Habari

KIBAKI AMTEUA JAJI RAMADHAN KUMCHUNGUZA NAIBU JAJI MKUU – KENYA

NAIROBI, Kenya

RAIS Mwai Kibaki wa Kenya amemteua aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhan kuongoza jopo la majaji watakaochunguza kashfa inayomkabili Naibu Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Nancy Baraza.

Jaji Baraza ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi na Rais Kibaki, anatuhumiwa kumtishia maisha kwa bastola mlinzi wa duka moja kubwa mjini Nairobi, Rebecca Kerubo katika mkesha wa mwaka mpya.

Wajumbe walioteuliwa kwenye jopo hilo ni Profesa Judith Behemuka, Philip Ransley, Surinder Kapila, Beuttah Siganga, Grace Madoka na Profesa Mugambi Kanyua.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Ikulu ya Kenya imeeleza kuwa, Rais Kibaki alisema wakati wa uchunguzi huo, Baraza hataendelea na majukumu yake katika Idara ya mahakama. “Kwa wakati huu, Mheshimiwa Jaji Nancy Makokha Baraza, Naibu Jaji Mkuu, Mahakama Kuu ya Kenya, amesimamishwa kazi mara moja kwa mujibu wa kifungu cha 168 (5) cha katiba,” alisema Rais Kibaki katika taarifa hiyo.

Kibaki alisema kwamba, katika kipindi ambacho Jaji Baraza atakuwa  amesimamishwa kazi, atakuwa akipata nusu mshahara hadi pale uchunguzi utakapokamilika na kufahamika kupitia mapendekezo ya jopo kama atarejeshwa kazini au aachishwe kazi.

Kuundwa kwa jopo hilo kumetokana na mapendekezo yaliyowasilishwa kwa Rais Kibaki na tume inayoshughulika na masuala ya Idara ya Mahakama ua nchi hiyo yaliyotaka  Jaji Baraza asimamishwe kazi na uchunguzi juu ya mwenendo wake kufanyika.

Jaji Ramadhan alistaafu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania Desemba, 2010 kwa mujibu wa sheria na nafasi yake ikachukuliwa na Jaji Mohamed Chande Othman.

Kenyatta ajiuzulu uwaziri wa Fedha  Wakati huohuo, Naibu Waziri Mkuu wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Muthaura wamejiuzulu nyadhifa zao.

Kenyatta na Muthaura, wamechukua hatua hiyo siku chache baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuwaona wana kesi ya kujibu katika shtaka kuhamasisha vurugu na kusababisha vifo vya watu wengi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Kenya jana ilisema kuwa, Rais Kibaki ameridhia uamuzi wa Kenyatta kujiuzulu na amemteua Robinson Githae kuzibaa nafasi yake.  Awali Githae alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jiji la Nairobi.

Kenyatta amejiuzulu wadhifa huo siku chache baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kumwona ana kesi ya kujibu kutokana na machafuko yaliyotokea mara baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu wengi.

Mbali na Kenyatta, Rais Kibaki pia amekubali kujiuzulu kwa Muthaura na nafasi yake imezibwa na Francis Kimemia.

Share: