Habari

KESI MOJA YA VIONGOZI WA HARAKATI YA JUMUIYA NA TAASISI ZAKIISLAM ZANZIBAR YAFUTWA.

Viongozi harakati ya Jumuiya na Taasisi za kiislam Zanzibar wamefutiwa mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili na Mahakama ya Wilaya Mwanakwerekwe dhidi ya kesi ya kufanya mkusanyiko bila ya kibali iliofunguliwa Mei mwaka juzi visiwani Zanzibar.

Uamuzi huo umetolewa na Hakim Ame Msaraka Pinja baada ya kukamilika kusikilizwa kesi hiyo na washitakiwa kuonekana hawana hatia katika mashtaka yaliokuwa yamefunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar DPP mapema Mei mwaka jana.

Hakimu Pinja amesema kuwa kwa kuzingatia mashahidi wanne upande wa mashitaka pamoja na washitakiwa wenyewe waliithibitishia mahakama kwamba katika mkusanyiko wao hawakuzungumzia mambo ya dini isipokuwa waliungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema kuwa kwa msingi huo washtakiwa hawakuhitajika kuwa na kibali chochote cha kisheria kabla ya kuandaa mkusanyiko huo kwasababu walikuwa wakizungumzia mambo ya Muungano na kwa msingi huo hakuna shitaka linalowatia hatiani na mahakama imetupilia mbali dai hilo.

Amesema baada ya mahakama kupitia jalada la kesi hiyo,imeonekana washitakiwa hawana hatia,ninawaachia huru kwasababu kosa waliloshitakiwa halikuhitaji kibali cha mufti kabla ya kuandaa mkusanyiko huo”Alisema Hakimu Pinja.

Hata hivyo Hakimu huyo wa mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe alisema kuwa upande wa mashitaka wa Serikali kama haujaridhika na uamuzi wa mahakama hiyo unaweza kukata rufaa mahakama ya mkoa ndani ya siku 30 tokea kutolewa kwa uamuzi huo.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Amiri mkuu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar Samahatu Sheikh Farid Hadi Ahmed ,maustadh Mussa Juma Issa, Haji Sadifa Haji,Suleima Juma Suleiman,Fikirini Mjawaliwa Fikirini na Katibu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara yakiislam Zanzibar Al-ustadh Abdallah Said Ali. .

Washitakiwa hao walifunguliwa mashitaka kwa kufanya mihadhara ya kiislam bila kibali cha mufti kinyume cha kifungu cha 6(1)(2) cha kanuni za kuidhinisha na kuratibu mihadhara zinazotengenezwa chini ya kifungu 15(1) ya sheria Namba 9 ya mwaka 2001 ,kifungu cha 10(1)(c) na kifungu cha 14(2) ya sheria namba 9 ya mwaka 2001.

Ilidawa kuwa bila ya halali Mei 26 mwaka juzi majira ya saa 3;30 huko katika viwanja vya Lumumba wilaya ya Mjini Unguja washitakaiwa walifanya mihadhara ya kiislam bila ya kuomba kibali cha mufti wa Zanzibar.

Tagsslider
Share: