Habari

Karume: Kuheshimu haki zawengine chanzo cha amani

Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume

By Noor Shija – Mwananchi
Wednesday, March 14, 2018

“Kuheshimu haki za wengine ni amani.” Ndivyo anavyosema Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume wakati akihutubia mkutano wa amani katika mji wa Belfast nchini Ireland hivi karibuni.

Karume ni rais wa sita wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ni mtoto wa rais wa kwanza visiwani humo, Abeid Amani Karume.

Karume ambaye ana historia ya kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kufanya mabadiliko ya kikatiba na kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), alizungumzia umuhimu wa amani kwa kumnukuu Rais wa zamani wa Mexico, Benito Juarez aliyewahi kusema palipo na heshima pana Amani. Na kuwa kuheshimu haki za wengine maana yake ni amani.

Suluhu ya kisiasa ya Zanzibar kati ya vyama vya CUF na CCM wakati wa utawala wake pengine ndiyo iliyowafanya waandaaji wa mkutano wa amani kutoka Taasisi ya Amani Duniani (GBF), kumwalika Karume kuhutubia mkutano huo unaofanyika Belfast.

Karume anabebwa na mwafaka wa tatu baada ya kufanya mazungumzo na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CUF na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad na kuunda SUK.

Hapo ni baada ya mwafaka wa kwanza wa 1996 uliosimamiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Chifu Emeka Anyaoku na mwafaka wa pili uliokuwa kati ya Katibu Mkuu wa CCM kwa wakati huo, Philip Mangula na Maalim Seif.

Mbali na kunukuu kauli ya Benito, kwamba penye heshima ndipo ilipo amani, Karume pia amewaambia washiriki wa mkutano huo wa Belfast kwamba kiongozi mwenye maadili lazima awe mpole, anayeweza kujieleza vizuri, anayeongozwa kwa haki na usawa, kuwajibika kwa kasi inayotakiwa, kukiri makosa na kuheshimu haki za kila raia.

Hotuba ya Karume kwa washiriki wa mkutano huo ililenga umuhimu wa uadilifu na ubunifu wa viongozi kwa amani barani Afrika ambapo GPF tangu kuanzishwa kwake imejikita katika kuinua ubunifu na msingi bora kuendeleza ujenzi wa amani duniani.

Karume aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kwamba hivi karibuni alikuwa Kampala nchini Uganda ambako alikutana na Rais Yoweri Museveni na mazungumzo yao yalijielekeza kwenye hoja mbili za kujenga amani na maisha bora kwa wananchi.

Akizungumzia hoja ya msingi ya uongozi wenye misingi ya uadilifu na ubunifu, Karume anasema hoja zote mbili ni muhimu katika kuendeleza amani na kuboresha maisha ya watu.

“Kwa ushahidi, si mimi tu ninayethamini uongozi wa uadilifu na ubunifu ikiwamo umuhimu wa kuijenga amani, mahudhurio yenu kwenye mkutano huu yanaonyesha namna mnavyothamini ujenzi wa amani.

Tumekutana wote hapa kubadilishana mawazo ambayo ni muhimu sana yanayohusu maadili ya uongozi katika kujenga amani endelevu miongoni mwetu, hasa katika uongozi wenye uadilifu na ubunifu,” anasema Karume.

Karume aliweka historia ambapo uhasama wa CCM na CUF uliwekwa pembeni Novemba 3, 2010 alipoapishwa rasmi kushika uongozi wa nchi kwa awamu ya kwanza Dk Ali Mohamed Shein.

Sare za CCM, CUF na vyama vingine zilivaliwa bila kujali itikadi. Mfuasi wa CCM alivaa sare ya CUF na wa CUF alivaa ya CCM au NCCR-Mageuzi.

Historia hiyo ya uvumilivu wa kisiasa ilijitokeza pia kwenye hotuba ya Karume kwa kusema kiongozi mwenye maadili anatawala maeneo yote katika jamii kama ilivyokuwa kwa kiongozi wa kisiasa na wa kijeshi wa Roma ya kale, Julius Caesar.

Caesar au Gaius Julius Caesar anakumbukwa hasa kwa mafanikio mbalimbali yanayoonekana kuathiri dunia hadi leo.

Baadhi ya mafanikio hayo ikiwamo kuheshimika na jina lake kuwa neno kwa ajili ya cheo cha watawala wa Kiroma waliomfuata. Kutokana na badiliko hilo la jina “Caesar” kuwa cheo, lugha mbalimbali zilipokea cheo hicho kama vile Kijerumani (“Kaiser”), Kirusi (“Tsar”) na Kiswahili (“Kaisari” – kutokana na neno la Kijerumani).

Pia, aliunda kalenda ambayo imekuwa msingi wa kalenda ya kimataifa leo (Kalenda ya Juliasi). Kwa heshima yake, mwezi wa saba unaitwa Julai.

Karume anasema historia ya Caesar ambayo inaendelea kugonga vichwa vya habari, kutawala mijadala ya wasomi na maeneo mbalimbali ina muhimu wake hata katika dunia ya sasa ambayo imeendelea kuwa na siasa zinazoyumba, misuguano ya kimaadili, migogoro ya uongozi wa kisiasa, rushwa na uroho wa madaraka.

Anasema kama inavyofahamika siasa ni moja ya shughuli muhimu za kibinadamu inayoongozwa na kanuni, sheria na usawa katika kuvumiliana.

Karume anaendelea kusema siasa inahitaji uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwa wananchi, vyama vya siasa, wabunge, watendaji wa Serikali, mahakama, vyombo vya habari, jumuiya za wafanyabiashara, taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za dini na taasisi za elimu.

Karume ambaye wakati akigombea urais wa Zanzibar kwa mara ya kwanza alitambulishwa kama ‘mtoto wa simba’ kwa maana baba yake alikuwa na msimamo mkali katika uongozi wake na yeye (Karume) alitabiriwa kuwa vivyo hivyo, anasema uaminifu ni heshima katika siasa na vyombo vya umma ni muhimu kwa amani, maendeleo kwa jamii, hasa katika kuinua demokrasia.

Anasema kupitia uaminifu, viongozi wanatakiwa wawe imara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kimaadili katika kukabiliana na changamoto za kisiasa na jamii iliyogawanyika kwa kuweka taratibu za kuaminia na zenye maadili, ikijumuisha uaminifu, ukweli na haki.

Karume anasema viongozi wa kisiasa wanatakiwa kuwa mfano kwa wanaowaongoza, wananchi wao waone uaminifu wao, ukweli na ujasiri huku akisema Afrika ina bahati ya kuwa na viongozi wengi ambao wameonyesha viwango vikubwa vya uongozi wa uadilifu na ubunifu kama vile Samora Machel (marehemu) wa Msumbiji, Kenneth Kaunda wa Zambia, Nelson Mandela (marehemu) wa Afrika Kusini na hakumsahau baba yake Abeid Amani Karume (marehemu) kwamba katika uongozi wake alibadili Zanzibar kiuchumi na kijamii.

Mwasisi huyo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 kwa kuondoa utawala wa kisultani wa Waarabu, Abeid Amani Karume alishika uongozi wa visiwa hivyo vya Unguja na Pemba na kuamuru mwingiliano wa kijamii kwa kuruhusu ndoa kati ya Waafrika na raia wa kigeni.

Pia, ujenzi wa majumba ya Michenzani na mambo mengine ya kiuchumi kama ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya Bwawani na uanzishwaji wa kituo cha kwanza Televisheni ya rangi kwa Afrika.

Anasema Afrika ni bara lililo kwenye mabadiliko lina utajiri wa asili na rasilimali watu, lakini bado linaendelea kuogelea kwenye dimbwi la umaskini, njaa, kipato kisichowiana na usalama mdogo kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi na vurugu zinatokana na migogoro kadhaa.

Karume anasema kwa sasa uongozi wenye maadili ndiyo unaohitajika zaidi kuliko huko nyuma, hasa changamoto za kisiasa, kiuchumi na maendeleo ya kijamii.

Mbali na kuzungumzia mkutano wa ‘kuendeleza amani, usalama na maendeleo endelevu kwa Afrika Mashariki’ uliofanyika Zanzibar 2015 ambao ulisisitiza umuhimu wa uaminifu na heshima kwa kila mmoja, pia alizungumzia uzoefu wake kuhusu Zanzibar ilivyogawanyika kutokana na migogoro ya kisiasa na kwamba ni namna gani uongozi wa uaminifu na ubunifu ulivyoleta amani Zanzibar.

Anasema uzoefu wake alipokuwa Rais wa Zanzibar mgawanyiko wa kisiasa uliwanya wabuni utamaduni wa maelewano kupitia ushirikishwaji wa pamoja kwa njia ya kidemokrasia, ilikuwa ni suluhisho pekee la kisiasa katika visiwani hivyo.

Karume anasema kama kiongozi, alitumia haki na uwakilishi wa wananchi wote kupitia vyombo vyao vya uwakilishi ikiwamo chama chake cha siasa, ilikuwa ni wakati wa kuwa mbunifu, mwenye msimamo, kufikiria malengo ya muda mrefu na kuweka pembeni hisia zake za kisiasa.

“Nina hakika hiyo ilikuwa ni uamuzi sahihi wa kisiasa kwa maslahi ya wananchi.” Anasema Karume huku akimnukuu mshindi wa tuzo ya amani duniani, Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini alisema; “Tunataka watu ambao wapo kwa masilahi ya watu na si kwa masilahi binafsi.”

Nalo, Gazeti la RAI la leo Alhamisi, Machi 15, 2018 limeripoti habari hiyo hiyo kwa kichwa cha habari; KARUME AWAKOSOA VIONGOZI, BALOZI MWAPACHU AMUUNGA MKONO

RAIS mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume amekosoa hatua ya viongozi wengi wa Afrika kukosa uadilifu na uwajibikaji, hatua inayoweza kutowesha amani katika nchi zao.

Kiongozi huyo wa zamani wa Zanzibar ambaye alifanikisha kurejesha amani ya kisiasa visiwani humo kwa kuridhia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, aliwataka viongozi wa Afrika kutambua kuwa siasa ni harakati muhimu na halali za binadamu kwa sababu zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Alisema katika kuendesha siasa safi inapobidi si vibaya ikatolewa nafasi na uwiano sawa kwa masilahi ya makundi mbalimbali ndani ya jamii.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kwa uadilifu na uwajibikaji kutoka kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa, Wabunge, Mahakama, wananchi, tasnia ya habari, asasi za kiraia na hata taasisi za dini.”

Karume aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa Taasisi ya Amani Duniani-Global Peace Foundation (GBF), uliofanyika kwenye ukumbi wa Skainos, mjini Belfast nchini Ireland, Machi 8 mwaka huu.

Katika mkutano huo mada kuu ilikuwa ni “Umuhimu wa uongozi adilifu na wa ubunifu kwa ajili ya amani Barani Afrika.”

Katika hutoba yake hiyo, Rais mstaafu Karume alihimiza utamaduni wa kuaminiana na kuheshimu siasa na taasisi za utawala na kusema kwamba vitu hivi ni muhimu kwa kudumisha amani ndani ya jamii, hususani katika nchi zenye demokrasia changa.

Alisema katika suala la uaminifu ni lazima viongozi wasimame kidete kushughulikia majukumu yao ya kiutawala na maadili hasa katika medani za siasa zenye changamoto nyingi ndani ya jamii zilizogawanyika.

Aliyataja maadili yanayopaswa kusimamiwa na viongozi kwa nguvu zao zote kuwa ni uadilifu, uaminifu na utoaji wa haki.

“Viongozi wanapaswa kuwa waadilifu,lazima wawe wanyenyekevu na wasisite kuonyesha ari yao ya kuifanyia makubwa jamii inayowazunguka, wajitahidi kutokuwa na upendeleo, wawe tayari kuwajibika, kukiri makosa na kuheshimu haki za kila raia.”

Akimnukuu Rais wa zamani wa Mexico, Benito Juarez, Rais mstaafu Karume alisema: “kuheshimu haki za wengine ndiyo amani yenyewe.”

“Viongozi wa kisiasa lazima wawe mfano kwa wafuasi wao ambao wanapaswa kuwaona viongozi wao kama ni waadilifu, wakuaminika na wenye ujasiri.

“Barani Afrika tuna bahati ya kuwa na viongozi wengi walioonyesha viwango vya juu vya uadilifu na ubunifu katika uongozi wao kama vile waasisi wa mataifa yetu Samora Machel wa Msumbiji, Kenneth Kaunda wa Zambia, Nelson Mandela wa Afrika ya Kusini hapa nimewataja wachache tu.

“Na kama ni lazima basi pia nijitaje mimi mwenyewe na marehemu baba yangu Abeid Aman Karume ambaye katika kipindi kifupi tu aliweza kuleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi Zanzibar.”

Alisema suala la uongozi wa uadilifu halitokani na uzoefu wake wa urais wa Zanzibar, bali ni suala ambalo linaendelea kumiliki fikra zake, mazungumzo na wenzake na matumaini yake katika hali ya baadaye ya nchi yake kwa ujumla.

“Si peke yangu ninayethamini uongozi wa adilifu na kufahamu umuhimu wake katika kuijenga amani. Uwepo wenu kwa wingi leo katika mkutano huu unaonyesha umakini wenu mlio nao katika suala hili.

“Tumekutana hapa kupeana na kujadili mawazo muhimu ya uongozi adilifu katika kujenga na kudumisha amani miongoni mwetu, suala la uongozi adilifu limejikita katika jamii zote duniani tangu enzi za Julius Cesar na bado linaendelea kumiliki vichwa vya habari katika vyombo vya habari na kuwa katika mijadala mbalimbali miongoni mwa wasomi na watu wengine.”

Gaius Julius Caesar alikuwa kiongozi wa kisiasa na wa kijeshi wa Roma ya Kale. Anakumbukwa hasa kwa mambo mbalimbali yanayoonekana kuathiri dunia hadi leo

Aidha, Karume alisema Afrika ni Bara lililo katika mageuzi makubwa, lina utajiri mkubwa wa rasilimali za asili na nguvukazi kubwa, lakini bado linajikongoja katika kuuondoa umasikini, njaa na ongezeko la tofauti kati ya walionacho na wasio nacho.

Akizungumzia suala la kukosekana kwa usalama katika nchi nyingi za bara hilo, alisema kunatokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi na vurugu nyingine.

Alisema muda sahihi wa kuondoa changamoto hizi zilizopo chini ya mwavuli wa utawandawazi barani Afrika ni sasa, lakini ili tufanikiwe kwenye hilo kunahitajika kuwepo viongozi waadilifu na wenye utayari wa kuwajibika.

WASHIRIKI WENGINE

Katika mkutano huo uliokuwa na dhamira ya kuimarisha masuala ya amani, Rais mstaafu Karume aliungana na watoa mada wengine 14 kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na wa kisiasa.

Miongoni mwao ni rais wa taasisi ya GBF James P. Flynn, makamu wake Dk. Tony Devine na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Peter Sheridan.

Wengine ni mchungaji Dk. Lesley Carroll, Mchungaji Gary Donegan, Mbunge wa zamani wa jimbo la Belfast Mashariki, mwanaharakati wa haki za lugha Linda Ervine, Mchungaji John Joseph Hayab na mwanaharakati David Holloway.

Wasemaji wengine katika mkutano huo walikuwa ni Mwanasheria wa kimataifa Conor Houston, Shekhe Halliru Abdullahi Maraya kutoka Nigeria, mwanasiasa wa zamani wa Ireland Tina McKenzie, mpigania haki za binadamu Andree Murphy na Mkurugenzi wa GPF nchini Nigeria, John Oko.

BALOZI MWAPACHU

Akizungumzia hotuba ya Karume kupitia mtandao wake ya Twitter, mwanasiasa mkongwe Balozi Juma Mwapachu ameiunga mkono na kuipongeza hotuba hiyo kwa kusema inaelezea hali halisi ya kisiasa na kiuchumi ilivyo Barani Afrika kwa sasa.

Mwapachu ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini pamoja na kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa alisema hotuba hii ingefaa kusambazwa nchini kwani ina umuhimu mkubwa hususani kwa vijana ambao wanahitaji kufahamu vyema kasi ya mabadiliko katika kipindi hiki.

 

Tagsslider
Share: