Habari

Kamati ya Bunge na Fatma Karume waililia misaada ya MCC

Mwanasheria wa kujitegemea, Fatma Karume

By Waandishi wa Mwananchi
Sunday, April 3, 2016

Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeiomba Serikali ya Marekani kupitia Bodi yake ya Changamoto za Milenia (MCC) kuziachia fedha ilizozuia ili zisaidie maendeleo.

Kilio hicho pia kimetolewa na mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume ambaye amesema uamuzi wa MCC kuinyima Tanzania msaada wa zaidi ya Sh1 trilioni, utawaathiri zaidi wananchi wa vijijini ambao ndiyo wanufaika wakubwa wa misaada hiyo.

Hivi karibuni MCC ilizuia misaada yake kwa Tanzania kwa madai kwamba haijatimiza viwango vinavyohitajika. Msaada uliozuiwa ulikuwa wa awamu ya pili.

Fedha hizo hutumika katika kufadhili miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo ya Watanzania ikiwamo ujenzi wa barabara, miundombinu ya maji, usambazaji wa nishati ya umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati ya Vijijini (Rea).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Mary Nagu alisema juzi mjini Bagamoyo kuwa Marekani haikupaswa kusitisha miradi inayoileta nchini kupitia MCC kwani imekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania.

Dk Nagu alisema hayo wakati kamati yake ilipofanya ziara katika mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji Ruvu Chini na ujenzi wa bomba la maji kutoka kwenye chanzo hicho hadi katika matanki ya Chuo cha Ardhi, Dar es Salaam.

“Mradi wa MCC umetusaidia katika upanuzi wa chanzo hiki cha maji cha Ruvuchini kwa hiyo Marekani ione inapofanya mambo mazuri kama haya inatufurahisha sisi kwa hiyo na MCC ya awamu ya pili tunayoingojea wasiizuie, wailete.”

Fatma Karume aonya
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Fatma alisema ni rahisi kwa watawala kupuuza msaada huo kwa sababu hawaoni madhara yake moja kwa moja kwa kuwa wengi wao wanaishi mijini kwenye miundombinu na huduma zote muhimu za kijamii.

Alisema Watanzania walio wengi waishio vijijini wamekuwa na changamoto kubwa ya kuishi gizani na kwamba msaada huo wa MCC ungeweza kuwasaidia kuondokana na matatizo mengi.

Alisema MCC ilikuwa tayari kuendelea kutoa misaada yake Tanzania kwa ombi, watawala kuheshimu wananchi, haki za binadamu na demokrasia, watu kutoa maoni yao bila kubughudhiwa.

Imeandikwa na Allan Goshashy, Joyce Mmasi

Share: