Habari

Kesi ilofunguliwa na Ali Saleh dhidi ya bodi mpya ya wadhamini

Mbunge Malindi Zanzibar wa Chama cha Wananchi (CUF), Ally Saleh amefungua kesi Mahakama Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) akipinga usajili wa wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.

Wakati huohuo; Mahakama Kuu leo itasikiliza pingamizi la awali la Serikali dhidi ya maombi ya Bodi ya Wadhamini wa CUF ya kutaka ipatiwe kibali cha kumshtaki Msajili wa Vyama vya Siasa, kwa madai kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa yamefunguliwa na bodi iliyomaliza muda wake.

Katika maombi hayo, bodi hiyo inaomba kibali cha kumshtaki Msajili wa Vyama kwa kitendo chake cha kutoa ruzuku kwa chama hicho kambi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba.

Hivi karibuni kambi ya Profesa Lipumba ilitangaza ilitangaza wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini wa chama hicho, huku kikiwaengua wajumbe waliokuwapo awali, waliokuwa wanamuunga mkono, Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Wajumbe wapya wa bodi hiyo ni pamoja na Peter Malibo, Hajira Silia, Azizi Dangesh, Amina Mshamu, Abdul Magomba, Asha Suleimani, Salha Mohamed, Suleiman Issa and Musa Kombo.

Hata hivyo, Saleh katika kesi hiyo anahoji uhalali wa wajumbe hao walioteuliwa na kambi ya Profesa Lipumba na kuidhinishwa na Rita, ambao ni mdaiwa wa tatu mpaka wa 12. Mbali na wajumbe hao wa kambi ya Lipumba, wadaiwa wengine katika kesi hiyo n ya wajumbe walioteuliwa na kambi ya Maalim Seif na majina yao kupelekwa Rita, lakini Rita ikayaweka kampuni.

Wajumbe hao wa kambi ya Maalim Seif ambao majina yao yaliachwa na Rita ni na Abdallah Khatau, Joran Bashange, All Suleiman, Juma Muchi, Mohamed Mohamed na Yohana Mbelwa, ambao katika kesi hiyo ni wadaiwa wa 13 mpaka 18.

Katika kesi hiyo, mbunge huyo anaiomba Mahakama itamke kama mdaiwa wa 3 mpaka wa 12 (wajumbe wa Profesa Lipumba) kwa mujibu wa Sheria chini ya Katiba ya chama hicho ya mwaka 1992 ya toleo la mwaka 2014, wanastahili kuwa wajumbe wabodi ya wadhamini.

Pia, anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wa 13 mpaka wa 18 (Wajumbe wa Maalim waliowekwa kapuni) na ambao pia ni miongoni mwa wajumbe wa bodi ya awali, ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa CUF.

Sambamba na kesi hiyo, mbunge huyo pia amefungua maombi ya zuio, akiiomba mahakama hiyo itoe zuio la muda dhidi ya wadaiwa wote katika kesi hiyo, wala wakala wao kutokujihusisha kwa namna yoyote na masuala chama hicho cha upinzani.

Anaiomba mahakama itoe zuio hilo la muda dhidi ya wadaiwa wote hadi kesi yake aliyoifungua akiomba zuio la kudumu dhidi wajumbe wapya wa bodi hiyo waliosajiliwa na Rita, itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Saleh anayewakilishwa na Wakili Mpale Mpoki, amefungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura akieleza kuwa suala hilo linahitaji kuamuriwa haraka kwa kuwa chama hicho kiko katika mgogoro mkubwa na wa hatari kisiasa, kutokana na Rita kusajili wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini.

Anadai kuwa ikiwa maombi hayo hayasikilizwa haraka maelfu ya wanachama wengine wa chama hicho wataathirika kwa kuwa wanataka kujua ni kina nani ni wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa Cuf.

Kwa mujibu wa hati yake ya kiapo, Saleh anaeleza kuwa Juni 23-27, mwaka 2014, Mkutano Mkuu wa chama hicho uliwateua wajumbe 47 wa chama hicho katika nafasi ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama hicho, lenye mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bodi ya Wadhini wa chama.

Anaeleza kuwa Mach 19, 2017, kutokana na kuisha kwa muda wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, walioteuliwa mwaka 2012, baraza hilo liliwateua Abdallah Khatau, Ali Suleiman, Juma Muchi, Mohamed Mohamed, Yohana Ubelwa, Zumba Kipanduka, Mwanawetu Zarafi, Blandina Mwasabwite na Mwana Masoud, kuwa wajumbe wa Bodi.

Anafafanua kuwa majina hayo yalipelekwa Rita na baadaye Rita ikatoa mrejesho kwa uongozi kwamba wanayafanyia kazi majina hayo na kwamba wangewafahamisha hatima yake.

Saleh anaeleza kuwa wakati huohuo Rita ilipokea maombi mengine kutoka kundi linguine ya kubadili wajumbe wa bodi, ambazo zilionesha kuwa wajumbe wapya waliokuwa wakipendekezwa ni mdaiwa wa tatu hadi wa 12.Kwa mujibu wake, Saleh, wajumbe hao si halali kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho kwa kuwa Baraza Kuu la Uongozi halikuwahi kukaa kupendekeza mabadiliko hayo.

Saleh anadai kuwa kwa kutokuzingatia Katiba ya Chama na Sheria, hatimaye Rita iliendelea na kusajili wajumbe hao wapya kama wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho na bila kuzingatia majina yaliyowasilishwa na Baraza Kuu la Uongozi.

Hivyo anasema kuwa kutokana na usajili huo wa Rita haijulikanai miongoni mwa makundi hayo mawaili ni lipi ni wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa chama waliochaguliwa kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Chama.

Chanzo: mwananchi

Share: