Habari

Katiba – Tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi

Julius S. Mtatiro
3 hours ago
“”BUNGE MAALUM LA KATIBA; TUMETOKA WAPI, TUKO WAPI NA TUNAKWENDA WAPI.

1. Wajumbe wengi(asilimia 81) kati ya wale 201 walioteuliwa na Rais Kikwete ni viongozi na wanachama waandamizi wa CCM. Tukavumilia na kukaa kimya.

2. Kwenye kutengeneza kanuni za Bunge Maalum CCM walipambana kila kukicha kupitisha kanuni zitakazotetea MFUMO wao – tukatumia nguvu kubwa kuwazuia lakini tulifanikiwa kidogo sana -Tukakaa kimya.

3. Katika kuanza kuzitumia kanuni, Mwenyekiti wa Bunge Maalum kwa shinikizo la wazi la CCM alikiuka kanuni bila aibu, ikapangwa kuwa hotuba ya Jaji Warioba ianze ili aje Rais wa nchi baadaye, jambo hili ni kinyume kabisa na kanuni. Suala hili likaleta mvutano mkubwa sana tukaamua KUJIFANYA HATUTAKI MAKUU, tukaliacha – Tukakaa kimya.

4. Jambo hili lilipokubalika, CCM wakamshinikiza Mwenyekiti wa Bunge Maalum amnyime jaji Warioba muda. Mwenyekiti akatangaza kuwa atampa dkk 60 tu, tukakataa, siku jaji Warioba alipokuja kuwasilisha tukalikwamisha ili aongezewe muda, baada ya mashauriano ya baadaye, ikakubaliwa apewe saa nne.

5. Baada ya uwasilishaji wa Rasimu wa Warioba, Rais Kikwete alikuja na kuivunjavunja na kuweka misimamo ya chama chake dhidi ya maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya katiba. Tukamsikiliza Rais kwa nidhamu kubwa na kuvumilia hatua yake ya juu ya kupinga hadharani rasimu ya katiba ambayo imetokana na maoni ya wananchi ambayo ameyakusanya baada ya kuiunda tume ya Warioba. Tukakaa kimya.

6. Ikumbukwe kuwa hata kwenye kuchagua Mwenyekiti wa Bunge la Katiba CCM walipigania nafasi hiyo na kushinda. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti pia waliipigania wakachukua. Tukakaa Kimya.

7. Jana Mwenyekiti wa Bunge la Katiba aliteua kamati za uandishi na kamati ya Kanuni. Kamati zote hizi mbili, kila moja, mwenyekiti na makamu mwenyekiti walioteuliwa wote ni viongozi wa CCM, Tukakaa kimya. Wenyeviti wa kamati hizi wote wanaingia kwenye kamati ya uongozi ya Bunge Maalum. Tumekaa kimya.

8. Juzi CCM walipokutana kwenye kikao cha wajumbe wa CCM waliamua kuteka kamat zote 12 zitakazojadili sura za Rasimu ya Katiba.

Jana tulipokwenda kwenye uchaguzi wa viongozi wa kamati, wateuliwa wote wa CCM walishinda akiwemo HAMAD RASHID na Dr. Francis Michael ambao pia wamejivika joho la kusimamia maoni ya wananchi huku ukweli halisi ni kuwa wapo ili kusmamia matwaka na Maslahi ya CCM.

Ikumbukwe kuwa, wenyeviti wa kamati hizi 12, wote ni wajumbe wa kamati ya Uongozi ambayo ndiyo dira itakayoongoza kila jambo linaloletwa katika bunge Maalum.

9. Leo, Mwenyekiti wa Bunge Maalum ameteua wajumbe watano ili kuingia kwenye kamati ya uongozi kama kanuni zinavyoelekeza. Jambo la ajabu ni kuwa, kati ya nafasi hizo 5, nafasi 4 zote amewateua wajumbe ambao ni viongozi waandamizi wa CCM akiwemo mwakilishi wa walemavu Amon Mpanju.

Mjumbe mmoja wa walemavu amesimama na kupinga uteuzi wa mwakilishi wao palepale.

Prof Lipumba amesimama na kukataa uteuzi huo, ameeleza si wa haki hata kidogo. Ameeleza alijiunga na siasa ili kutafuta haki za wananchi na umoja wa kitaifa na si vinginevyo. Lipumba amesema kuwa hawezi kutumika kama mhuri.

Kama CCM wana nia njema wasingehodhi nafasi zote katika mchakato wa katiba.

10. Hoja kubwa ya CCM kuchukua nafasi zote za uongozi wa bunge maalum ni “eti” wao ni wengi. Hoja ya ajabu sana hii! Kama hoja ni nani au kundi gani lina idadi gani basi nafasi hizi zingegawanwa kwa mantiki hiyo. Vyama visivyo CCM peke yake vina wajumbe zaidi ya 130, kama hoja ni wingi vyama hivi peke yake vingepewa nafasi 5 kwenye kamati ya uongozi. Badala yake tumepewa nafasi 1 tu a Prof. Lipumba ambayo ameikataa kwa sababu si nafasi ya haki.

11. Tuko hapa kwenye Bunge Maalum kutafuta katiba ya wananchi wa Tanzania, hatuko hapa kutafuta katiba ya chama chenye wabunge wengi kuliko vyama vingine kama anavyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalum Samwel Sitta. Ili tupate katiba ya watanzania wote lazima chama chenye wabunge wengi kitambue wingi wao, na kiutumie wingi huo kuunganisha makundi muhimu yenye idadi ndogo ili kutafuta katiba yenye maridhiano na inayokubalika na makundi madogo na makubwa ndani na nje ya Bunge Maalum.

12. Michakato mingi ya kutafuta katiba mpya inaonesha kuwa vyama vilivyoko madarakani huwa ni chanzo kikubwa cha kuvuruga mchakato wa katiba. Na sbb kubwa ya kuvuruga mchakato husika huwa ni chama dola kutaka kuhodhi na kulinda maslahi yake dhidi ya maslahi ya wananchi. Pamoja na uzoefu huu, bado CCM hawataki kujifunza, wanataka kushinda bila kujali wananchi watapata nini.

ANGALIZO;

Masuala hayo 12 yanaonesha wazi kuwa CCM hawana kabisa nia ya kuona nchi inapata katiba inayokidhi matakwa ya wananchi. CCM wanataka kuchukua kila kitu, wanataka kupata kila kitu, wanataka kuhodhi kila kitu, hawajali wananchi wamesema nini.

Wasidhanie kuwa tulioko hapa Dodoma ni watoto wadogo, tutachukua hatua, hatua stahili kwa wakati muafaka. Idadi yao na wingi wao havina maana katika na juu ya maslahi ya taifa na matakwa na maoni ya wananchi.

MWISHO;
CCM watambue kuwa TUTAKULA nao sahani moja, hatutatumiwa kuwa mhuri wa Maslahi ya chama chao na kwamba katiba mpya siyo hisani yao, ni matakwa halisi ya watanzania na serikali na chama kinachoongoza dola lazima kitii maoni ya wananchi na matakwa ya misingi ya kdemokrasia, na kwa sababu mchakato huu umeshaanza lazima ufike mwisho. “Jini likitoka kwenye chupa, halirudi”(hadithi za Alfu Lela Ulela).

Share: