo na yeye anajua, ndio maana siku zote mnamsikia anapita akiwaambia vijana wake ‘MSICHOKOZEKE” kwa mwenye kufahamu hii ni lugha rahisi kuielewa,kwa nini anawatayarisha na kuwakumbusha siku zote kuwa msifanye fujo, hata baada ya kufanyiwa fujo?hiki ni kitendawili kina subiri siku kiteguliwe.

Tanzania karibu itatungwa sheria kuwa akisikika mtu anasema ‘MUNGU MKUBWA AU KARIMU KWA KIARABU’ basi huyo ashughulikiwe,kinacho ogopwa hapa ni lugha ya kiarabu sio maneno YENYEWE,Waarabu ndio maadui zetu siku zote mmesahau?maneno hayo hayo ukiyasema au ukipita ukipiya pigia ukelele kwa Kiswahili watu watakushangaa, na kukuona ama mwenda wazimu au umerogwa,wengine wataburudika kwa kukucheka huku wakiendelea na yao,lakini badili lugha yaweke kiarabu sasa utamsikia Magufuli.Kangi Lugola na Jaji Mutungi wote watu wa Yesu ,uone kesi zako za ugaidi zitakavyopishana KISUTU.

Huu ni msiba mkubwa ndugu zanguni,hivi karibuni baada ya kutokea ule msiba wa waislamu waliouwawa msikitini New Zealand wakati wakisali sala ya Ijumaa,mkuu wa polisi wa eneo lile ambae ni mwanamke mzungu na ni muislamu, alifuatana na viongozi wenziwe wa polisi wakaenda msikitini wiki iliyofuata kutoa POLE pamoja na wakaazi wengi sana wa eneo lile la Christchurch.

Alitoa hotuba yake kwa lugha yake ya kiingereza, kabla hajaianza risala yake alisoma sura mbili tatu za Quran takatifu kwa kiarabu kisha akaendelea,sasa sikusita kujiuliza huyu angalikuwa hapa kwetu basi angelitafutiwa sababu afukuzwe kazi, kwa sababu amechanganya dini na kazi za KIPOLISI wakati akiwa kazini, na amevaa sare za kiaskari,ndugu zangu sisi tunapigwa vita vya kidini bure.

Ugaidi ni kisingizio tu,sasa gaidi nani hapo alieuliwa huku akisjudu msikitini au yule alie kwenda kuwauwa?na hata hao waislamu wanao uwa watu ovyo, wao na wakristo au mabaniani wanao uwa hayo ni yao wao sio ya DINI ZAO,kwa  nini wakifanya wao mnatenganisha, lakini wakifanya wengine na dini zao mnaziburuza mahakamani.

Mimi naamini ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar uko usoni, kwa sababu Molla ndie anae panga siku zote sio sisi, pia kheri mara nyingine hupitia tumbo la shari,ndio maana viongozi kama Lowassa,Membe,Kikwete, Mkapa,Mwinyi hawa wanauma huku wanatupuliza, na siku zina sogea mbele na sisi bado tunatawaliwa,lakini huyu Muungwana anaeitwa Pombe safari hii nchi inaongozwa na mlevi na hakuna msalie mtume.

Hawa ndio viongozi MOlla huwatumia kuwaokoa viumbe vyake,mifano tunayo tele kama Firauni,Hitler,Iddi Amin,Pinochet wa Chile, na wengine wengi wa aina hii, hawa hawakuwa viongozi wenye huruma wala lugha nzuri,matusi na ujeuri ndio SUBAL KHEIR kwao, sasa msiogope,msishituke wala msikate Tamaa, huu ndio mwisho wa Utawala unavyoanza wa viongozi makatili.

MAKOSA YA UCHAPAJI NAOMBA TAHFIF.

MUNGU MKUBWA/ KIARABU MTASEMA NYIE.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Share: