Habari

Karume awatoa khofu wana CCM

Salma Said,

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dk Amani Abeid Karume amewafananisha Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar (JUMIKI) kuwa sawa na waamsha daku wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuwataka Wana CCM kubakia na misimamo yao katika suala la Muungano.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika Jimbo la Rahaleo Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Dk Karume alisema kwamba CCM haijalala hivyo wanachama wa CCM hawana sababu ya kuwa na hofu na Uamsho kwani wao hawakulala.

“Kwani nyie mmelala mpaka muamshwe,nyie mko macho eti…hao ni kama wale wanaoamsha daku utakasirika,lakini ukiamka unasema ahaa kumbe muda wa kula daku tena hofu ya nini” Alisema Dk Karume.

Makamu huyo Mwenyekiti alilazimika kutoa maelezo hayo baada ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini Unguja,Borafia Silima Juma kueleza wasiwasi wa wanachama wa CCM kuhusu vurugu zilizotokea mwezi Mei mwaka huu na harakati kundi la Uamsho.

Dk Karume akijibu hilo,alisema juhudi za kuiweka Zanzibar katika hali ya maelewano ilifanywa na Jumuiya za Kimataifa na Mataifa kutoka nje,lakini hawakuweza kusuluhisha migororo ya kisiasa iliyodumu kwa takriban miongo mitatu,lakini baada ya Wazanzibari wenyewe kuamua kuacha tofauti zao maridhiano yalifikiwa mwaka 2009.

Alisema wakati wa utawala wake walihakikisha kabla ya kumaliza kipindi cha utawala wake anaiwacha Zanzibar ikiwa salama,yenye umoja na mshikamano na isiyokuwa ya vipande vipande ambapo hali hiyo ilifanikishwa baada ya kufikiwa kwa maridhiano ya kisiasa baina ya Chama ch Wananchi(CUF) na Chama cha Mapinduzi.

“Mimi na Katibu Mkuu wa CUF,maalim Seif Shariff Hamad tulikutana Ikulu na kukazungumza kwanini kumaliza tofauti zetu maana sisi sote ni wamoja na leo mafanikio yake ndio haya ya Zanzibar imetulia” Alisema Dk. Karume.

Akizungumzia suala la maoni kuhusu Muungano,Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM alisema watu wote wanaotoa maoni kimsingi wanatumia haki ya kikatiba na kidemokrasia hivyo wanaCCM wanachotakiwa ni kuendelea kusimamia azma yaujenzi wa chama chao huku wakiendelea kuheshimu misimamo yao bila ya kuyumbishwa.

Dk Karume alisema hoja ya Muungano wako baadhi ya watu amewasikia wakitaka Muungano uendelee,wengine wakishauri ufanyiwe marekebisho na mabadiliko huku wengine wakitaka uvunjike.
“Msipatwe na homa, ondoeni hofu na wasiwasi , waacheni masheikh wajibishane na masheikh wenzao na sisi wanasiasa tutafute majibu mjarab yatakayofaa ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha vijana wetu kutambua mahali tulikotoka, tulipo sasa na kule tuendako”Alisema.

Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar alitamka bayana kuwa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi njia pekee ni kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura ili kushinda katika kila uchaguzi na si kinyume chake.

Mkutano huo uliofanyika katika Tawi la Gulioni ambako alizungumza na wanachama wa matawi mawili la Gulioni na Mwembeladu ni wanachama wachache waliohudhuria tofauti na matarajio ya watu wengi

Tagsslider
Share: