Habari

Katiba mpya mbadala yaandikwa mafichoni

Mwandishi WetuToleo la 337
5 Feb 2014
Rais Jakaya Kikwete
Maprofesa, majaji wachambua taarifa nyeti za Warioba
CCM sasa kuingia Bunge la Katiba na rasimu mbadala
WIKI takriban mbili kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba, mjadala wa muundo wa serikali tatu uliopendekezwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba mpya umeendelea kupasua vyama vya siasa, Raia Mwema ikielezwa kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeandaa rasimu mbadala ndani ya Bunge hilo la Katiba.

Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili, CCM ni kama vile imetengeneza tume yake ya Katiba mpya inayoshikirisha jopo la maprofesa, majaji na baadhi ya wanasiasa.

Kati ya taarifa wanazotumia kutengeneza rasimu hiyo mbadala ya Katiba ni viambatanisho vya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, viambatanisho ambayo pia walikabidhiwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

Mbali na hao wengine waliokabidhiwa viambatanisho hivyo sambamba na Rasimu ya Pili ya Katiba mpya ni viongozi wengine mbalimbali wa kitaifa, akiwamo Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro.

Ndani ya ‘tume’ hiyo ya CCM aliyepata kuwa mwanasheria mkuu wa serikali (AG) Andrew Chenge, anatajwa kuwamo na inaelezwa kwamba, ‘tume’ hiyo inalenga kuibua mawazo mbadala na yale ya Tume ya Warioba, hususan muundo wa serikali tatu ndani ya Muungano.

Tayari, Rais Jakaya Kikwete, katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 37 ya CCM mkoani Mbeya Jumapili iliyopita alisema msimamo wa CCM ni serikali mbili na anayewapinga anapaswa kuibua hoja mbadala zenye ushawishi na si kutumia mabavu, akisisitiza hoja hazifutwi kwa “kupigwa rungu” bali hufutwa kwa kutumia hoja mbadala zenye mantiki.

“Kinachofanywa na CCM ni kutengeneza mawazo au mapendekezo mbadala yenye mantiki zaidi. CCM haing’ang’anii mwonekano wa sasa wa serikali mbili. Ndani ya mwonekano wa sasa kuna imani kwamba yapo mabadiliko yanayoweza kufanywa ambayo pia yanaweza kuungwa mkono na wapinzani, lakini ni mabadiliko ambayo si ya moja kwa moja kwenda kwenye serikali tatu kama ilivyopendekeza Tume ya Warioba,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Inaelezwa kwamba huenda CCM ikaibua mawazo mbadala wa muundo wa serikali ambayo chanzo chetu cha habari kimeelezea mawazo hayo mbadala kuwa ni “mawazo ya kati, yasiyo na msimamo mkali kuhusu muundo wa Muungano.”

Lakini wakati CCM ikiwa katika juhudi za kuingiza rasimu mbadala kwenye Bunge la Katiba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinashikilia msimamo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.

Katika msimamo wake, CHADEMA hakina mapendekezo mbadala kuhusu serikali tatu, bali kinaungana na yale ya Tume ya Warioba, kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani, hususan vyenye wabunge bungeni.

Hali hiyo inajitokeza katika wakati ambao vyama hivyo vya siasa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vikitaraji kukutana Februari kesho, kujadili nafasi yao katika Bunge la Katiba.

Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Vyama, Jaji Francis Mutungi, vyama hivyo vitakutana kupitia chombo chao maalumu, kinachoitwa Baraza la Vyama vya Siasa, kikiwa ni chombo cha kisheria ambacho wajumbe wake ni viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walioteuliwa kuwakilisha vyama vyao.

Katika hatua nyingine, duru za kisiasa kutoka Zanzibar zinaarifu kwamba tafsiri ya mambo kuhusu serikali tatu au serikali mbili imebadilika, baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa uwakilishi katika Jimbo la Kiembesamaki, ambako Mahmoud Thabit Kombo wa CCM ameshinda baada ya jimbo hilo kuachwa wazi kutokana na kufukuzwa kwa mwakilishi wa awali, Mansoor Himid.

Vyanzo kadhaa vya habari vinabainisha kwamba uchaguzi huo ulibeba tafsiri kubwa kuhusu mijadala mizito ya kisiasa Zanzibar.

Wengi wanasema ushindi wa Kombo ambao msingi wake ni wapiga kura wa ngazi ya chini na si safu ya viongozi wa juu pekee, tafsiri yake ni ushindi wa serikali mbili, ikielezwa kwamba Kombo ni muumini wa serikali mbili na alihojiwa na kuthibitisha hivyo katika Kamati Kuu ya CCM iliyoketi Zanzibar mwezi uliopita kwa ajili ya uteuzi wa mgombea wa jimbo hilo.

Mansoor Himid aliyefukuzwa, aliweka wazi msimamo wake kwamba si tu serikali tatu, bali Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili, akitajwa kuungwa mkono na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

“Matokeo ya uchaguzi huo mdogo maana yake ni kwamba watu wa chini hawana tatizo na hoja za aina ya serikali, bali hizi ni hoja za viongozi wa kitaifa tu. Uchaguzi huu ulikuwa na kambi mbili tofauti na ulikuwa kipimo mbele ya wananchi kwamba kambi ipi inakubalika.

“Kambi ya kwanza ni ile iliyokuwa ya Mansoor. Na unapomwona Mansoor ni dhahiri Karume yupo. Lakini kambi ya pili ni Dk. Shein (Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein) na CCM kwa ujumla, ambamo wamo watu kama kina Seif Khatib na wengineo. Kambi hizi zilikuwa zikipimwa kwa hoja ya serikali tatu, ndani yake madai ya mamlaka kamili ya Zanzibar na nyingine ni hoja ya serikali mbili. Ushindi umekwenda kwa kambi ya CCM,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

– See more at: http://www.raiamwema.co.tz/katiba-mpya-mbadala-yaandikwa-mafichoni#sthash.O1XtdU5c.dpuf

Share: