Habari

Khalifa asema CUF kitashinda U-rais wa Zanzibar 2020

Amani, Zanzibar
Jumamosi, Aprili 13, 2019

CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimesema kitaibuka mshindi wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu hapo mwakani 2020 kwa sababu kina mikakati imara na kinakubalika kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Sulemain Khalifa akizungumza Jumamosi, Aprili 13, 2019 Amani, mjini Zanzibar katika mkutano wa ndani na wanachama na viongozi wa chama hicho, alisema kwa sababu wana mikakati imara inayokubalika kwa wananchi hawana shaka na ushindi huo.

Katika hatua nyingine alisema wakati umefika wa kupingana na vitendo vya udhalilishaji na wananchi wasikubali tena kudhalilishwa na wawafikishe kwenye vyombo vya sheria wahalifu.

Hata hivyo, Khalifa alisema kwa sasa mikakati zaidi inaandaliwa kukijenga upya chama hicho ikiwemo kuendelea kuyadhibiti matawi yote ya chama hicho.

Alisema siasa isiwe sehemu ya chuki na kila mtu yupo huru kufanya siasa katika chama anachokitaka. Kadhalika alisema hana shaka ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2020 na wanajipanga kuweka mazingira ya chama hicho sawa zaidi.

Khalifa, Katibu Mkuu wa CUF anayeonekana kukwamisha ndoto za Wazanzibari kupitia chama hicho, akizungumza kuhusu baadhi ya wanachama na viongozi kuhama alisema, bado hawajatetereka na kwamba chama chao kitakua salama wakati wote.

“Watuachie chama chetu kama wafuasi na sisi tunao na sisi si majambazi ‘kama wao’, hivyo tufanye siasa kwa amani na utulivu,” alisema Khalifa ambaye hana mvuto mbele ya macho ya Wazanizbari waliyochoshwa na utawala wa CCM.

Khalifa alisema anafahamu kwa kina wanaoshawishi watu (bila kuwataja majina) kuwa wana mkakati maalum wa kuiingiza Zanzibar kwenye machafuko ili wapate maslahi yao.

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Abbas Juma Muhunzi alisema chama hicho kiliingia kwenye mgogoro baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kutofahamu dhamira ya Profesa Lipumba kufuatia kujiuzulu kwake.

Muhunzi ambaye kuanzia baba yake na familia yake yote imemsutia chama hicho cha CUF, alisema kwa sababu Maalim Seif alishindwa kufahamu dhamira ya Profesa Lipumba, imepelekea chama hicho kuwa na mpasuko mkubwa.

Alisema dhamira ya Profesa Lipumba ambayo ilikua ni kulinda heshima yake ikapelekea chama hicho kuwa na mpasuko mkubwa ambao matokeo yake kimegawanyika.

Muhunzi amesema wakati umefika kwa viongozi wa sasa na wanachama kukataa kubaguliwa na kutenganishwa, kilichobaki wafanyekazi kwa umoja wao.

Share: