Habari

Kesi nne kutikisa Mahakama ya Afrika Mashariki

Moja ya kesi hizo ni ile inayohusu Muungano wa Zanzibar na Tanganyika (unaofahamika kwa jina la Muungano wa Tanzania), itakayosikilizwa na majaji watatu.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, tangu ulipoanzishwa Aprili 26, 1964 umekumbwa na manung’uniko mengi kuhusu dhuluma (maarufu KERO za Muungano) kutoka kwa watawala wa Tanganyika dhidi ya nchi ndogo ya Zanzibar, yenye watu takriban milioni moja na nusu.

By Filbert Rweyemamu – Mwananchi
Tuesday, March 6, 2018

Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) imeanza kusikiliza kesi zilizofunguliwa na watu binafsi pamoja na mashirika mbalimbali dhidi ya nchi wanachama wa jumuiya na zinatarajiwa kuuanza kusikilizwa hadi Machi 29 mwaka huu.

Kati ya kesi zinazotarajiwa kuvuta hisia za watu wengi ni kesi namba 7 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Rashid Salum Adiy na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Muungano itakayosikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Monica Mugenyi.

Majaji wengine ni Fakihi Jundu na Charles Nyawello watatoa uamuzi wa awali wa mpeleka maombi aliyetaka mahakama hiyo ihamishie kwa muda kikao chake Zanzibar ili kuwawezesha wananchi wengi kuhudhuria.

Taarifa iliyotolewa leo kwa waandishi wa habari na Msajili wa Mahakama hiyo, Yufnalis Okubo ilisema pia kesi namba 2 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) itasikilizwa Machi 13 mwaka huu.

Walalamikaji wengine ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) huku mahakama hiyo ikitarajiwa kusikiliza maelezo ya awali juu ya hoja zitakazobishaniwa .

Kesi hiyo ambayo waleta maombi wanadai sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 inaminya uhuru wa kupata na kutoa habari hivyo kukiuka Itifaki iliyoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ibara ya 6,7 na 8 kwa pamoja zinazotoa haki hizo.

Katika hatua nyingine Mahakama hiyo pia imesema Machi 14 mwaka huu itasikiliza kesi namba 15 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Baraza la Serikali ya Kijiji cha Ololosokwan wilayani Ngorongoro na watu wengine watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa na majaji watano wakiongozwa na Jaji Monica Mugenyi, Dk Faustine Ntezilyalo, Fakihi Jundu, Audace Ngiye na Dk Charles Nyawelo.

Walalamika wanadai haki zao kukiukwa kwa kuhamishwa kwa nguvu kwenye kijiji chao chenye hati halali za usajili.

Mawakili wawili, Donald Deya na Nicholaus Opiyo wa taasisi ya Pan African Lawyers Union (Palu) wanawawakilisha walalamikaji ambao ni vijiji vinne ambavyo ni Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo na Arash.

Pia, kesi namba 7 ya mwaka 2016 inayotarajiwa kusikilizwa Machi 22 mwaka huu iliyofunguliwa na Mhariri Mtendaji wa Mseto & Hali Halisi Publishers Limited dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakati huo huo, Kalunde Jamal wa Gazeti la Mwananchi la leo Ijumaa, Machi 6, 2018 ameandika kwamba, kesi za kikatiba kuanza kusikilizwa mwishoni mwa wiki hii.

Mashauri mawili ya kikatiba yaliyofunguliwa na umoja wa wanaharakati wa kudai demokrasia Tanzania yataanza kusikilizwa Ijumaa Machi 9, 2018 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Mashauri hayo ya kikatiba yalifunguliwa katika mahakama hiyo na umoja huo kwa kushirikiana na wanasheria kupinga namna demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa kujieleza na kukusanyika unavyokiukwa hapa nchini.

Pia, mashauri hayo yalilenga kuhoji namna utendaji wa vyombo vilivyoundwa kwa mamlaka ya kikatiba vinavyoikiuka katiba hiyo.

Mratibu wa Umoja huo Dk Makongoro Mahanga amesema kesi hizo zitatajwa Ijumaa mahakamani hapo, kuanzia saa tatu asubuhi.

Amesema shauri namba 6/218 lililofunguliwa na Bob Chacha Wangwe, akisimamiwa na Wakili Fatuma Karume kuhusu Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi litatajwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu.

Dk Mahanga amewataja majaji hao kuwa ni Jaji Wambali JK, Jaji Mwandambo J na Jaji Teemba J.

Amesema shauri namba 4/2018 lililofunguliwa na Francis Garatwa, Baraka Mwango na Allan Bujo ambao wanatetewa na Wakili Jebra Kambole kuhusu Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya vyama vya siasa litatajwa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Wambali JK, Jaji Sameji R na Jaji Teemba J.

“Wananchi wapenda demokrasia ya kweli ni vema na busara kuhudhuria na kufuatilia mashauri haya yatakayokuwa yakiendelea kunguruma Mahakama Kuu, ”amesema Dk Mahanga.

Share: