Habari

KATIBU WA MUFTI ZANZIBAR SHEIKH FADHIL SORAGA ARUSHIWA TINDI KALI

Salma Said, Zanzibar

KATIBU wa Mufti Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amemwagiwa tindikali (Acid) jana kulepekea kuathirika mwili wake ambapo amekimbizwa katika hospitali ya Aghakhan Tanzania Bara.

Tukio hilo limetokea karibu na nyumba yake Mwanakwerekwe majira ya saa 12 asubuhi wakati akifanya mazoezi muda mfupi baada ya kumaliza kusali sala ya Alfajiri.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar ACP, Yussuf Ilemba alisema wakati Sheikh Soraga akifanya mazoezi alitokea mtu ambaye naye alivaa nguzo za kufanyia mazoezi na kumrushia tindikali usoni na kisha kukimbia.

“Kitendo hiki hakifanywi na mtu mwenye akili yake na hivyo na mtu huyo hakuweza kufahamika kwa kuwa kulikuwa gizagiza lakini tunaahidi kumsaka kwa hali yoyote na atafikishwa katika vyomvo vya sheria” alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema ni lazima mtu huyo atatiwa nguvuni na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi katika kutoa taarifa za watu wneye kuendeleza vitendo kama hivyo mitaani.

Mkurugenzi huyo alisema licha ya kuwa kazi ya kuwasaka inaendelea lakini watahakikisha watu wenye kutenda makosa kama hayo watakamatwa na ikiwa ni mtu mmoja au ni vikundi vilivyojitokeza kufanya uhalifu vitachukuliwa hatua na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Tutahakikisha tunawakamata wahalifu wote kwa hali yoyote ikiwa ikiwa kuna mtu ambaye anajishirikisha katika vitendo vya kihalifu tunamkamata kwa kushirikiana na raia wema ambao watatupa taarifa za watu hao katika mitaa” aliahidi Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wakati akizungumza na waandishi wa habari huko katika ofisi ya makao makuu ya jeshi la polisi Migombani.

Sheikh Soraga kabla ya kupelekwa Jijini Dar es Salaam kwa matibabu alifikishwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja na kupatiwa huduma ya kwanza na baadae kuchukuliwa na gari la kubebea wagonjwa na kusafirkishwa hadi Dar es Salaam ambapo atapatiwa matibabu katika hospitali ya Agha Khan.

Tukio la kumwagiwa tindikali Sheikh Soraga ni miongoni mwa mfululizo wa matukio ya kihalifu na ukiukwaji wa haki za binaadamu unaofanyika katika Visiwa vya Zanzibar katika hiki ambacho Zanzibar inatimiza miaka miwili ya serikali ya umoja wa kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa imepunguza matukio ya kihalifu pamoja na ukiukwaji w ahaki za binaadamu baada ya vyama viwili vya CCM na CUF kukubaliana kuzika tofauti zao za kisiasa na kuanzisha ukurasa kwa kuheshimiana na kuendesha siasa za kistaarabu.

Watu kadhaa wakiwemo viongozi wa serikali walikwenda hospitali kumshuhudia Sheikh Soraga na baadae uwnaja wa ndege kabla ya kusafirishwa akiwemo Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari pamoja na mawaziri na maafisa wa serikali.

Muda mfupi baada ya ndege ya serikali kuruka uwanjani hapo akitoa nasaha zake, juu ya tukio hilo, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi aliwataka wananchi kuacha kuchukua sheria mikononi mwao na kuwataka watulie ili haki itendeke bila ya kuonewa mtu.

Sheikh Kaabi alisema vitendo vinavyofanyika hivi sasa vinaashiria dalili mbaya na havina dhamira nzuri hivyo amewataka wananchi kurudi kwa Mwenyeenzi Mungu na kujizuwia kuchukua maamuzi ambayo yanakwenda kinyume na maadili ya dini zao.

“Huu ni mfano mbaya sana kufanywa na watu ambao tumeishi kwa pamoja na sote ni ndugu lakini dalili kama hizo haziashirii wema bali zinashiria sheria kila mmoja atimize wajibu wake kwa kutenda haki, raia atimize wajibu wake kwa serikali na pia serikali itimize wajibu wake kwa raia vitendo hivi vitaondoka” alinasihi Sheikh Kaabi.

Sheikh Kaabi aliwanasihi wazanzibari kurudi kwa Mwenyeenzi Mungu na kuacha kuchokozana kwani kulipizana visasi kunaweza kuleta athari kubwa katika nchi na kusababisha maafa makubwa kama yake ambayo yametokea katika nchi za jirani ikiwmeo Burundi na Rwanda ambapo awali kabla ya vita walianza na chokochoko za kulipizana visasi.

“Tunayo mifano kama hii kule Burundi watu walikuwa wakianza na maneno na kisha kuingiana mwilini lakini baadae katika kugombana kwao wakawa wanalipizana visasi mtu mmoja mmoja na baadae makabila mawili yakawa yanapigana vita na kusababisha maafa makubwa sana …kwa hivyo nasaha zangu turudi na kukaa na kuacha tofauti zetu mambo haya ni khatari katika taifa letu nawanasihi wananchi wote kuacha mambo kama haya” alisema Mufti.

Tokea kuanza kwa mchakato wa katiba hali ya kutokuwepo kwa uvumilivu wa kisiasa imeanza kujirejea upya baada ya hali hiyo kuibuka kwa kuanza kutupiana vipeperushi vya kukashifiana, kutukanana, na hata kupigana na kulipiziana visasi.

Matukio mengine ambayo yanahusishwa na vikundi vibaya vya kihalifu ambavyo vimeibuka katika miezi ya hivi karibuni baada ya kuzuka tofauti kati ya serikali na taasisi za kiislamu zinazoongozwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) kwa kiasi kikubwa vikundi hivyo vimepata nafasi ya kufanya uhalifu.

Tukio la kukamatwa kwa Kiongozi wa Taasisi za Kiislamu hapa Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed kumesababisha vurugu kubwa baada ya wafuasi wake kuingia barabarani na kuharibu miundombinu, hali za serikali na watu binafsi huku wajanja wakipata fursa ya kufanya wizi na uhalifu mkubwa ambapo mafuasi hao wakishindikiza serikali kumuachia kiongozi wao, vurugu ambazo zimechukua siku nne mfululizo na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa mujibu wa serikali ya Zanzibar.

Mbali na kuharibiwa kwa miundombinu lakini pia watu watatu wameripotiwa kufariki katika matukio hayo tofauti ikiwemo Koplo Said Abdulrahman, Salim Hassan Mahaji na Hamad Ali Kaimu ambao wamefariki katika operesheni ya jeshi la polisi ya kuwasaka wahalifu ambapo inadaiwa kijana Hamad alifariki mikononi mwa jeshi la polisi baada ya kupata kipigo na kusababisha kifo chake.

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein na Makamo wake wa kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na viongozi wa dini wamekuwa wakikemea vitendo hivyo vya uvunjifu wa haki za binaadamu lakini bado taarifa za matukio kama hayo zinaripotiwa kila kiukicha na kuhusishwa na baadhi ya vikundi vilivyojitokea kufanya vitendo hivyo lakini pia utendaji kazi wa vikosi vya ulinzi na usalama unalalamikia katika matukio ya ukiukwaji wa haki za raia.

Kufuatia tukio hilo la kutiwa tindikali Sheikh Soraga, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kipokea “kwa mahuzuniko na masikitio makubwa tumepokea taarifa ya tukio la kinyama na la kikatili la kumwagiwa TINDIKALI mwilini kwa Sheikh Fadhil Suleiman Soraga lililotekea leo tarehe 6/11/2012 asubuhi huko Magomeni kwa Mabata”. imesema taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu Salim Bimani.

Bimani amesema tendo hilo ovu lililofanywa dhidi ya Sheikh Soraga limeleta huzuni na simanzi kubwa kwa Wananchi wa Zanzibar na kumshangaza kila Raia.

Aidha Chama cha Wananchi kinatoa pole kwa Sheikh Fadhil, pamoja na familia yake na kwa Mufti wa Zanzibar ambae Sheikh Fadhili ni Katibu katika Ofisi ya Mufti, pia inawaomba familia iwe tulivu katika kipindi hichi kigumu.

“Chama cha Wananchi kinamuombea duwa kwa Mwenyezi Mungu apone haraka ili aendele na majukumu yake katika Taifa hili. Vile vile CUF – Chama cha Wananchi kinawomba Wanachama wake, Wananchi wote kwa ujumla kutojiingiza katika vitendo viovu vinavyoashiria uvunjaji wa Amani Nchini, na kuwataka kuheshimu kauli za Viongozi wao wa Kitaifa zinazosisitiza utunzaji wa Amani ya Nchi yetu”. alisema Bimani katika taarifa yake.

Wakati huo huo chama hicho kimelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili waliohusika na kadhia hiyo wachukuliwe hatua na kufikishwa katika vyombo vya sheria ili sheria ichukuwa mkondo wake sambamba na hilo wametoa wito kwa Wananchi watoe mashirikiano ili kuwafichua wale wote wanaotenda uovu.

Tagsslider
Share: